‘Homework’ Zinavyodumaza Ukuaji wa Watoto Wadogo
PICHA: PhillyVoice |
Ukiwauliza wazazi kitu gani wanafikiri
kikisitizwa mapema zaidi kwa watoto kitawasaidia kufanikiwa, wengi watakwambia elimu. Kwa sababu hiyo, wazazi
hasa wasomi wanaharakisha kuwapeleka shule watoto wenye umri mdogo.
Ninawafahamu watoto wengi wa miaka minne wanaosoma
darasa la kwanza. Wazazi wa watoto hawa wanafanya hivyo wakiamini mtoto akisoma
mapema, maana yake uwezekano wa kufanikiwa maishani unakuwa mkubwa.
Shuleni pia, watoto hawa wanakutana na walimu wanaofanya
kila linalowezekana kuhakikisha ‘wanafaulishwa’ mitihani. Sababu ya walimu
kufanya hivyo, kama nilivyogusia kwenye makala yaliyopita, ni kujaribu kukidhi
matarajio yetu sisi wazazi.
Mbali na mtoto kufundishwa mambo mengi
yanayomzidi umri wake, kuna hili la walimu kuwapa watoto kazi nyingi
wanazotakiwa kuzikamilisha baada ya muda wa masomo. Kazi hizi, maarufu kama ‘homework,’
zinafahamika kama kazi za nyumbani.
Faida
Kazi hizi za nyumbani zina nafasi ya kutengeneza
daraja muhimu kati ya mazingira ya shule na nyumbani. Mwalimu anapompa mtoto
kazi hizi, kimsingi anatarajia kumfanya mzazi awajibike kutengeneza mazingira
ya kitaaluma nyumbani.
Mathalani, mzazi atalazimika kuacha kazi nyingine
na kumsaidia mtoto kukamilisha kazi. Kufanya hivi kunamlazimisha mzazi kujenga
ukaribu na mwanae na pia atafuatilia maendeleo yake kimasomo. Mawili haya
yanasaidia kutilia mkazo kile ambacho mwalimu anakuwa amekifundisha darasani.
Kadhalika, ‘homework’ zinamfudisha mtoto tabia ya kuwajibika.
Inaeleweka kwamba mtoto anaporudi nyumbani na kazi za shule, akili yake inakuwa
na kazi ya kuhakikisha wajibu aliopewa na mwalimu shuleni unakamilika.
Harris Cooper, wa Chuo Kikuu cha Duke amefanya
tafiti nyingi kuhusiana na utamaduni huu. Profesa Cooper anasema, “Kazi za
nyumbani ni utaratibu mzuri wa kujifunza. Kuna faida kadhaa, lakini faida hizo
zinategemea umri wa mtoto.”
Kwa watoto wa madarasa ya awali (yaani shule ya
awali na msingi), Harris Copper anafikiri inatosha shughuli ya mtoto kufanya
kazi za shule iishie darasani.
Mwalimu akitumia muda wake vizuri darasani, hana
sababu yoyote ya kumpa mtoto kazi za ziada kwa sababu hakuna uhusiano wa moja
kwa moja kati ya wingi wa kazi za nyumbani na mafanikio ya mtoto kimasomo.
Nikijitolea mfano mimi mwenyewe, pamoja na kuwa mtoto
wa mwalimu, sikumbuki ni lini niliwahi kukaa nyumbani nikifanya kazi za shule
nikiwa nasoma shule ya msingi. Kazi zote za shule ziliishia shuleni na
niliporudi nyumbani nilifanya mambo mengine yasiyo na uhusiano na shule.
Baada ya masomo, ratiba ya nyumbani ilikuwa ni
kumsaidia mama kufanya kazi za mikono kama kusafisha vyombo, kufua nguo zangu,
kuteka maji, kutumwa dukani na shughuli nyingine za kawaida.
Nilipokamilisha shughuli nilizopewa, nilikwenda
kucheza na kufanya shughuli nilizozipenda kama kucheza mpira, kuruka kamba,
kuchora na hata kusoma hadithi. Bado,
hata hivyo, nilitumia muda wangu wa shule vizuri na nilifanya vizuri shuleni.
Tafiti tofauti
Etta Kralovec, Profesa wa Elimu, Chuo Kikuu cha
Arizona anasema, “Tafiti ziko wazi kabisa kuwa masaa mawili ya kufanya kazi za
shule baada ya muda wa shule, yanatosha kwa mtoto mkubwa (wa sekondari.) Lakini
kwa mtoto mdogo (shule ya msingi), kazi za nyumbani hazina faida ya maana.”
Binafsi nimekuwa nikifuatilia kazi ambazo watoto
wengi wa madarasa ya chini wanapewa kuzikamilisha nyumbani. Nyingi, kwa kadri
ninavyoziona, hazina ulazima wowote zaidi ya kujaribu kumwaminisha mzazi kwamba
kuna kitu kinafanyika shuleni.
Kwa mfano, kazi nyingi ni za kukariri kwenye
vitabu, ambavyo mara nyingi havijapitiwa kwa makini na wataalam kujiridhisha ikiwa
vinafaa kwa watoto wadogo.
Pia, baadhi ya vitabu vina masimulizi yenye maudhui
yasiyolingana na umri wala utamaduni wetu lakini ndio vitabu ambavyo watoto
wetu wanatumia muda mwingi kuhangaika navyo kukamilisha kazi za nyumbani.
