Mwanaume anapokimbia 'kelele' nyumbani

 


Mwanadamu ana uwezo mkubwa wa kuficha tabia. Samahani. Namaaminisha mwanaume. Unajua, katika jamii zetu, ni aibu mwanaume kukiri mahusiano yamekushinda. Kuliko kuitwa kila aina ya majina saa nyingine tunalazimika kujenga taswira ya ukamilifu hata kama kiuhalisia tunaugulia maumivu makali. Jumlisha hapo dini, kwa maana ya hizi itikadi za ufuasi wa halaiki, kiwango cha kuonesha ukamilifu lazima kiwe juu zaidi.

 

Tumeaminishwa ndoa ni kielelezo cha ukamilifu. Hakuna kukosea. Ukishasema una changamoto na mwenzako, watu wanakupiga jicho la dhihaka, “Hukumwomba Mungu akupe mke? Humtegemei Mungu vya kutosha?” Nani yuko tayari kuonekana hana uhusiano mzuri na Mungu?  Kwa upande mmoja, ninamuelewa sana Godi. Hofu ya kuchafua jina lake inamfanya aigize amani ya ndoa isiyokuwepo.

 

Swali nililojiuliza, kwa nini sasa Godi amefikia mahali hajali watu wa nyumbani kwake? Kama ana tatizo na mkewe, inakuwaje anashindwa kujali hata watoto? 

 

Kila tabia, kwa kawaida, haikosi historia.  “Godi alibadilika baada ya mimi kumzaa Glady mtoto wa kwanza,” mke wake anakumbuka. Uso unajaa haya. “Niliongezeka sana uzito baada ya uzazi na baba Glady [Godi] akawa anasema nimejiachia.” Ninakuna kichwa nikijiuliza maswali. Godi huyu huyu mwenye kitambi analalamikia kitambi cha mkewe?  Shemeji anaenda mbali, “Tulianza kugombana mara kwa mara maana alikuwa hakamatiki na mimi nilihitaji awepo nyumbani.” Ilivyoonekana kuna mengi niliyohitaji kuyafahamu zaidi. Nikamwomba shemeji anipe muda nizungumze na Godi kwanza.

 

Basi. Mazungumzo na Godi hayakuwa rahisi. Mada yenyewe ngumu. Tunaanzia wapi kama Godi mwenyewe anajihami? Kajizungushia ukuta hataki ifahamike nyumbani kunawaka moto. Nikaamua kumwambia ukweli kuwa nina faili lake lote. Lahaula. Uso unakuwa mwekundu. Ile aibu ya kiume haijifichi. Lakini, hata hivyo, anafanyaje mke mwenyewe keshamwaga mchele?

 

Godi, kiume, anatoa maelezo yanayoonesha hana kesi ya kujibu: “Hakuna mwanaume anaweza kuvumilia makelele. Unajua saa nyingine mtu unalazimika kupotea nyumbani ukatulize kichwa. Hawa wanawake ni wajinga sana,” anapangua malalamiko ya mke wake. Nahoji kujua hayo makelele yenyewe ni yapi?

 

“Kila mnapokaa mzungumze na mtu ni malalamiko tu. Unakaa nyumbani kufanya nini?” Namwelewa Godi. Kuna kale kahulka cha wanaume kupenda sifa na heshima hata kama hastahili. Halafu kuna ile mwanaume huwa hakosei. Kidogo inahitaji hekima kumwambia vitu asivyoweza kuvipatia ufumbuzi. Ukimsikiliza Godi unaona kabisa hizo ‘kelele’ ni yale matarajio ya mkewe anayojua hana majibu nayo. Hapo nikataka kujua kwa nini anakuwa hana majibu. Je, anafahamu kweli mahitaji ya mkewe?

 

Msikilize Godi: “Ninampa kila anachohitaji. Hana shukrani yule mwanamke. Mwezi unapoanza nanunua kila kitu kinachohitajika nyumbani kwa jumla. Mshahara wake wala siuulizii na bado kila mwezi nampa posho. Nimpe nini zaidi?” anajigamba kiume. Godi hajui kuwa mke anahitaji zaidi ya hayo. Hajajifunza moyo wa mke wake unahitaji nini. Hajui lugha ya mapenzi ya mke wake. Kutokufahamu afanye nini kumridhisha mke wake ndio kunamchanganya zaidi Godi. Kila mke wake anapojaribu kuusemea moyo wake, Godi anaona anasumbuliwa. Mkewe akileta agenda ya kuusemea moyo ndiyo kwanza jamaa yangu anaona anapigiwa ‘makelele.’

