Wanavyokufahamu Watu Ndivyo Ulivyo?
‘Jamaa ana madharau sana!’ alilalamika Lazaro.
‘Nani?’ alihoji Msafiri.
‘Si Peter?’
Uso wa Msafiri ulionesha mshangao. Hakufikiri Peter anaweza kuwa
na dharau kama Lazaro anavyodai. Msafiri anamfahamu Peter mwenye tabia nyingine
kabisa. Kwake, Peter ni rafiki, mtu wa
watu asiye na neno na mtu.
‘Peter huyu huyu ninayemfahamu mimi?’ Msafiri aliwaza kimya
kimya akikumbuka namna Peter alivyomsaidia hivi majuzi alipokuwa na shida ya
fedha. Hakuna rafiki aliyemsaidia isipokuwa Peter.
Hakupata kufikiri hata mara moja kwamba Peter angeweza kuwa
dharau akaona aulize imekuwaje, ‘Kwa nini umefikiri hivyo Lazaro?’
‘Jamaa ana kiburi sana aisee. Nimepishana nae mjini kati
jamaa kama hanifahamu vile. Na kile ki Vitz
chake yaani kama hanioni vile!’
‘Labda hakukuona mkuu. Peter hayuko hivyo.’
‘Hapana alikuwa ananiangalia kabisa. Kaudhi sana jamaa. Tangu
awe na hicho kigari kabadilika mbaya. Kijiweni haji tena. Anajifanya yuko
busy.’
Msafiri haamini anachokisikia kwa Lazaro anayeonekana
kuufahamu upande wa pili wa Peter. Je, nani kati ya Lazaro na anamfahamu Peter?
Kwa nini Peter afahamike kwa sura zaidi ya moja?
Kubadilika
badilika kwa tabia
Kwa nyakati tofauti, katika shughuli zako za kila siku, nawe kama
Peter, unaweza kuwa na sura zaidi ya moja. Sura yako inabadilika badilika
kulingana na mazingira uliyopo.
Unapokuwa nyumbani, kwa mfano, unaweza kuwa na sura ya baba
mkali asiye na muda wa kumsikiliza yeyote. Watoto na mama yao, wanakuona kama mtu
mkorofi, asiyejali majukumu yake kama mume na baba.
Lakini unapokuwa kazini, unavaa sura ya kazi na kugeuka kuwa
mchapakazi hodari, mkali kidogo lakini anayefuatilia mambo kwa karibu.
Wafanyakazi wenzako, tofauti na familia yako, wanakuona kama mtu mwenye bidii
ya kazi, mwenye msimamo thabiti lakini mpenda watu.
Kanisani, pengine wanaokuona kama mtu asiye na bidii na mambo
ya dini, mzembe, lakini mwenye upendo kwa waumini wenye shida. Kila wakati panapokuwa
na uhitaji, unakuwa mwepesi kutoa msaada kwa fedha zako. Kwa namna hiyo,
umejijengea taswira ya mtu mwadilifu mwenye upendo ingawa hapatikani kirahisi.
Kubadilika kunakidhi
mahitaji yetu
Tabia zetu zinabadilika badilika kukidhi mahitaji ya
mazingira tunayokuwemo. Watu wanaotuzunguka wanakuwa na matarajio fulani kwetu.
Namna tunavyojiweka mbele zao, ni muhimu.
Chukulia umekutana na mtu unayejua atakayekusaidia kesho. Kwa
kuwa unajua atasaidia kesho, msukumo wa kuwa mnyenyekevu unakuwa mkubwa. Utaongea kwa lugha ya kistaarabu na uungwana
ukijaribu kujenga sura ya mtu anayestahili kusaidiwa. Lakini unapokuwa na mtu
unayejua hana hadhi wala msaada wowote kwako, ni rahisi kuonesha dharau.
Peter alifanya kitu kilichoonesha dharau kwa Lazaro, kwa
sababu pengine, Lazaro hakuwa na msaada kwa Peter. Inawezekana kwenye macho ya
Peter, hawa jamaa wawili Lazaro na Msafiri wana hadhi mbili tofauti. Pengine
Peter alimhitaji zaidi Msafiri na hivyo akawa mwema zaidi kwake kuliko
ilivyokuwa kwa Lazaro asiyemhitaji.
Tumeona kuwa tunachokifanya kwa watu kinategemea na mahitaji
na matarajio yetu kwao. Kwa sababu hiyo, ni vigumu sana kufikiri unamfahamu mtu
kwa sababu huwezi kujua kwa nini alifanya kile ulichokiona. Mtu anaweza
kukusaidia, mathalani, kwa sababu anajua kesho na keshokutwa utamsaidia. Ikiwa
atafahamu hutakuwa na msaada kwake, hawezi kukusaidia.
Tumewaona matajiri wanaotoa misaada mingi hadharani lakini
hawako tayari kusaidia watu wanaowafuata kwa faragha. Watu hawa wanapotoa
misaada, ni dhahiri lengo ni kujipatia heshima kwa jamii na sio kuwasaidia
wanaopokea misaada hiyo.
Unawezaje
kumfahamu mtu?
Hapa kuna mambo mawili ya kuzingatia. Kwanza, ni namna anavyowatendea watu anaojua fika kwamba hawana msaada wowote kwake. Kwa mfano,
mwalimu anapozungumza kwa heshima na Mkuu wa Shule au Ofisa Elimu, hatuwezi
kusema hiyo ndiyo tabia yake. Wema, unyenyekevu kwa mtu anayekuzidi si kipimo cha utu wako. Utu wa mwalimu huyu unaonekana pale anapokuwa na uwezo wa
kuzungumza kwa heshima na unyenyekevu kwa mwanafunzi wake. Katika mazingira yake hiyo inakuwa ndiyo tabia yake kwa sababu hana maslahi anayoyatafuta kwa mwanafunzi wake.
Lakini pia, namna gani mtu habadiliki badiliki kulingana na
mazingira, hiyo pia inaweza kuonesha kiwango chake cha kujitambua. Tabia tunazozionesha hadharani zinapokwenda sambamba na yale tunayoyafanya tukiwa faragharani maana yake ndivyo tulivyo.
Tabia
yako unapokuwa kazini, inapooana na tabia yako ukiwa nyumbani au kwingineko kokote, uwezekano ni
mkubwa kwamba hivyo ndivyo ulivyo. Lakini unapobadili tabia kulingana na matakwa ya
mazingira na watu wanaokuzunguka, uwezekano ni mkubwa kwamba tabia hiyo haianzii ndani yako. Ni namna fulani ya maigizo.
kazi nzuri sana ndugu Christian Bwaya. Post zako ni zaidi ya darasa. Najifunza mengi sana kupitia Jielewe blog . Ningependa kukukaribisha kutembelea blog yetu ya 90 Newz blog kwa elimu,buruani na habari za kila siku , pia kama utahitaji kupata muonekano mzuri na wa kisasa wa blog yako, wasiliana nasi kwa namba zilizopo ndani ya blog yetu. Ahsante
JibuFuta