Maswali Matano Yatakayokusaidia Kujua Thamani ya Kazi Yako
Nianze
kwa kukuuliza swali rahisi. Kitu gani kinakupa motisha ya kuamka asubuhi na kwenda
kazini? Unafikiri nini hasa kinaongeza thamani ya kazi yako?
Kwa
mujibu wa tafiti, takribani asilimia 80 ya watu wanaofanya kazi za kuajiriwa au
kujiajiri hawapati utoshelevu. Kwa hakika mambo mengi yanachangia watu
kutokupenda kazi zao. Kuna migororo kazini, kutokufikia matarajio waliyokuwa
nayo na wakati mwingine mazingira hafifu ya kazi.
Pia,
sababu nyingine ni kutokuona namna gani kazi anayofanya mtu inakidhi makusudi mapana
ya maisha yake. Katika mazingira haya, ni vigumu kuona thamani ya kazi yake na hivyo
itakuwa vigumu kutosheka.
Mtu
anayependa kazi yake mara nyingi anakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuwa
mbunifu, kuwa na bidii zaidi na hivyo kupata matokeo mazuri kuliko mtu
anayesukumwa kufanya kitu asichoona thamani yake.
Kwa
kuzingatia ukweli huo, katika makala haya tunaangazia maeneo matano yanayoweza
kukusaidia kuelewa kwanini kazi unayoifanya inaweza kuwa na thamani usiyoiona.
Unajua wewe ni nani?
Swali
hili linaonekana jepesi lakini si kila mtu anaweza kulijibu. Kwa wengi wetu,
tunapoulizwa sisi ni nani, mawazo yetu yanakwenda kwenye majina yetu.
Tunafikiri sisi ni majina yetu.
Lakini
ukweli ni kwamba tungeweza kubadili majina yetu na bado tukabaki kuwa sisi.
Maana yake sisi ni zaidi ya majina yetu.
Usipojua
kwa hakika wewe ni nani itakuwa vigumu kujua unachopaswa kukifanya. Utajaribu
kujifunza kila ujuzi, utafanya mambo mengi kwa wakati mmoja, matokeo yake
hutajipambanua kwa jambo mahsusi litakalokufikisha kwenye kilele cha mafanikio.
Hatua
ya kwanza ya kujitambua ni kujua vitu maalum ambavyo Mwenyezi Mungu ameviweka
ndani yako. Hapa tunazungumzia vipaji, ujuzi, maarifa na uzoefu ulionao. Vitu
hivi kimsingi ndivyo vinavyobeba utambulisho wako.
Unapojiulizwa
wewe ni nani, maana yake unaulizwa kuubaini uwezo wa kipekee unaoishi ndani
yako. Uwezo huu ndio uliobeba thamani yako.
Unafanya nini?
Ingawa
sote tunafanya kazi kwa bidii, si kila mmoja wetu anajua kwa hakika kitu gani
hasa mahsusi anachotakiwa kukifanya.
Tumezungukwa
na mashinikizo ya kila aina yanayojaribu kutushawishi kuchukua uelekeo fulani katika
maisha. Mashinikizo haya, mara nyingi yanatufinyanga kufuata mkumbo unaotulazimisha
kukidhi matarajio yasiyokidhi thamani zetu.
Kutokujua
kitu kinachobeba thamani ya kazi tunazozifanya, hutufanya tukate tamaa na yale
tunayoyafanya, hali inayochangia kutukosesha furaha ya kazi.
Hata
hivyo, ukizungumza na watu wanaojivunia kazi zao unagundua hawa ni watu
wanaojua kwa hakika kitu gani hasa wanachokifanya. Hawapati shida kujua eneo
lipi la maisha wanaliweza zaidi kuliko maeneo mengine. Wanajua kitu gani
wanachokifanya kinachobeba thamani zao.
Hebu
jiulize unazo sifa zipi maalum unazodhani zinakuweka kwenye nafasi nzuri zaidi
ya watu wengine kujifunza kwako? Je, kazi unayofanya inatumia uwezo na sifa
hizo unazoamini unazo?
Unalinufaisha kundi lipi katika jamii?
