Hisia Zilizojeruhiwa Zinavyoweza Kujenga Ukatili Usiotarajiwa
PICHA: Pride News Magazine |
Baraka amekuwa akilalamikiwa kwa tabia yake ya udokozi tangu akiwa
darasa la tatu. Ingawa alikuwa mdogo kwa umbo, jina lake maarufu lilikuwa ‘Baraka
kibaka.’ Mbali ya kuwa kibaka, baraka alikuwa mgomvi aliyepambana na karibu
kila mwanafunzi shuleni.
Akiwa darasa la sita, Baraka alisimamishwa shule kwa kosa la kumshambulia
na kumwuumiza mwanafunzi wenzake. Baadae, Baraka aligundua kuwa aliyesababisha
afukuzwa ni mwalimu wa Hesabu aliyepeleka taarifa za tukio hilo kwenye uongozi
wa shule. Mara moja Baraka alimfuata mwalimu huyo ofisini na kumpiga makonde.
Lilikuwa ni tukio baya la mwanafunzi kumdhalilisha mwalimu ambaye si tu
anamfundisha, lakini pia ana umri wa mzazi wake.
Nilimfahamu Baraka kama jirani yangu. Maisha yake ya nyumbani
yalitawaliwa na ghasia tupu. Mbali na kuwa mgomvi kwa karibu kila mtu, Baraka
alikuwa na uwezo wa kujibizana na wazazi wake na hata ikibidi kukabiliana nao
pale walipotaka kumuadhibu. Ilikuwa kawaida kumsikia Baraka akipiga mayowe saa
za jioni. Wakati mwingine yalikuwa ni majibizano makali ya maneno kati yake na
kaka zake, baba au mama.
Nakumbuka si mara moja Baraka alijikuta akilala barazani akiwa amefungwa
mikono na miguu kwa kamba. Ilikuwa ni adhabu kali yenye udhalilishaji mkubwa
kwa mtoto mwenye umri mdogo kama Baraka. Ingawa wazazi wake walifikiri
wanatumia njia sahihi kumrekebisha, ni dhahiri walijeruhi moyo wake kuliko
kumsaidia. Kadri walivyomdhalilisha, ndivyo Baraka alivyozidi kuwa ‘gaidi.’
Majuzi nilisikia Baraka amekuwa kilema. Jicho lake moja limeng’olewa,
hana mkono moja, usoo umejawa makovu shauri ya vipigo vya ‘wananchi wenye
hasira kali.’ Baraka anadaiwa kuwa jambazi sugu, anayetishia usalama wa watu. Kwa miaka mingi, Baraka anadaiwa kushiriki
matukio mengi ya kihalifu ikiwa ni pamoja na ubakaji, unyang’anyi wa kutumia
mabavu na matumizi makubwa ya madawa ya kulevya.
Kwa haraka haraka tunaweza kumbebesha lawama zote Baraka. Tunaweza
kusema yeye ndiye aliyechagua maisha ya ukatili na kutokuwa na huruma na watu.
Lakini uwezekano ni mkubwa kuwa ukatili wa Baraka umetengenezwa na mazingira ya
malezi yasiyojali hisia zake.
Tafiti zinaonesha kuwa majambazi wengi na watu waliowahi kufanya matukio
ya kikatili, walizaliwa na wazazi wakali, wenye kutumia mabavu na wasiojali
hisia za watoto hao. Wengine wao huwa na historia ya utoto wenye maumivu
makubwa ya kihisia. Aidha, baadhi yao huwa hawajawahi kuelewa maana ya upendo
wa wazazi kwa sababu ya kuwa watoto wanaoitwa ‘wa mitaani’.
Ukweli ni kwamba hakuna binadamu anayependa kudhalilishwa. Kila mtu
tangu akiwa mdogo anatamani kuishi na watu wanaomwelewa na kujali hisia zake. Inapotokea
mtu anakuwa katika mazingira yanayomwuumiza kihisia na watu aliotegemea
wangemjali, hali hiyo hujenga kisasi ndani yao kama ilivyokuwa kwa Baraka.
Ukorofi wa mtoto mara nyingi ni ujumbe.
Ni muhimu wazazi kuuelewa ujumbe huu kabla hawajafanya maamuzi ya aina gani ya
adhabu waitoe. Ukorofi, mathalani, ni lugha ya mtoto kusema ndani yake
anajisikia utupu. Hisia zake hazijapata mtu wa kuzisikiliza. Anapofanya ukorofi
wake, kimsingi anatuambia kwamba sisi tunaomzunguka hatujatambua hisia zake.
Ndani yake mna sauti inayomwaminisha kuwa hatambuliki. Imani hiyo potofu
huchochea jitihada za kutafuta kutambulika kwa namna isiyokubalika.
Ugomvi, udokozi na ghasia nyingine
anazofanya –wakati mwingine bila hata yeye kung’amua anachokifanya– ni namna ya
kujirudishia mamlaka anayoamini hana. Anapobishana na mzazi, anapogombana na
wenzake, kama alivyofanya Baraka, kimsingi anajaribu kujiliwaza kuwa na yeye
bado anauwezo wa kupambana kama wengine.
Mtoto wa namna hii, kama ilivyokuwa Baraka, huishia kuwa na hisia
zilizokufa hali inayoweza kumfanya awe tayari kufanya chochote bila kujali
maumivu anayoyasababisha kwa wengine. Bahati mbaya, kadri anavyowaumiza
wengine, ndivyo anavyojisikia unafuu ndani yake kwamba na wengine nao wanaumia
kama anavyoumia yeye.
Matukio ya ukatili yanayoendelea kwenye
jamii yetu, yanaweza kuwa na mzizi kwenye aina ya malezi tunayowapa watoto
wetu. Matumizi ya mabavu kupita kiasi, adhabu kubwa zinazoumiza mno hisia za
watoto, zinaweza kuwa mbegu mbaya itakayozalisha watu wasiojali hisia za
wengine, watu watakaokuwa tayari kuumiza wengine na hata ikibidi, kuwatoa roho
ili tu kuridhisha nafsi zao kwamba nao wana uwezo wa kufanya matendo ya
‘kishujaa’ yatakayowanyoosha wengine.
Tunahitaji kutambua kwamba watoto, bila kujali makosa yao, wanaelewa vizuri
zaidi lugha ya upendo inayojali hisia zao kuliko adhabu kubwa tunazowapa. Tukijenga
mazoea ya kuumiza hisia za mtoto, tunatengeneza kizazi cha watu watakaofurahia
kuwaumiza watu wengine wakiamini kufanya hivyo ni ushujaa.
Maoni
Chapisha Maoni