Mbinu za Kumshirikisha Mwanafunzi Katika Ujifunzaji
PICHA: United Nations |
Majuzi
niliwatembelea walimu wanafunzi waliokuwa wakiendelea na mazoezi ya
ufundishaji. Mafunzo kwa vitendo yana umuhimu wa kipekee katika maandalizi ya
walimu.
Katika kipindi
hiki, mwanafunzi anapewa fursa ya kutumia maarifa aliyojifunza darasani katika
mazingira halisi ya kazi. Kwa mwalimu, kama mimi, hiki ni kipindi cha
kutathmini uwezo wa mwanafunzi wa ualimu kumudu majukumu yake.
Moja wapo
ya vipindi vingi nilivyopata bahati ya kuhudhuria ni Baiolojia kidato cha III
kilichokuwa kikifundishwa na mwanafunzi wangu wa mwaka wa II.
Baada ya
kufanya utangulizi wa somo lake, mwalimu huyu mwanafunzi aliwaelekeza wanafunzi
wake kukaa katika makundi ya watu watano watano kusudi wafanye majadiliano.
Majadiliano
ni mbinu muhimu ya ufundishaji inayowawezesha wanafunzi kujifunza. Kama
tulivyosema kwenye makala yaliyopita, kupitia majadiliano, mwanafunzi hupata fursa
ya kusikiliza mtazamo tofauti kutoka kwa wenzake.
Aidha,
majadiliano ni mbinu shirikishi inayolenga kumfanya mwanafunzi awe mhusika wa
moja kwa moja katika ujifunzaji.
Pengine
kwa kutambua umuhimu wa ushirikishwaji huu wa wanafunzi, mwalimu yule aliwaonesha
wanafunzi wake mchoro wa jicho wenye herufi zinazoonesha sehemu mbalimbali za
ndani ya jicho.
‘Naomba
kwenye makundi yenu mjadili majina ya sehemu za jicho kwa kutumia herufi hizi zinazoonekana,’
aliwaelekeza wanafunzi wake na kuendelea, ‘mkishajadili mniambie kila herufi
inawakilisha nini.’
Ingawa mwalimu
aliwapa wanafunzi muda wa dakika 10 kukamilisha mjadala huo, kilichonishangaza
wanafunzi hawakuweza kujadili chochote.
Walionekana dhahiri wakisubiri muda uishie ili wapate majibu kutoka kwa
mwalimu.
Pengine
kwa kuhisi wanafunzi wake ‘wanamwangusha’ kwa kumfanya aonekane hajaweza
kuwashirikisha wanafunzi wake, mwalimu huyu alimua kupita kwenye makundi
akiwasaidia wanafunzi kupata majibu sahihi.
Ushirikishaji wenye manufaa
wanafunzi
Kimsingi
mwanafunzi wangu huyu aliyekuwa akijifunza kazi hakufanya tofauti na
yanayofanywa na walimu mashuleni.
Walimu
wengi, kama ilivyokuwa kwa mwanafunzi wangu, hupata shida kujua ni wakati upi
mwanafunzi ashirikiane na wenzake na anaposhirikiana na wenzake afanye nini.
Matokeo
yake mwalimu hujikuta akiwafunga wanafunzi ufahamu wasijue nini cha kufanya kwa
sababu hajaweza kuwawekea mazingira ya kujadili kitu kinachoeleweka.
Ili
ushirikishwaji uwe na manufaa, ni vyema mwalimu ampe ampe mwanafunzi mtaji wa
taarifa za msingi kuhusu jambo analokusudiwa kulijadili. Kazi ya mwanafunzi inakuwa
ni kuchambua na kutafuta majibu ya maswali yake kwa kutumia nyenzo alizonazo.
Mfano,
badala ya kuwaambia wanafunzi wajadili sehemu za jicho, kama alivyofanya
mwalimu wangu yule, ingefaa awape nyenzo zilizosheheni taarifa za macho kisha
awape swali linalowaongoza kutafuta majibu kwa minajili ya kuwawezesha kubungua
bongo zao kwa ushirikiano.
Aidha,
angeweza kuwauliza wanafunzi wake swali ambalo lingewasaidia kutumia uzoefu
walionao tayari bila kulazimika kutumia rejeo fulani ili kazi ya mwalimu iwe ni
kujenga kwenye kile ambacho tayari wanafunzi wanakifahamu.
Kwa
kufanya hivyo, wanafunzi wasingebaki wakishangaa wasijue nini cha kufanya kwa
sababu tayari wana kitu mahususi kinachowasaidia kuendesha mjadala wenye
mwelekeo unaoeleweka.
Tofauti za
wanafunzi
Wanafunzi wanatofautiana uwezo na vile wanavyoweza
kujifunza. Kwa mfano, wapo wanafunzi wanaojifunza kirahisi kwa kusikiliza na
kuona.
Hawa wanatumia zaidi masikio na macho yao
kufyonza taarifa wanazokutana nazo darasani. Uelewa wao unategemea namna gani
wanaweza kumsikiliza na kumwona mwalimu darasani kuliko kujisomea wenyewe.
Pia, wapo wanaojifunza vizuri zaidi kwa kuongea.
Hawa wanahitaji kusema, kwa maana ya kujadiliana na wenzao ili waweze kuchakata
maarifa. Bila kujadili wanakuwa na wakati mgumu kuelewa.
Lakini pia wapo wanaotegemea kutenda na
kushughulisha viungo vya miili yao ili waelewe. Bila kutenda, kushika, kutumia inakuwa
vigumu kwao kuelewa.
Uelewa wao, kwa kiasi kikubwa, unategemea namna
gani wanatumia mikono yao, miguu yao na hata kutembea tembea kama namna ya
kushiriki kile wanachojifunza.
Namna gani mwalimu anayefundisha darasani
anazingatia tofauti hizi? Je, mwalimu anawezaje kufikia mahitaji ya kipekee ya
kila mwanafunzi ndani ya kipindi cha dakika 40?
Badala ya kukazana kuelezea dhana kwa hotuba
pekee, mwalimu hawezi kuwafanya wanafunzi wakaongea, wakatumia michezo,
wakaona, wakagusa?
Kutumia nyenzo
tofauti
Tofauti hizi za ujifunzaji zinamlazimu mwalimu
kutumia nyenzo tofauti za maarifa. Kwa mfano, mwalimu anaweza kutumia vitabu
kama nyenzo yenye maelezo kina kwa kile anachokusudia kieleweke.
Wanafunzi wanaposoma vitabu wanapata nafasi ya
kuzama kwa undani kupata maelezo ambayo pengine mwalimu hatakuwa na muda wa
kuyagusia.
Hata hivyo, pamoja na uzuri wake, vitabu vinaweza
kuwasaidia baadhi ya wanafunzi hasa wale wasio na ugomvi na usomaji wa kina.
Kwa hiyo, pamoja na kutumia vitabu, mwalimu
anahitaji kufikiria nyenzo nyingine kuwafikia wanafunzi wengine. Kwa mfano,
penye uwezekano, mwanafunzi ashiriki kwa kubuni michezo inayoweza kuwasaidia
wanafunzi wanaojifunza kwa kutenda kuliko kusoma.
Pia, mwalimu anaweza kufikiri kutumia picha za
mnato na video kama namna ya kuwasisimua wanafunzi kujifunza. Faida ya kutumia
picha na video ni mwanafunzi kuona kwa uhakika kile kinachozungumzwa.
Kwa mfano, mwalimu anayefundisha ‘sehemu za moyo’
anapokuwa na nyenzo za picha halisi za moyo anamrahisishia mwanafunzi kazi ya
kujenga taswira ya kitu kinachozungumzwa.
Mwanafunzi anayeona kitu halisi, ni tofauti na mwenzake
anayeambiwa tu kitu asichojua kinafananaje. Nguvu atakazotumia kujaribu
kutengeneza picha ya kile anachofundishwa inaweza kuhujumu uelewa wake.
Binafsi nimekuwa nikitumia mbinu ya kuonesha
vipande vya filamu kwa wanafunzi wangu. Mbali na kuwasisimua kufuatilia kile
wanachohitaji kujifunza, nimeona namna nyenzo hizi zinavyowasaidia wanafunzi
kujifunza kwa wepesi zaidi.
Kukabiliana
na changamoto
Naelewa shule zetu zina changamoto kubwa ya
vifaa. Ninapoongelea kutumia filamu, naelewa shule zetu nyingi hazina umeme na
hivyo kuzungumzia teknolojia ni sawa na kuwadhihaki walimu wanaofundisha kwenye
mazingira haya.
Hata hivyo, mazingira haya magumu bado si kisingizio
cha mwalimu kuendelea kung’ang’ania mbinu za kimazoea katika ufundishaji.
Kwa mfano, badala ya kutumia muda mwingi kuandika
‘notes’ ubaoni, kwa nini mwalimu asitumie muda huo kuwafanya wanafunzi
wahusianishe somo lake na maisha yao ya kila siku? Je, mwalimu hawezi kufikiri
namna ya kuendesha mjadala mpana badala ya kuishia kuhutubu?
Mwalimu anahitaji ubunifu kutengeneza zana za
kufundishia kwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika mazingira yake.
Mfano, badala ya kuilalamikia serikali kwa
kutokumpelekea tufe, mwalimu anaweza kutumia kibuyu, rangi na mbao na akapata
mfano wa tufe.
Ndio kusema, pamoja na changamoto nyingi
zinazokabili shule zetu, bado upo uwezekano mkubwa kwa mwalimu aliyefuzu kubuni
nyenzo mbalimbali zitakazomsaidia kuwashirikisha wanafunzi wake.
Maoni
Chapisha Maoni