Unamsaidiaje Mtoto Asiyefanya Vyema Kimasomo?
Kwa mzazi mwenye mtoto
anayesoma shule, ni rahisi kuelewa inakuwaje pale unapokuwa na uhakika mwanao
ana uwezo mzuri lakini matokeo anayoyapata shuleni hayalingani na uwezo wake.
Kama mzazi unayejali unajaribu kufanya wajibu wako, unamsaidia kazi za shule, unamwekea
mazingira mazuri yanayomhamasisha kujisomea akiwa nyumbani, unashirikiana na
walimu wake, lakini bado matokeo yanakuwa kinyume.
Hii ndiyo hali aliyopitia
rafiki yangu na mke wake. Mtoto wao wa miaka 9 anayesoma darasa la nne alikuwa
anafanya vizuri darasani. Alipofika darasa la tatu, maendeleo yake yalianza
kusuasua. Kwa mujibu wa wazazi, maendeleo yake darasani yaliendelea kuwa mabaya
siku hadi siku.
Kazi za shule ambazo
mtoto alipaswa kuzifanya akiwa nyumbani wakati mwingine hazikukamilika.
Kulikuwa na namna fulani ya uzembe. Kuona hivyo, wazazi waliamua kufuatilia
shuleni kupata ushauri. Walimu hawakuonesha wasiwasi na uwezo wa mtoto ingawa
wazazi bado waliamini mtoto alikuwa na uwezo wa kufanya vizuri zaidi.
Mama, ambaye ni mwalimu
wa sekondari, aliamua kuchukua hatua ya kuhakikisha anakuwa karibu na mtoto
kumsaidia kufanya kazi za shule. Pia, wazazi kwa pamoja walijitahidi kuweka
mazingira rafiki nyumbani kwa lengo la kumwezesha mtoto kupata muda wa kufanya
kazi za shule bila usumbufu. Utaratibu mzuri wa kutazama televisheni uliwekwa
kuongeza uzingativu wa mtoto kwenye masomo. Vifaa vya kieletroniki kama tablet
viliwekwa mbali na mtoto.
Pamoja na kuchukua hatua
hizo, bado hapakuwa na badiliko la dhahiri. Ilibidi wazazi wawe wakali kidogo
na kutumia adhibu ilipobidi. Kwa mujibu wa mama, adhabu zilikuwa na lengo la
kumfanya mtoto akamilishe kazi alizopewa shuleni. Kila mtoto alipofanya vibaya,
mama kwa ushirikiano na baba walitoa adhabu.
Hata hivyo, matokeo yake
bado yaliendelea kuwa kinyume. Adhabu na ukali vilianza kujenga hali ya woga na
wasiwasi kwa mtoto, kiasi kwamba kila alipowaona wazazi nyakati za jioni, alijawa
hofu. Kilichowastua zaidi wazazi ni kujengeka kwa tabia ya uongo kwa lengo la
kuficha kazi alizokuwa amepewa shuleni.
Punguza shinikizo la mafanikio
Kisa hiki kilinikumbusha
hali niliyowahi kukutana nayo nyumbani. Mwanangu hakuwa na tabia ya kukamilisha
kazi anazopewa bila kukumbushwa. Tabia hii, kama mtoto wa rafiki yangu,
ilichangia kuzorotesha maendeleo yake darasani. Kwa kuamini kwamba alikuwa na
uwezo mkubwa asioutumia, mimi na mke wangu tulianza kumwadhibu.
Kwanza, tulimzuia kwenda
kucheza na wenzake baada ya masomo. Pia, hatukumruhusu kutazama vipindi vya televisheni.
Ingawa alianza kufanya kazi za shule bila kusukumwa, ile furaha yake kama mtoto
ilipotea. Wakati mwingine alifanya kazi huku machozi yakimtiririka. Kosa moja
lilimaanisha kukemewa na kusimangwa.
Nakumbuka siku moja
asubuhi wakati anaondoka kwenda shuleni kufanya mtihani wa majaribio ya mwezi,
alidai anaumwa. Kwa kumtazama, nilihisi amejawa hofu ya matokeo mabaya.
Niliamua kumwondolea wasiwasi. Nilimwambia asiwe na hofu kwa sababu nilikuwa na
imani naye na sikuwa na hofu kwamba angefanya vizuri. Lakini pia, nilimweleza
kwamba hata kama asingefaulu vizuri, bado nilikuwa na imani yake.
Mtoto aliposikia hivyo,
alibadilika haraka. Uso wake ulichangamka na akaondoka kwa furaha. Siku chache
baadae alipokuja na karatasi za mitihani, matokeo hayakuwa mazuri kama
nilivyotarajia. Dalili kwamba hakuwa amefanya vizuri ni kuficha baadhi ya
karatasi.
