Kinachofanya Wanafunzi Wasielewe Wanachokisoma

PICHA: SciTech Daily


Ujifunzaji (learning) ni mchakato wa kupata uzoefu mpya katika maeneo makubwa matatu. Kwanza, kubadili namna mtu anavyofikiri. Maarifa mapya huja na uzoefu mpya unaobadilisha uelewa wa mambo.

Kwa kulielewa hilo, mwalimu mzuri hufanya kazi ya kumwezesha wanafunzi wake kupata uelewa mpya wa mambo. Mwanafunzi anayejitambua, naye pia kwa upande wake, husoma akilenga kuelewa.

Mara nyingi mwanafunzi anayeelewa anakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufaulu kuliko mwanafunzi anayetegemea kukariri nadharia.

Hata hivyo, uelewa pekee si kipimo kizuri cha ujifunzaji. Lazima mabadiliko yanayotokea kwenye ufahamu wa mtu yajidhihirishe katika namna mpya ya kuyatazama mambo.

Kwa mfano, mtu anapoelewa hatari ya kunywa maji yasiyo safi na salama, tunatarajia mtazamo wake dhidi ya unywaji wa maji yasiyosafi na salama utabadilika.

Kubadili mtazamo pia haitoshi. Lazima mtazamo huo ulete mabadiliko katika maisha ya mtu. Huwezi kuwa na mtazamo hasi na maji yasiyo safi na salama na bado ukaendelea kunywa maji yasiyo safi na salama. Tunategemea uanze kuchemsha maji, kunywa maji unayojua ni safi na salama kama kipimo cha juu cha ujifunzaji.

Kwa hiyo ili tuwe na hakika mtu amejifunza jambo, lazima tujiridhishe kwanza kama alielewa. Bila kuelewa, hatua mbili zinazofuata hazitawezekana.

Kujifunza namna ya kujifunza

Tangu tunapozaliwa, mchakato wa kujifunza unaanza. Tunajifunza wapi maziwa ya mama yanapatikana; nani anatupa mahitaji yetu na namna gani tunaweza kupata kile tunachokihitaji. Ujifunzaji huu unaratibiwa na ubongo na hautegemei jitihada zozote.

Lakini kadri tunavyokua, mahitaji yetu yanakuwa makubwa zaidi. Tunaanza kulazimika kujifunza mbinu za kujifunza ili kupata mahitaji yetu.

Mfano, unapomtuma mtoto wa miaka mitano dukani, upo uwezekano akarudi na kitu kingine tofauti na kile ulichomtuma. Umbali kutoka nyumbani kwenda dukani unatosha kumfanya asahau maelekezo uliyompa.

Mtoto huyu anaweza kujifunza namna ya kukumbuka kwa kuimba wimbo unaotaja bidhaa alizotumwa. Kama alitumwa kiberiti, unga na sukari, mtoto huyu anaweza kwenda dukani akiimba ‘kiberiti, unga na sukari’ mpaka atakapokabidhiwa bidhaa hizo na kuondoka dukani. Akiweza, mtoto huyu anakuwa amejifunza mbinu za kujifunza kukumbuka.

Ndivyo ilivyo hata katika masomo. Kuna mambo mengi ambayo ili mwanafunzi ayaelewe analazimika kujifunza namna ya kujifunza. Katika makala haya, tunaanza kwa kutazama sababu kubwa za wanafunzi kushindwa kuelewa yale wanayojifunza.

Kutokufurahia unachokisoma

Huwezi kuelewa kitu kama huoni thamani yake. Kila kinachoingia kwenye ufahamu wa mtu, kinapimwa katika mizania ya umuhimu wake. Kinachoonekana kuwa na manufaa kinafanyiwa kazi wakati kile kisicho na umuhimu kinachukuliwa kama usumbufu.

Unapojihisi huelewi masomo, anza kwanza kwa kujiuliza kama kweli unapenda hicho unachokisoma.

Unaweza kuwa huzielewi hesabu kwa sababu tu ufahamu wako unazichukulia hesabu kama usumbufu usio na sababu. Usichokipenda, kwa hakika ni vigumu akili yako kupoteza muda kukielewa.

Pia, yapo mazingira yanaweza kukufanya usifurahie kitu kwa sababu tu una hofu. Kwa kawaida hofu huchosha akili. Mwanafunzi mwenye hofu hawezi kufikiri vizuri kwa sababu akili yake hutumia nguvu nyingi kupambana na kile anachokiogopa. 