Kwa
asili binadamu ni mbinafsi anayejifikiria yeye na mahitaji yake. Ndio maana tunapofikiri
kazi gani tufanye, mara nyingi tunafikiria namna gani kazi hiyo itakavyotusaidia
kuwazidi wengine.
Hakuna
ubaya kimsingi kuwa mbinafsi kwa sehemu. Hata hivyo, watu wanaofurahia kazi zao
wanafanya tofauti. Watu hawa, wanakwenda mbele ya mahitaji yao binafsi. Badala
ya kujifikiria wenyewe, wanakuwa na aina fulani ya kundi la watu wanaolenga
kulifikia kupitia kazi zao.
Kwa
lugha nyingine, watu hawa wanajua kwa hakika nani ananufaika na kile
wanachokifanya na hivyo wanatumia ujuzi na uzoefu walionao katika kuhakikisha
watu hawa wananufaika.
Nikuulize,
unalijua kundi mahsusi la watu wanaonufaika na kazi yako? Akina nani ni
walengwa wa kazi yako? Ukiwatambua vizuri watu unaowatumikia, uwezekano ni
kubwa utaanza kuona thamani ya kazi yako.
Unatatua tatizo gani?
Furaha
ya kazi yako inategemea pia namna gani unaamini kazi hiyo inakufanya kuwa jibu la
matatizo yanayowakabili watu wengine. Usipokuwa na uhakika kazi yako
inakuwezesha kutatua tatizo gani kwa watu, kwa hakika, itakuwa vigumu kuifurahia.
Unaweza
kuwa na madaraka, kipato, heshima na umaarufu, lakini kama huna hakika kazi
yako inakusaidia kutatua shida gani za watu wanaokuzunguka, unaweza kuendelea
kujisikia utupu ndani yako.
Je,
kazi yako inakuwezesha kutatua tatizo gani? Je, watu unaowalenga wanakabiliwa
na changamoto gani ambazo kwa uwezo, vipaji, ujuzi ulionao unaamini unaweza
kuwasaidia kuzitatua?
Ukweli
ni kwamba kila kazi inaweza kukupa utoshelevu. Muhimu ni kujua aina ya matatizo
unayoyatatua kwa kupitia kazi yako. Utoshelevu wa polisi, kwa mfano, unategemea
namna gani anajua vile anavyowezesha watu kuishi bila hofu ya uhalifu. Polisi
huyu, akiweza kuelewa tatizo analolitatua katika jamii, bila shaka anaweza
kuipenda zaidi kazi yake kuliko anapojifikiria kama ‘mie polisi tu.’
Unaleta tofauti gani kwa watu?
Tunaweza
kupima mafanikio yetu kwa kipato, mamlaka tulivyonayo, umaarufu lakini kama
vyote hivyo haviwasaidii watu wengine kuwa bora zaidi, itakuwa vigumu kujisikia
utoshelevu.
Njia
rahisi ya kujua nafasi uliyonayo katika jamii ni mchango unaoutoa kuboresha
maisha ya watu unaowalenga. Unapoona maisha ya watu yanabadilika kama matokeo
ya kile unachokifanya kupitia kazi yako, ni wazi utapata utoshelevu zaidi.
Ukitaka
kujua tofauti unayoileta kupitia kazi yako, jifunze kwenda mbele ya jina la
kazi yako. Fikiria matokeo ya kazi unayoifanya katika jamii.
Kwa
mfano, kama wewe ni mwalimu wa shule ya msingi, kazi yako ni kuwasaidia watoto kujitambua
na kufikia ndoto zao. Kazi yako ni zaidi ya ualimu. Ukianza kuitazama kazi yako
kwa mtazamo huo, unaweza kushangaa namna utakavyokuwa na utoshelevu kuliko mtu
anayesema, ‘Mimi ni mwalimu tu.’
Kama
wewe ni muuguzi, badala kujibana kwenye jina la kazi yako, jione kama mtu anayefanya
kazi ya kuwasaidia wagonjwa kuwa na furaha zaidi wanapopata huduma za daktari.
Kwa
kifupi, tukiweza kuzitathimini kazi zetu kwa kuangalia nani tunayejaribu
kumsaidia, tutajiongezea uwezekano wa kuwa watu wenye furaha zaidi.
Maoni
Chapisha Maoni