 

Ni malezi yanayoututumua mfumo dume? Labda. Wanaume wengi hawajihangaishi kabisa kuijua hiyo lughafichi ya mwanamke. Kuna kile kiburi cha kiume kwamba, “Usinisumbue. Nakupa hela na bado unalalamika, unataka nifanye nini? Sasa sirudi nyumbani na hutonifanya kitu.” Kishunuzi tunasema, hapo mwanaume huwa kaamua kujificha. Hataki kujua zaidi. Hataki kuelimishwa. Chochote unachomwambia kinatishia heshima yake kama mwanaume. Kwa haraka haraka, anaona bora akafurahishe watu ‘wanaomwelewa’ ambao wengi hata hawafahamu jina lake la pili.

 

Uamuzi wa ‘kujificha’ nao hutengeneza tatizo jingine kubwa zaidi. Kwanza, hakutani na mtu anayethubutu kuhoji uanaume wake. Wengi anaoshibana nao wanaongozwa na kile kibwagizo: “Furaha! Ni kuwa na marafiki. Furaha! Ni kulewa na marafiki.” Kazi inabaki kuwa moja tu. Kujibamba. Kupiga soga zisizojeruhi uanaume wa yeyote gengeni. Mpira. Siasa. Dini. Kazi. Majigambo ya kiume, "Nimeanzisha biashara mpya." "Nimepanda cheo kazini nk." Hivyo. Ikitokea urafiki umekolea kidogo basi soga linaweza kujikita kwenye kuelezea ‘ujinga wa wanawake.’ Unajua saa nyingine mkishirikiana matatizo mnapendana. Mnajiliwaza.

 

Sasa hapo Mungu aepushie mbali. Mwanaume huyu asikutane na wanawake wanaojua kutumia fursa zinazojileta. Mpango wenyewe wa siku hizi umebadilika. Nipe nikupe. Hawa wanawake wa kibepari wanajua kabisa wanaume wengi wanaozurura mtaani hawawezi kupenda. Kubwa kwao ni tamaa. Inaitwa kutuliza kichwa. Kwa nini ujitafutie matatizo na mume wa mtu? Si unaweza kumfanya chanzo cha mapato na maisha yakaenda?

 

Hayo ndio mazingira niliyomkuta nayo Godi. Kukiri moto unawaka ndani ya ndoa hawezi. Kusema ana mpango mwingine wa kumsaidia ‘kutuliza kichwa’ nayo ni aibu. Tunamsaidiaje ndugu yetu, mwenzetu, Godi aka baba Glady asiyetaka mke awe na kitambi kama chake?


Niandikie: bwaya@learninginspire.co.tz

Maoni

  1. The greatest enemy of a man is the ignorance of self .

    Wale wa Biblia wanasema Asiyejali wa kwao ni Mbaya kuliko asiyeamini.
    Ni ujinga wa Nafsi ya God unaomsumbua, Pamoja na sifa njema lukuki ambazo God huzionesha Mtaani na Mahala popote nje na Nyumban Kwake na Nyumban Kwake kuwa na sura hiyo Bado hakuwezi kumdhihirishia God kuwa Mtu Mwema na anafanya hivyo kama kupunguza hatua Kwa Yale anayoyafanya Nyumban kwa familia yake.

    Nashauri God ayaangalia mambo katika uasili wake na sio katika Ufahamu Wake, Ikiwa alimchagua Mkewe na kuamua kufunga naye Ndoa awe Mkewe na mama WA watoto wake Basi inampasa afanye Moja ya haya mawili.
    1:Arejee Maisha yake ya awali na Mkewe kabla ya Mke kubadilika kiumbo, awe karibu na Mkewe kuona ni namna gani Hicho kitambi kibadilike au kiwe Fahari kwake
    2. Aamua sahihi Kwa namna ya kuhamisha Nyumban wema anauotenda Kwa watu Halafu amor Mkewe muda na kipaumpele zaidi, Hata Yale anayoyaona ni Bora Kuliko Mkewe, yatakuwa ni ya kawaida kabisa.

    IELEWEKE kuwa Mengi ya Mabadiliko ya wake katika Ndoa zetu, wanaume ni Chanzo

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?