Kwa mfano, hofu kwamba unaelekea kufeli, hofu ya aina ya adhabu utakayopata ikiwa utafeli, hofu ya kuwakatisha tamaa wanaotarajia ufaulu, ni baadhi ya mambo yanayoweza kuifunga akili isielewe kitu. Kujaza ufahamu wako hofu kunanyonya nguvu ya kuelewa kile anachotamani kukielewa.

Kusoma mambo kijuu juu

Ukiwasikiliza wanafunzi wengi utagundua wengi huamini wanaelewa wakati ule wanaposoma lakini wanapopewa mtihani wa yale yale waliyojifunza, ndipo wanagundua walikuwa wanajidanganya.

Hapa kuna mambo mawili. Kwanza, kuna kusahau unayoyasoma. Lakini pili, inawezekana umeshindwa kutathimini uelewa wako kadri unavyosoma.

Kinachochangia kukufanya uamini unaelewa, mara nyingi ni njia za mkato unazotumia kutafuta matokeo ya haraka. Kwa mfano, badala ya kusoma kitabu kwa utulivu, unaamua kuchagua njia rahisi kama kusoma ‘summary’ ili uwahi ‘kuelewa’. Njia hii ya mkato, hata hivyo, inaweza kuonekana inalipa kwa haraka lakini matunda yake yanaweza kuwa ya muda mfupi.

Wanafunzi wengi hawana utamaduni wa kusoma kitu kwa undani. Hili haliishi sekondari. Hata kwa ngazi aya chuo kikuu hali inaweza kuwa mbaya zaidi. Tabia ya kupenda njia za mkato ili ‘kuelewa’ huwafanya wanafunzi wengi waishie kujua dondoo za kitu badala ya kukijua kitu chenyewe.

Hatari ya usomaji huu wa kijuu juu, hata hivyo, ni sawa na mtu anayeandika kwenye mchanga, maandishi yanaonekana leo, kesho hayafamiki yalikoelekea.

Kusoma mambo mengi kwa wakati mmoja

Nakumbuka nilipokuwa kidato cha 6 hatukuwa na mwalimu wa Baolojia. Hali hii ilitufanya muda mwingi tuwe na wasiwasi na hatma yetu. Hofu hiyo ya kuanguka mtihani ilifanya tuendeshe mikesha darasani. Hakuna wakati wowote katika masaa 24 ya siku darasa lilikosa mwanafunzi. Tuliingia darasani kwa ‘shift.’  

Walio darasani walilazimika kuwaamsha waliokuwa wamelala usingizi wa mang’amung’amu. Wengine shauri ya kuota wanafeli, walijikuta wakiamka muda mfupi baada ya kulala. Hapakuwa na nafasi ya kulala isipokuwa kufumba macho ukingoja kukurupushwa na ndoto ya mtihani wa taifa uliokuwa njiani.

Usomaji huu, kwa kweli, haukuwa na tija. Tulipokutana kwa ajili ya majadiliano darasani, kila mtu alikuwa anakuja na uelewa wake. Wengine waliishia kusema ‘walimeza’ na hawana maelezo ya ziada.

Wakati mwingine mabishano yalikuwa makali kiasi kwamba mijadala ilivunjika bila taarifa ili watu wakaendelee kukesha kuona wapi mambo yameharibikia.

Wanafunzi wengi wanasoma kwa mtindo huu. Pengine kwa kuhisi hana muda wa kutosha, mwanafunzi anasoma mada nzima kwa mkao mmoja. Wengine hukaa na makaratasi pembeni wakinukuu yale wanayoyasoma kwenye vitabu.

Tatizo la kusoma kwa kurudia rudia ni kukutia moyo kwamba unaelewa kwa sababu tu unaweza kurudia yaliyoandikwa kwenye kitabu. Unapoona ‘unatiririka’ hoja moja baada ya nyingine unajinyoosha kwa matumaini. Taabu inakuja pale unapoulizwa swali linalovuruga kile ‘ulichotiririka’ nacho usiku kucha.


Mbinu kama hii ni upotevu wa muda na nguvu bure. Huwezi kuwa mwanafunzi mwenye tija kwa kutumia masaa mengi ‘ukitiririka.’ Lazima kujifunza mbinu zenye tija zitakazokufanya uelewe kile unachokisoma. Tutajadili suala hili katika makala inayofuata panapo uzima.

Maoni

  1. Wooooow asante sana...nimependa namna yako ya utoaji mafunzo kwa mifano thabiti inayomfanya msomaji asikate tamaa ya kutaka kujua kitu ulicho andika.Hii ni kwa sababu ya uhalisia uliopo

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?