Usipompata utotoni, ukubwani atakutoroka

 


Kuna umri ukifika maisha hudai vingi. Tunakimbizana na pilika za kuongeza kipato. Tunapambana na majukumu mengi kiasi kwamba wazazi tulio wengi tunakosa muda wa kuwa karibu na watoto. Ukaribu hapa ukiwa na maana ya kumsikiliza mtoto, kuelewa maendeleo yake na ha
ta kujua nini kinausumbua moyo wake. Ingawa wazazi wengi tunaelewa fika kwamba watoto wanatuhitaji, lakini sasa tufanyeje na mambo yalivyomengi?

 

Simulizi la rafiki yangu Slaquara linaweza kukusaidia mzazi kufikiri upya vipaumbele vyako katika maisha. Katika mazungumzo yetu kuhusu familia, Slaquara ananisumulia jambo linalonishangaza kidogo:

 

“Mzee wangu analalamika sana kwamba siwasiliani naye. Namwelewa. Inaweza kupita hata mwezi mzima sikumbuki kuulizia hali yake. Kwa umri wake kusubiri kupata habari zake kupitia kwa mke wangu si sawa.” Namfahamu Slaquara kama mcha Mungu anayejali sana watu. Hili la kumtelekeza mzazi wake limekaaje?

 

“Hata sijui. Lakini ni kama sina kabisa habari naye. Hata tukionana huwa sina mambo mengi ya kuzungumza naye. Tunasalimiana ndio inakuwa basi. Juzi hapa nilimleta hapa kwangu apate matibabu. Nimetumia fedha nyingi kumtibia. Lakini huwezi amini, aliporudi Karatu, ni kama ufahamu wangu umemfukia.”

 

Mke wake Slaquara, mwanamke mwema, mchangamfu na muongeaji. Hapa anaingilia kati kidogo kueleza namna anavyosaidia kurejesha mawasiliano kati ya mumewe na baba yake, “Mara zote mimi ndio huwa ndio nakukumbusha kumpigia mzee. Sikulaumu lakini ni jambo ambalo kweli mwanzoni mwa ndoa yetu lilinisumbua sana. Nilikuwa najiuliza kwa nini huna mawasiliano na baba yako?”

 

“Lakini unaelewa sio kwamba simpendi…” anajitetea Slaquara na sote tunaangua kicheko chenye maswali.

Ushunuzi unatambua uhusiano mkubwa kati ya malezi na tabia zetu ukubwani. Tunayokutana nayo utotoni yana nguvu ya kuamua tunavyokuwa ukubwani. Namwuuliza Slaquara anachokumbuka utotoni. Maisha yake na baba yake yalikuwaje?

 

“Baba yangu alikuwa mkali sana. Sikumbuki ni wakati gani nikiwa mdogo niliwahi kufurahia uwepo wake kama baba.” Slaquara ananyamaza ghafla. Huenda kagundua kaponyokwa na siri. Uso wake unajaa aibu. Namwona akilazimisha tabasamu. Nahisi ni kama anakumbuka matukio mengi yanayomwuumiza. Sote tunampa muda achague cha kutuambia.

 

Slaquara anavunja ukimya: “Mzee alikuwa mtata sana. Hakuwa mtu wa kufikika. Ungeweza kumsogelea karibu kabisa na wala asijue upo. Mke wake anajisikia huruma. “Jamani. Hapo unatia chumvi.” Slaquara hamjibu.

 

Kwa mbali machozi yanalenga lenga, “Kuna siku nakumbuka tunatembea kwenda kanisani. Darasa la nne au tano kama sijasahau. Baba yuko mbele anapiga hatua kubwa za kiutu uzima na mimi na utoto wangu nalazimika kumkimbilia. Natamani baba anisubiri anishike mkono niende naye sambamba. Baba wala hajali kuna mtoto anamfuata kwa nyuma.” Wote tunacheka kwa masikitiko. Tunaponyokwa na pole isiyotarajiwa, “Inatia huruma jamani!”

 

Slaquara anatuonesha namna mtoto kimaumbile anavyotamani kuwa karibu na mzazi wake. Ufahamu wa mtoto unatafsiri kujali kama kitendo cha mzazi kupunguza mwendo na kumshika mkono. Masikini baba yake hakuelewa.

 

Slaquara anatusimulia desturi ya wa-Iraq. Baba na mama, kwa kawaida walilala nyumba tofauti kwenye boma lile lile. Baba, kwa kawaida, alilala na wanae wa kiume. “Tulikuwa tunalala na baba kitanda kimoja. Kwetu mie nilikuwa mdogo zaidi. Kitu kilichokuwa kinaniuma enzi hizo ni saa za kulala zimefika natamani tukalale na baba na baba hata hana habari. Niliishia kwenda zangu kulala kinyonge nikiwa very dissappointed. Kuna namna nilijisikia kiumbe wa ziada kwenye ratiba za baba.”

 

Utoto wa Slaquara ulijaa upweke. Moyo wa Slaquara ulisukwa sukwa na njaa isiyoshibishwa. Hamu ya kuwa karibu na baba haikuwahi kutimizwa. Kidogo kidogo, Slaquara aliukubali ukweli kama anavyoeleza hapa, “Nadhani utakuwa sahihi. Sikuwahi kulifikiri hili kabla ya mazungumzo haya lakini nadhani ni kweli nilianza kukuuishi uhalisia nisioupenda kwamba ukaribu na baba yangu ni jambo lisilowezekana.”

 

Tunajifunza nini hapa? Wahenga walisema maisha ni mzunguko. Baba, ambaye miaka ile hakuona umuhimu wa kuwa karibu na mwanae, leo uzeeni anatamani kuwa karibu na Slaquara Slaquara alijifunza kuishi peke yake. Kibao kimegeuka.


Niandikie: bwaya@learninginspire.co.tz 

Maoni

  1. Nimefurahi sana kuona Unarejea katika Mtandao Tena Mkuu.
    Ninakushukuru sana

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?