Changamoto
Mtoto anayeanza shule, anahitaji kusaidiwa kupenda
kujifunza na kuona shule ni mahali pazuri. Utamaduni huu wa kuwapa watoto kazi
nyingi, hata hivyo, unawafanya watoto hawa waanze kuchoka shule.
Fikiria mtoto wa miaka mitatu anayehitaji kucheza,
anajikuta kwenye mazingira ambayo kuna mtu anamlazimisha kujua kujumlisha na
kutoa.
Ingawa ni kweli mtoto anaweza kujifunza kwa lazima,
lakini kufanya hivyo kunaweza kumdumaza mtoto kwenye maeneo mengine muhimu ya
ukuaji. Mfano mdogo, watoto wengi hujikuta kwenye migororo mikubwa na wazazi
wao kwa sababu tu hawajafanya kazi za shule.
Badala ya kukaa na kuwafundisha watoto wao maadili,
tunu za maisha na kuwakuza kiroho na hata kujenga mawasiliano ya karibu, wazazi
wengi wanaishia kufokeana na watoto kwa sababu tu hawajakamilisha kazi za
nyumbani.
Mara nyingi watoto hawafanyi kazi hizi si kwa
sababu ni wavivu, wajeuri au si wasikivu. Hasha. Mara nyingi sababu ni ukweli
kwamba tumewaingiza kwenye mduara wa shinikizo la kitaaluma mapema zaidi kuliko
umri wao.
Kujenga utegemezi
Fikiria mtoto ameshindwa kufanya kazi alizotakiwa
kuzifanya kwa uzembe. Katika mazingira kama haya, mzazi anageuka kuwa afande
anayehakikisha kazi zote zimefanyika hata kama mtoto mwenyewe kimsingi haoni
maana ya kile anachotakiwa kukifanya.
Inapotokea
mtoto hana uwezo wa kuzifanya, badala ya mzazi kubeba wajibu wa kukazia
yale ambayo mtoto alijifunza shuleni, mzazi anaamua kuzifanya mwenyewe kwa
niaba ya mtoto, ili mwalimu shuleni asione mtoto hana mtu wa kumsaidia
anaporudi nyumbani.
Hapa tunatengeneza tatizo jingine la mtoto kujenga
utegemezi kwa watu wazima na kumnyang’anya mtoto tabia ya kuwajibika kwa mambo
yanayohusu.
Ingawa kumsaidia mtoto kukamilisha kazi zake
inaweza kuonekana kama mchango chanya wa mzazi kwa mtoto, tabia hii inaweza
kupanda mbegu ya kuwategemea watu wengine hata atakapokuwa mtu mzima.
Ushauri
Shughuli zisizo za kitaaluma moja kwa moja zina
nafasi kubwa ya kumfundisha mtoto vizuri zaidi kuliko kazi za nyumbani. Kwa
mfano, kuwasomea na kuwasimulia watoto hadithi ni namna bora zaidi ya
kuwafundisha watoto mambo wanayoyahitaji katika maisha yao ya kila siku.
Baada ya shughuli ya kujifunza shuleni, ni vyema nyumbani
pawe sehemu ya kumfanya mtoto ashiriki shughuli nyingine akiwa na familia yake.
Pia, tuweke mazingira ya mtoto kutumia akili yake
katika kuyachunguza mazingira yake kupitia michezo na kazi za mikono. Shughuli
hizi tunazoona hazina maana, zina nafasi kubwa ya kukuza uwezo wa mtoto
kukumbuka, kuzingatia, kufikiri kwa haraka, kukaa na wenzake na hata kuvumbua
vipaji vyake ambavyo wakati mwingine hatuvigundui kwa sababu muda wote tunataka
afanye hesabu, asome na aandike.
nimefurahishwa na mada hii nzuri bwana Bwaya ingawa Homework zangu za ukubwani zimefanya nichelewe kuweka hoja zangu, lakini naungana kabisa na hoja yako kuhusu Homework.
JibuFutaBinafsi nakumbuka sana wakati nakua kijijini huko ambako kwa kweli ufaulu ni mdogo, maswala haya ya Homework yalikuwa hayapo kabisa, Ingawa tulikuwa hatufurahii shule kwa sababu ya viboko, ila muda wa nyumbani ulikuwa hauna maswala ya Homework.
Nadhani basi inabidi wazazi waelimishwe namna bora ya kuspend muda na watoto wao, na pia shule hizi zielemishwe pia. Si siku nyingi iligundulika kuwa uwezo wa watoto kujua kusoma ,kuandika na kuhesabu ulipungua sana kiasi kwamba Baadhi ya watoto walikuwa wakimaliza elimu ya msingi bila kuwa na uwezo wa kusoma kitabu cha darasa la tatu kwa usahihi!
pengine ni kwa sababu homework nyingi ambazo pia hulazimika kufanywa na wazazi ili mwanae kesho asioneakana mjinga shuleni !
swala la kujiuliza, mwalimua anaandaliwa kweli ili kuwa na namna bora ya kumaliza kila kitu? je ikiwa darasa lina wanafunzi 50, na nyenzo hakuna? na je wazazi ambao pia hawaelewi na hawana muda? Je nafasi ya katuni na toy ambazo sasa zinatawala muda mwingi wa watoto?
ahhah