Ufanyeje Kijana Chipukizi 'Anapokata' Mawasiliano na Wewe?

PICHA: Parent Pump Radio


Kama nilivyoeleza kwenye makala yaliyopita, tofauti za kimtazamo kati ya mzazi na kijana anayechipukia ni hali zinazotarajiwa. Wakati mwingine tofauti hizi zinaweza kuonekana kama mambo madogo yasiyo na msingi. Lakini tofauti hizi zinazoonekana kuwa ndogo zisiposhughulikiwa zinaweza kukomaa na hatimaye kusababisha matatizo makubwa.

Wazazi, mara nyingi, hatupendi kuzipa uzito tofauti hizi mara zinazopoanza kujitokeza. Kijana wako anaweza kuanza kuwa mkimya bila sababu za msingi, anaanza kukukwepa na hata kupunguza mawasiliano na wewe, lakini ukachukulia ‘kawaida.’

Kimya hiki, kwa hakika, kinasema mengi. Kwa kukaa kimya mwanao anakutumia ujumbe usiowazi kuwa hali si shwari. Kukunyamazia si tabia mbaya moja kwa moja bali namna ya kueleza manung’uniko yake kwako.

Najua katika mazingira kama haya, wazazi wengi huwa tunajitetea kwamba sisi tuko sahihi na mtoto ndiye mwenye tabia mbaya. Wakati mwingine inawezekana ni kweli tatizo ni la mtoto.

Hata hivyo, pamoja na kuwa sahihi kama wazazi, hiyo bado haikuondoi wewe mzazi kwenye wajibu wa kurudisha mawasiliano na mwanao.  Haitoshi kusema, “Huyu kijana amenishinda. Nimejitahidi kumfanyia kila nilichoweza lakini bado anaendelea kunisumbua.”

Inawezekana kweli umefanya mengi kwake na unapoona anapoteza mwelekeo unakata tamaa. Unajisikia kusumbuliwa. Hata hivyo, natamani kama mzazi uelewe kinachomtokea kijana mwenye umri wa miaka 12 mpaka 19. Huyu ni mtu anayepita kwenye kipindi cha mpito chenye mitikisiko mingi inayomsaidia kupanda ngazi ya kuwa mtu mzima.

Kwa umri huu, kama tulivyoona, kijana chipukizi anajichukulia mtu mzima ingawa ukweli wa mambo bado ni mtoto kiakili na kimwili. Mwili wake unapitia mabadiliko makubwa ambayo wakati mwingine yanamfanya atawaliwe na hisia. Mabadiliko haya ndio hasa yanafanya aumizwe na mambo madogo.

Kimsingi, huu ndio umri wa kumwelekeza kipi ni kitu sahihi cha kufanya pasipokujeruhi zaidi hisia zake. Wajibu wako kama mzazi unayeelewa haya ni kufanya jitihada za kumweka karibu na wewe kutafuta imani yake. Akiisha kukuamini huo ndio unakuwa mtaji unaokuwezesha kumwambia jambo unaloamini ni sahihi na atakusikiliza.

Ndio kusema, hata pale anapokuwa amefanya makosa ya wazi, kijana chipukizi bado anahitaji kuamini bado kuna mtu ana imani na yeye. Hata katika mazingira ambayo watu wengine wanamhukumu, kijana huyu anahitaji kuona bado yupo mtu asiyemhesabia makosa yake. Mtu huyo ni wewe mzazi auliyetayari kulinda uhusiano wenu kuliko kutafuta ushindi unaweza kubomoa uhusiano wenu.

Tuchukulie kijana wako mwenye umri wa miaka 16 ameanza kujitenga na wewe. Kila ukitaka kukaa naye, anakuponyoka. Wakati mwingine unashangaa inakuwaje hajisikii fahari kuzungumza na wewe. Unaweza kumkuta akizungumza kwa furaha na marafiki zake au watu wengine. Lakini akiwa na wewe ‘hana stori.’

Katika mazingira kama haya, wazazi wengi hufikiri kijana huyu anastahili adhabu kwa kosa la kuonesha kiburi kwa wazazi wake. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba, kisaikolojia, ukuta kama huu haubomolewi kwa kumfokea na kupambana naye.

Namna nzuri ya kumsaidia kijana anayeonekana kushindana na wewe kama mzazi, wakati mwingine, ni kuacha kupambana naye na badala yake kufanya kazi ya kubomoa ukuta wa mawasiliano uliojengeka kati yenu.


Badala ya kujadili nani ni mkosefu, ambaye ni dhahiri atakuwa yeye, jenga imani akuamini. Akikuamini, ni rahisi kumweleza kosa lake na akawa tayari kukuelewa.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia