Nafasi ya Mzazi Katika Kukuza Vipaji vya Watoto



Jioni moja, mwanzoni mwa miaka ya tisini, nikiwa darasa la tatu, mama alikuja nyumbani na barua aliyoniambia ilikuwa yangu. Barua hiyo fupi iliyoanza na maneno, ‘Mpendwa mwanangu Christian,’ ilikuwa ndani ya bahasha yenye barua ya mama kutoka kwa baba yangu, ambaye kwa wakati huo alikuwa masomoni.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kupata barua niliyoiita yangu. Kabla ya hapo, nilizoea kukaa pembeni mwa mama kumsikia akinisomea sehemu ya barua yake iliyokuwa na salamu zangu kutoka kwa baba. Jioni hiyo, bila kutegemea, nikajikuta napanda ngazi na ‘kumiliki’ barua. Sitasahau nilivyojisikia vizuri. Niliisoma mara kadhaa bila kuchoka.

Kesho yake ilibidi nimshawishi mama tujibu barua ya baba. Kipindi hicho hapakuwa na namna yoyote ya mawasiliano isipokuwa kwa njia ya barua. Mama alikubali ombi langu la kumwandikia baba barua. Ulikuwa ni uzoefu mwingine wa pekee. Nilimtaarifu mambo mengi ya shule na nyumbani ambayo siwezi kuyakumbuka hivi leo. Huo ukawa ni mwanzo wa tabia yangu ya kupenda kuandika.

Mazingira ya uandishi

Aliporudi baada ya masomo, baba alikuwa na tabia ya kukaa mezani akiandika. Meza yake ilijaa madaftari yaliyokuwa na maandishi mengi. Wakati mwingine alitusimulia yale aliyoyaandika kwa lugha tunayoweza kuiielewa. Alikuwa akishiriki shindano la uandishi wa muswada wa kitabu lililoandaliwa na Kituo cha Maandiko Habari Maalum.

Siwezi kukumbuka kitu gani hasa kilifanya nami, katika umri ule, nipate wazo la kutunga na kuandika hadithi yangu kwenye daftari dogo. Nafikiri, kama mtoto, niliiga kile nilichozoea kukiona baba akikifanya nyumbani.
  
Nakumbuka siku moja nikiwa nimejilaza sebuleni baada ya chakula cha jioni, nilimsikia baba akiwasomea rafiki zake ile hadithi yangu. Nilijifanya nimelala na sisikii lakini nikisikia kila kitu. Siwezi kusimulia nilivyojisikia fahari kuona watu wazima wakisifia kazi yangu. Nilijifanya kukoroma lakini moyoni nilijaa kicheko cha ufahari. Nilijisikia fahari kuona baba yangu  anatambua kile nilichokuwa nakifanya kama mwanae.

Bila kujua ilikuwaje, nilianza kujitambulisha na kile ambacho baba alikifanya karibu kila siku. Baba yangu ni mpenzi wa maandishi hata leo. Nyumbani kwetu alijaza nakala za magazeti, majarida na vitabu. Pia, alikuwa na tabia ya kutunza kumbukumbu za matukio kwenye maandishi. Kwa kuwa nilijipambanua na yale aliyoyafanya, nilianza kuvutiwa na yale niliyoamini anayapenda. Naamini nilifanya nilichokiona anakifanya kwa sababu ndicho nilichofikiri kinamfanya ajisikie fahari na mimi.

Kipaji kilichojificha?

Nikiwa sekondari, maandishi yalikuwa sehemu ya muda wangu mwingi. Sikuchukulia kusoma vitabu kama adhabu. Nilisoma kama sehemu ya burudani. Nakumbuka siku moja, mwalimu wa somo la Kiswahili aliyeitwa Kitumbuizi alinishauri nikakuze kipaji changu kwa kusomea lugha. Sikufikiri nilikuwa na kipaji alichokiona yeye. Marafiki na wanafunzi wenzangu nao walifikiri ningefanya vizuri kama mwandishi. Sikukubaliana nao.

Ingawa hatimaye nilikwenda kidato cha tano kusoma Fizikia, Kemia na Baolojia, nilianzisha gazeti la shule tulilolibandika kwenye ubao wa matangazo. Mule tuliripoti matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea mabwenini na madarasani. Ilikuwa kama sehemu ya burudani ya wanafunzi. Waandishi wenzangu, hivi sasa wengine ni madaktari.

Sina hakika kama nilizaliwa nikiwa na mapenzi na maandishi. Nafikiri kukulia kwenye mazingira yenye harufu ya maandishi kuliumba uwezo fulani ndani yangu.

Nyumbani tulikuwa na desturi ya kusikiliza hadithi za biblia kila siku jioni. Baba alitenga muda mfupi kila siku kutusimulia matukio mbalimbali kama yanavyoelezwa kwenye biblia. Wakati mwingine alitusomea hadithi mbalimbali kwenye vitabu. Kuna uwezekano mkubwa kwamba mazingira ya namna hii yalichochea kipaji ambacho, hata hivyo, sikufikiri ningekuwa nacho.

Kuchochea vipaji

Siwezi kukumbuka nilianzaje kuchora. Sikujifunza kuchora. Uchoraji ulianza bila mimi kuelewa. Nikiwa darasa la V, nilikuwa na uwezo wa kuchora sura inayomtambulisha mtu anayefahamika. Niliwachora rafiki zangu, wazazi wangu, walimu wangu, wadogo zangu pamoja na mimi mwenyewe.

Sijawahi kumwona ndugu yangu mwingine akichora. Lakini nafahamu wazazi wangu walichochea kipaji hicho. Baba alikuwa mwalimu wa Jiografia. Mara nyingi nilimwona akichora ramani. Pale shuleni tulikokuwa tukiishi, alitengeneza ramani ya dunia ardhini kwa kutumia saruji na mawe. Sehemu zenye bahari ziliwekwa maji, milima ilionekana vizuri na maandishi yenye majina ya mabara na bahari yalionekana vizuri. Niliiga alichokifanya shuleni kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi wake. Nilitengeneza kitu kile kile nyumbani.

Wakati mwingine, nakumbuka alikuja na tufe yenye ramani ya dunia nyumbani. Nilipata wazo la kutengeneza kitu kama kile. Nilitumia kibuyu, nyaya, mbao na rangi kutengeneza ‘tufe ya bandia.’ Sikumbuki nilikuwa darasa la ngapi.

Hiyo ni mifano ya namna mazingira ya kimalezi yalivyochochea ubunifu na vipaji vilivyokuwa vimejificha ndani yangu. Mzee hakuwa mchoyo wa pongezi. Wakati mwingi nilichora na kufanya vitu kwa lengo la kumsisimua mtu niliyejua anajivunia kwa dhati nikifanyacho. Hiyo, ninaamini, ndiyo hasa ilikuwa hamasa yangu.

Ingawa yeye hakuwa mchoraji wa picha, aliniwekea mazingira ya kisaikolojia kunifanya nipende kuchora. Kwanza, alitambua uwezo niliouonesha kupitia ‘michezo’ yangu ya kila siku. Lakini pia, hakuchukulia ‘michezo’ hiyo kama upotevu wa muda ambao ningeutumia kujisomea. Kumtia mtoto moyo kufanya kile anachopenda kukifanya kwa hiyari, kunaibua na kukuza vipaji alivyonavyo.

Kipaji na mafanikio

Sikuweka mkazo kwenye uandishi na uchoraji kwa sababu niliaminishwa mafanikio yangu yanategemea ufaulu wa darasani. Nilifikiri kupata daraja la I na kusoma sayansi kungeniongezea nafasi ya kushindana vizuri kwenye soko la ajira. Pamoja na kuyapata hayo, bado niliendelea kujisikia kukosa kitu fulani nisichokifahamu.

Nikaanza kujifunza kuheshimu vipawa vilivyoanza kuchipua tangu nikiwa na umri mdogo. Nikaanza kuoanisha vipawa vyangu na elimu rasmi. Ingawa kila mtu amezaliwa na uwezo fulani wa pekee ndani yake, si kila mtu anaujua vipawa vyake. Kipawa ni ule uwezo wa kufanya kitu ambacho si watu wengi wanaweza kukifanya. Kuna watu, kwa mfano, wana vipawa vya biashara. Ukiwapa fedha kidogo, wanajua namna ya kuzizungusha. Wengine, wana vipaji vya ufundi. Hawajasoma sana, lakini wanaweza kutengeneza vitu ambavyo sisi wengine hata tungefundishwa hatutaweza.

Kipaji, kwa kiasi kikubwa, ndicho kinachoamua mafanikio ya mtu. Mtu asiyefahamu uwezo wa pekee unaoishi ndani yake, anaweza kuchukua muda mrefu kufurahia kile anachokifanya.


Bahati mbaya, mfumo wetu wa elimu hausaidii kujenga vipaji vya watu. Tunachukulia vipaji kama ‘shughuli’ za ziada zisizo na umuhimu. Kama wazazi, tunao wajibu mkubwa wa kuwasaidia watoto kuibua vipaji vyao na kuvitumia.

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia