Jinsi ya kumlinda mtoto na tofauti zenu



Simulizi la Renee limenikutanisha na wadau wa ushunuzi mjini Moshi. Tunapata kahawa jioni baada ya shughuli za siku. Hatujaonana muda. Tunasalimiana na kisha mada inageuka ghafla. Rebert anarejea mfano wa Renee, “Suala la mgogoro wa wazazi kumuathiri mtoto hilo halina mjadala.” Robert ‘anavuta’ kahawa kidogo kama mtu anayesikilizia ladha ya kinywaji cha moto sana na kisha anaendelea.

 

“Ukimsoma huyu dada ni dhahiri migogoro ya kifamilia ilikuwa na nguvu ya kuchora mwelekeo wa maisha yake ya kimahusiano.” Robert anasita. Wajumbe wamepotelea kwenye vioo vya simu zao. Kajihisi anaongea mwenyewe. Natingisha kichwa kumwitikia.

 

“Inasikitisha sana namna maamuzi yetu kama wazazi yanavyoweza kumnyanyasa mtoto kwa kiasi kile. Sitamani niwe mzazi nitakayemfanya mtoto awe na kazi kubwa ya kurekebisha tabia alizojifunza kwangu,” anajitahidi kujieleza Robert lakini kakatishwa tamaa. Wanaume hawamsikilizi wanacheka na simu zao. Hata mimi pia ninahisi huenda ninamsikiliza mwenyewe.

 

Kishunuzi, analolisema Robert lina ushahidi wa kutosha. Matatizo mengi ya kitabia tunayopambana nayo ukubwani tulijifunza kwenye familia zetu. Hatukuwa na ufahamu wa kutosha kuchambua mema na mabaya lakini fahamu zetu zilinyonya kila tulichokishuhudia kwa wazazi wetu.

 

“Hili linanifanya nijisikie hatia sana kama mzazi,” anatikisa kichwa Denis kwa masikitiko huku akibinya simu ilale kwa muda. Denis anafafanua, “Unajua kweli kuna kutofautiana kwenye maisha ya ndoa. Lakini watoto kuwa wahanga wa mambo yasiyowahusu inanifanya nijisikie vibaya.”

 

Mhudumu anakuja. Denis anajikausha kwa muda. Faragha ya meza inarejea na Denis anatoboa siri, “Mie siku moja mwanangu wa miaka sita alikuja akaniambia kitu ambacho mpaka leo kinanifanya nijisikie aibu sana: Mtoto aliniuliza: baba kwa nini unagombeza mama? Swali lilinichoma sana” Denis kafunguka. Si kawaida kwa wanaume kufunguka kiasi hiki. Hulka hii ya kuficha aibu huzuia mazungumzo na wanaume kufikia kwenye kiini cha tatizo.

 

Hisia tulizonazo ukubwani nyingi ni mchanganyiko wa kumbukumbu  ya yale tuliyoyashuhudia utotoni na tafsiri iliyotokana na tuliyopitia. Hisia kama sonona, hasira, aibu, hatia na hisia nyingine hasi ni matokeo ya kumbukumbu za uonevu, maumivu na kutokutendewa haki utotoni.

 

Nade, mwalimu, anatoa ufafanuzi kidogo, “Watoto bwana wanakuwa-ga makini sana na maisha yetu wazazi kuliko tunavyodhani. Inamtisha sana mtoto kwa mfano kuona mama yake analia. Mama anaweza kuchukua kawaida lakini kwa mtoto hiyo ikampa wasiwasi labda shida ni yeye (mtoto).” Unaweza kuona kwa nini mgogoro baina ya wazazi unaweza kuwa na madhara makubwa kwa mtoto.

 

“Unachokisema ni kweli,” Eze anaunga mkono maelezo hayo, na haraka anatuonesha upande wa pili. “Nimeona Renee anakuwa kama anajutia maisha aliyoishi mwenyewe kwa hiyo kaamua kumkaribisha mwanaume waliyeshindwana asiwe mbali na mtoto. Uamuzi mzuri lakini sijui kama anaona uwezekano wa baba kupanda vitu visivyo sawa kwa mtoto? Vipi kama kilichowafarakanisha ni tabia za baba?”

 

Swali gumu. Tunalijadili. Baada ya mjadala mrefu, Majid mwanasheria kitaaluma, anayepambana na ufaulu wa Shule Kuu ya Sheria (LST) anahoji ikiwa ubaya wa baba ni sababu inayotosha kumnyima haki ya kuwa baba kwa mwanae. Sikiliza Majid anavyong’aka: “Wangapi wetu hapa tumelelewa na wazee waliokuwa pasua kichwa? Kwa nini watu wakipishana mmoja ndio akose haki ya kumlea mwanae? Unajua hivi vitu ukiviangalia vizuri mara nyingi ni ego (ubinafsi). Unagombana na mtu unataka agombane mpaka na mwanao. Kweli?”

 

Denis aliyekuwa kashika tama muda mrefu anaitikia, “Sio sawa kabisa na kwa mambo yalivyo mara nyingi mwathirika anakuwa-ga mwanaume,” wote tunaangua kicheko cha mashaka. “Tukimeza ego zetu, tunaweza kumtenganisha mtoto na matatizo yetu. Lakini wasiwasi nao sio jambo la kupuuzia. Kuna watu ni shida. Mkishagombana anakuwa na kisasi mpaka anaweza hata kum-abuse (mnyanyasa) mtoto kingono. Kuchukua tahadhari ni muhimu lakini kumnyima mtoto haki ya kuwa na baba yake nayo ni aina fulani hivi ya ukatili.”

Nade anamkatisha, “Aah bwana unatumia maneno makali sana na wewe. Au na wewe ni mkatili nini?” wote tunanyanyuka tusisikie Denis anavyojitetea.


Niandikie: bwaya@learninginspire.co.tz 

 

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia