Fikiria Yafuatayo Unapoomba Nafasi ya Kujiunga na Chuo Kikuu
PICHA: HuffPost |
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU)
imeviruhusu vyuo vikuu hapa nchini kuanza zoezi la kupokea maombi ya wanafunzi
kwa mwaka wa masomo wa 2017/2018. Katika kufanikisha zoezi hilo, tume
imewaelekeza wanafunzi wanaofikiri wana sifa za kujiunga na elimu ya juu, kutuma
maombi yao kupitia vyuo husika tofauti na ilivyokuwa awali. Kabla ya utaratibu
huu mpya, wanafunzi walituma maombi kupitia mfumo wa udahili wa pamoja uliokuwa
ukiratibiwa na tume yenyewe.
Kwa hakika mchakato huu wa
udahili una umuhimu mkubwa kwa wanafunzi. Maamuzi ya aina ya programu ambayo
mwanafunzi ataichagua na kisha kuisomea endapo atapata nafasi, kwa kiasi
kikubwa, inaamua mustakabali wake wa kazi na ajira.
Bahati mbaya maamuzi haya muhimu,
mara nyingi, hufanyika bila tafakari ya kina, pupa na kufuata mkumbo. Hatima ya
yote ni mwanafunzi kuwa kwenye hatari ya kupoteza ndoto zake za maisha.
Naelewa changamoto hii kwa sababu
na mimi yalinikuta. Nilipokuwa nafikiri nikasome nini chuo kikuu, nilipata
shida ya kujua ninataka nini. Niliongozwa na maoni ya marafiki, walimu na watu
wa mitaani. Matokeo yake hayakuwa mazuri. Baada ya miaka kadhaa ya kusoma
nilichokisoma, bado nilijisikia kama mtu aliyepotea. Ilinilazimu kufanya
maamuzi magumu kurudi kwenye njia yangu nilipopata fursa ya kusoma shahada ya shahada
ya pili.
Kwa vijana wengi, kama
nilivyokuwa mimi, maamuzi ya nini akasome chuo cikuu hutegemea maoni ya watu
ambao wakati mwingine hawana taarifa za kutosha kumsaidia kufanya maamuzi
sahihi. Makala haya yanalenga kumsaidia kijana, na hata mzazi, anayejiandaa
kwenda kusoma. Tunaangazia mambo manne makubwa ya kuzingatia katika mchakato
huu.
Una nini ndani yako?
Kila mtu ameumbwa kwa upekee wake.
Ndani ya kila mtu kuna uwezo unaomtofautisha na binadamu wengine. Uwezo huu
ndio unaobeba mafanikio ya mtu. Ni muhimu uwe na hakika kitu gani hasa ambacho Mwenyezi
Mungu amekihifadhi ndani yako. Maamuzi yoyote unayoyafanya hivi sasa ni vyema
yahakikishe elimu utakayoipata inakuza kitu hicho kilichomo ndani yako.
Bahati mbaya vijana wengi huwa
hawatumii muda wa kutosha kujitambua wana kitu gani ndani yao. Kutokujua wao ni
akina nani kunawafanya watumie muda mwingi kusikiliza maoni ya watu, kujua nini
kinalipa vyuoni, soko linataka nini na matarajio ya jumla ya jamii.
Sababu hizi ni za muhimu lakini haziwezi
kukusaidia. Ingawa kwa sasa unaweza kuwa na msisimko wa kusoma fani unayofikiri
itakuletea heshima kwa jamii, baada ya muda hutaona faida yake. Sababu kubwa ni
kwamba elimu isipokuza kile kilichomo ndani yao, haiwezi kukusaidia. Jitahidi
kujitambua kabla kujafanya maamuzi ya nini ukasome.
Changamoto, hata hivyo, ni kwamba
wakati mwingine kile tunachofikiri kiko ndani yetu kinaweza kuwa kimeumbwa na
matarajio ya watu. Ni muhimu kutafuta ushauri makini kwa wataalam wakusaidie
kujitambua.
Unataka kufanya nini baadae?
Sambamba na kujua kuna nini ndani
yako, ni muhimu kujua kwa nini unataka kusoma. Usisome tu kwa sababu na wewe
unataka uonekane msomi. Fahamu kwa yakini lengo lako la kwenda chuo. Je, unataka
kuajiriwa baada ya masomo au unalenga kujiajiri?
Ukweli ni kwamba tunatofautiana.
Ni makosa kufikiri watu wote wanaweza kujiajiri. Kwa wakati wowote, kokote,
bado watakuwepo watu ambao mafanikio yao yatapatikana kwenye ajira. Hawa, hata
ungewawekea mazingira ya kujiajiri, bado furaha yao inatimilika kwa kufanya
kazi chini ya watu wengine. Hakuna ubaya kutaka kuajiriwa na usikatishwe tamaa
na watu.
Ikiwa unataka kuajiriwa baada ya
masomo, lazima ulenge kusoma fani zinazokuelekeza kwenye kazi mahususi. Ningependa
kuziita fani hizi ‘kozi za kazi,’ mfano sheria, uinjinia, ualimu, uhasibu,
uandishi wa habari, udaktari na nyinginezo. Ukisoma ualimu, unasomea kazi
kuliko kusoma program za jumla ambazo wakati mwingine hazieleweki zinakuandaa
kufanya kazi gani hasa.
Pia, ikiwa lengo lako ni
kujiajiri, lenga kusoma fani itakayokusaidia kupata maarifa yatakayokusaidia kusimama
kwa miguu yako kukujengea uwezo thabiti wa kutatua matatizo fulani kwenye
jamii.
Soma kozi zinazokujengea ujuzi
fulani utakayokuwa na tija kwenye shughuli zako. Mfano, ukisoma fani kama uendeshaji
wa biashara, ufundi wa kompyuta, utunzaji wa mazingira, lugha, kilimo, sosholojia,
uwezekano ni mkubwa utaandaliwa kuwa mjasiria mali kuliko kusomea fani
zinazokuandaa kufanya kazi ofisini.
Pamoja na hayo, ieleweke kwamba
elimu ya chuo kikuu hailengi kukuandaa kujiajiri moja kwa moja. Kazi ya kuyageuza
maarifa unayoyapata darasani yewe ufanisi wa kazi inabaki kuwa ya kwako
mwenyewe. Unahitaji kuwa na mtazamo mpana tangu unapoanza chuo ili upate kile
unachokihitaji kulingana na mahitaji yako.
Umaarufu wa shahada
Kuna rafiki yangu mmoja aliwahi
kuomba kusoma shahada moja kwa sababu tu ilikuwa na jina zuri kutamkika.
Alipomaliza wiki ya kwanza darasani, akagundua haimfai. Alijaribu kufanya
mipango ya kubadilisha, lakini
haikuwezekana.
Fikiria mwanafunzi kama huyu
anayesoma kitu asichoona kinahusianaje na maisha yake ya baadae. Kwanza,
hatakuwa na bidii, hatajituma na hatakuwa na ubunifu wowote kwenye fani husika.
Mtu kama huyu akimaliza chuo
anaweza kuulalamikia mfumo wa elimu kwa sababu ni kweli kile alichokisoma
hakijamnufaisha kibinafsi. Atajikuta ametumia muda mwingi kusoma mambo
yasiyohusiana na wito wake, ambayo kwa bahati mbaya hayawezi kusaidia kutatua
tatizo lolote kwenye jamii, na mbaya zaidi, hayawezi kumpa ajira. Mtu huyu anaweza
kuishia kuwa mchuuzi wa bidhaa mitaani, na kuyalaani madarasa kwa kosa
alilolifanya yeye mwenyewe.
Naelewa yapo mazingira ambayo mtu
anaweza kujikuta akisoma kitu ambacho hayawahi kukifikiri. Kuna shinikizo la
wazazi, kuna shinikizo la kupata mkopo na sababu nyinginezo. Katika mazingira
kama haya, ni vyema kuelewa kwamba bado unaweza kutumia shahada usiyoipenda
kufikia kile unachokipenda. Ndivyo maisha yalivyo nyakazi nyingine.
Ukasome chuo gani?
Nimebahatika kusoma na kufanya
kazi kwenye vyuo vikuu tofauti. Nilichokibaini ni kwamba si kila king’aacho ni
dhahabu. Vipo vyuo vinasifika kwa majina lakini sifa hizo hazitafsiriki kwenye
ubora wa kile wanachokipata wanafunzi. Usiongozwe na historia ya vyuo
vilivyowahi kuwa bora kwa siku za nyuma.
Jina la chuo linaweza kuwavutia
watu, na wakati mwingine kukujengea ufahari mtaani lakini kamwe halitakuhakikishia
utendaji bora wa kazi. Katika siku za leo, ujuzi ni jambo la maana zaidi.
Kazini watu hawatajali ulisoma wapi. Watataka kuona matokeo ya kile
ulichokisoma. Hilo ndilo la muhimu. Usipumbazwe na mashindano ya chuo gani ni
bora kihistoria.
Pia, ni muhimu kuelewa kuwa kila
chuo kina fani inayokitambulisha vizuri kuliko fani nyinginezo. Chuo kinaweza
kuwa maarufu katika kuwaandaa wanasheria mahiri, lakini kisiweze kuwaandaa
walimu bora. Ni muhimu kufanya utafiti kwa kuongea na watu wanaoaminika ili
ufanye maamuzi sahihi.
Hata hivyo, bado ubora wa jumla
wa chuo ni jambo la muhimu. Hakikisha chuo unachokwenda kusoma, mbali na kuwa
na wahadhiri wa kutosha na wanaojituma, miundomsingi, ubora wa afunzo kwa vitendo, usimamizi wa karibu wa wanafunzi, hakikisha pia kinaweza kukupa mazingira ya kukulea kimaadili.
Makala haya yalichapishwa kwenye gazeti la Mwananchi, Ijumaa ya tarehe 4 Agosti, 2017.
Daah hakika yame tukuta wengi,
JibuFutaHaya mambo mwalimu Yametukuta wengi na bila shaka kila makala unayoandika Mr Christian Bwaya huwa nakuwa nishakurupuk kwa hulka za Wanajamii,,,,, na kumbuka kuna makala ushawahi eleza kuhusu Mambo ya kuzi gatia kabla ya kuacha kazi nilijikuta nimefanya makosa kibao zaidi Ahsante kwa hilo ngoja niwape sharing watanzania wengine
JibuFutaHaya mambo mwalimu Yametukuta wengi na bila shaka kila makala unayoandika Mr Christian Bwaya huwa nakuwa nishakurupuk kwa hulka za Wanajamii,,,,, na kumbuka kuna makala ushawahi eleza kuhusu Mambo ya kuzi gatia kabla ya kuacha kazi nilijikuta nimefanya makosa kibao zaidi Ahsante kwa hilo ngoja niwape sharing watanzania wengine
JibuFuta