Usidanganyike. Wema huanzia nyumbani.
Umewahi kukutana na mtu mwema kiasi kwamba unawaonea ‘wivu’
familia yake? Unajiuliza, “kama huyu jamaa anaweza kuwa mkarimu hivi kwa sisi
wapita njia tusiomhusu kivile, nyumbani kwake si watakuwa wanamfaidi sana?” Sasa
usinielewe vibaya. Silengi kukukatisha tamaa. Ni vile tu nimeshangazwa hivi majuzi.
Godi ni rafiki yangu wa siku nyingi. Kwa hulka, ni mtu
mchangamfu mwenye wingi wa bashasha. Kaa na Godi mzungumze utapenda namna yake
ya kuzungumzia masuala. Godi anajua aseme nini wapi na kwa nani.
Halafu kuna wema. Godi hasubiri umtafute. Haipiti wiki
hajakupigia na wala hatakuuliza kwa nini humpigii. Hivyo. Ukiwa na shida, Godi
huyu hapa. Hana uwezo sana kifedha. Maisha yake ni haya haya kama ya wengi wetu.
Sema ni ule utajiri tu wa roho ya mtu. Usha’nfahamu? Godi. Ukiniuliza mtu mwema
nimewahi kukutana naye, nitakwambia Godi bila hata kupepesa macho.
Jamaa yetu mmoja aliwahi kumsifia kiutani lakini alikuwa sahihi.
Kwa jinsi alivyo mwema, jamaa alisema, Godi anaweza asiwe na hata mia ya kukupa
lakini akaenda kukukopea mahali kusudi akunusuru na dharura. Huyo ndio Godi. Mwema
kupindukia.
Saa nyingine unajiuliza, mtu anaanzaje kuwa mwema vile? Dini.
Wengine wanaziona dini kama vyama vya kujenga himaya kwa mwamvuli wa imani. Mie
niko tofauti. Dini ni ule ucha Mungu unaojenga wema usiowa maigizo.. Ndio Godi
huyo. Ukifungua kibegi chake hukosi machapisho ya dini. Hakosi ibadani. Halafu
sasa sio tu ni mtu wa makanisa kanisa, Godi anachapa kazi. Naambiwa kazini
kwake ukitaka shughuli iende na matokeo yaonekane mpe Godi. Nadhani umepata
picha kidogo.
Sasa juzi mke wake kanitafuta
analia. “Shemeji nini?”nikamwuuliza kwa wasiwasi. Kwikwi kwa mbali. “Ongea na
rafiki yako Godi. Naondoka,” shemeji ananichanganya. “Unaondoka? Unakwenda wapi
shemeji?” nauliza kama mtu nisiyejielewa. “Nimechoka shemeji. Bora nife.” Kha!
Imekuwaje tena shemeji anathubutu hata kufikiria mambo ya kujitoa roho wakati
hata matokeo ya sensa hayajatoka. Kuna nini?
Shemeji, mke wake na Godi,
anafunguka. Nabaki kinywa wazi. Sijui nimwambie nini zaidi ya kuitikia. Mama
kateseka sana yule. Nabaki kishangaa. Godi kawa lini mkatili vile nyumbani? “Nimechoka
maisha ya maigizo shemeji. Nimeishi maisha ya ujane muda mrefu. Bora niende
kwetu. Nimesema nimechoka.”
Godi huyu huyu? Naona aibu maana ni
kama nimedanganyika muda mrefu: “Hatuongei miaka na miaka. Hatuwezi kutulia
mahali tuzungumze kitu kinachoeleweka. Godi hakamatiki nyumbani. Hajali la mtu
sio mimi sio mtoto. Juzi mtoto kaugua usiku. Baba ni kama hayupo. “Usipaniki
homa itaka yenyewe?” Ndio kitu cha maana alichosema. Muda wote anacheka na watu
kwenye simu. Hana habari na mtu humu ndani.”
Lahaula. Naogopa ninayoyasikia.
“Shemeji, hatulali chumba kimoja muda mrefu.” Jamaa yangu amekuwaje tena?
“Kutwa kusafiri utafikiri anafuatilia kitu cha maana. Kumbe ni wanamke.” Godi
huyu huyu anayetembea na vitabu vya Tumwimbie
Bwana kwenye mkoba?
Nikajifunza mambo mawili makubwa.
Kwanza, tabasamu halisi la mwanaume linaanzia nyumbani. Usidanganywe na watu
wachangamfu kwenye makundi sogozi mitandaoni. Bashasha la mwanaume wa ukweli
linaanzia nyumbani. Uungwana wa halisi wa mtu sio huu tunaouona mitaani. Uungawana
halisi wa mtu ni vile anavyoishi na watu wa nyumbani kwake. Hao ndio watu
wanaomjua ndani nje. Hao ndio wanaweza kukwambia undani wa mtu.
Lakini kingine, nikagundua kumbe
watu tunaishi kitalaam sana mjini. Si unajua dhana ya mtaji jamii? Nani
atakuamini mjini usipovaa sura fulani? Unalazimika kuchekea mpaka wapitia njia,
unagawa tipu kwa wahudumu, unajua usipofanya hivyo, wasifu wako mjini utajitia
doa. Tunaishi kwenye dunia ya kibepari. Ukiharibu jina mjini utajikosesha
vingi. Sasa hapo ndo’ unakutana na hizi sura ‘bora’ za watu zinazoonekana maofisini,
makazini, ibadani. Lengo, mara nyingi, ni kuwezesha mipango yetu iende.
Nategemea kukutana na Godi nisikie anasemaje. Lakini wakati tunasubiri kumsikiliza Godi mwenyewe, nimegundua watu wengi
hutafuta sana kuaminiwa na watu baki. Wanachasahau, masikini, imani inaanzia
nyumbani. Unsha’nsoma? Ogopa sana mtu anayeweza kuumiza watu wa nyumbani kwake
na wala haonekani kujali. Rudia sentensi hiyo.
Niandikie: bwaya@learninginspire.co.tz
Asante kwa darasa zuri
JibuFutaHii ni kweli kabisa, na inaumiza sana, kuna haja ya kujihoji na kubadilika
JibuFuta