Nguvu ya kumwamini
Niliamua kusimamia kile
ambacho nilikuwa nimemweleza kabla. Ingawa haikuwa rahisi kumpongeza,
nilijikaza na kumpongeza kwa kufanya vizuri. Hakuonekana kuamini. Nilimwambia
nina imani na uwezo wake. Niliweka msisitizo kwenye karatasi alizokuwa amefanya
vizuri. Nikamweleza kwamba nina imani kwamba anaweza, hata kama kuna baadhi ya
maswali hakuyapata.
Maneno hayo yalimwingia.
Niliuona uchangufu wake. Uso wake ulichanua. Hatia ilipotea. Kwa kuamini hakuwa
kwenye ‘kibano’ cha hukumu ya wazazi alinionesha karatasi nyingine alizokuwa
amezificha. Tulianza kuaminiana. Tuliweka mikakati ya kupata alama kubwa zaidi
kwenye masomo kwa namna ambayo ilionesha nina imani naye.
Kutambua jitihada
Baada ya siku hiyo,
nilianza kuona mabadiliko. Mtoto alianza kujituma kwa furaha. Alionekana kujua
anachokifanya. Kila niliporudi nyumbani ilianza kuwa mwepesi kunijulisha kile
alichojifunza shuleni. Kwake, ilikuwa ni fahari baba yake kusikia anavyoendelea
kujifikia malengo tuliyojiwekea pamoja. Nilimpa ushirikiano na kutambua juhudi
zake. Kama wazazi tulifanya maamuzi ya kumpongeza kwa kila hatua anayoichukua
na kumwonesha kwamba tuna imani na yeye.
Tangu wakati huo
hatujalazimika kutumia adhabu, kumkemea wala kumshinikiza kufanya kazi za
shule. Lakini amekuwa na hamasa ya kujituma yeye mwenyewe ili kututhibitishia
kwamba imani tuliyonayo kwake haikuwa bure. Maendeleo yake shuleni yamekuwa
bora zaidi.
Punguza matarajio
Pengine na wewe ni mzazi
kama mimi na rafiki zangu niliosimulia kisa chao awali. Unajitahidi kuhakikisha
mtoto anafanya vizuri shuleni lakini hujaona matokeo unayoyatarajia. Umemchapa
mtoto, umemkemea, umefuatilia shuleni, lakini bado mambo hayajabadilika. Usikate
tamaa. Kuna uwezekano mkubwa kwamba matarajio uliyonayo kwa mwanao ni makubwa
kuliko hali halisi. Pamoja na uzuri wake, matarajio makubwa yanaweza kuwa na
matokeo mabaya.
Fikiria mtoto amekuja
nyumbani na alama 73/100 wakati wewe kama mzazi unatarajia alama 95/100.
Utajisikiaje? Ni wazi utachukulia kwamba mtoto ‘anaendekeza uzembe.’ Katika
mazingira kama haya, tunaweza kusema, unayo matarajio makubwa yatakayokufanya
ama usimpongeze au umkemee kwa kufanya uzembe. Lakini je, ni lazima mtoto apate
alama 95/100?
Nimejifunza kwamba
matarajio makubwa kuliko kiasi inaweza kuwa adhabu mbaya kwa mtoto. Mtoto
anapojisikia hajaweza kufikia matarajio hayo, anaanza kukata tamaa. Moyo wake
unanyong’onyea kwa kujiona hawezi. Inapofikia hapo, mtoto anaweza kujenga
mtazamo hasi na shule. Mtazamo hasi unapochukua nafasi, mtoto anapoteza hamu ya
kujifunza.
Mwoneshe anaweza
Mtoto anayejiona hawezi ni
rahisi kudanganya. Ni kama mwanangu ‘aliyeugua’ siku ya mtihani. Kuugua
kulikuja kama namna ya kujihami na matokeo yanayoweza kuthibitisha kwamba ni
kweli hawezi. Uongo ulichukua nafasi kama namna ya kulinda uhusiano wake na
wazazi. Kule kuamini kazi za nyumbani zingemwingiza kwenye matatizo ya
kuadhibiwa, aliona ni afadhali ‘kuzipoteza’ ili awe salama.
Nimejifunza, kama mzazi,
ukiweza kuwa na ujasiri wa kumwamini mtoto bila kujali hali yake, ukiweza
kumthibitishia kwamba huna shaka na uwezo alionao, hiyo inatosha kuibua uwezo
wa ajabu ndani yake. Mtoto anayejua kuwa wazazi wake wanaona kitu ndani yake, wanajisikia
fahari naye, anakuwa na hamasa kubwa ya kuthibitisha kwamba hawajakosea
kumwamini. Tujifunze kutambua uwezo usioonekana ndani ya wanetu ili kuuchochea
udhihirike kwa mafanikio tunayoyataka.
Maoni
Chapisha Maoni