Young Scientists Tanzania: Kujenga utamaduni wa kutafuta ufumbuzi wa matatizo yetu kisayansi

YAMEKUWEPO madai ya siku nyingi kwamba elimu yetu haijaweza bado kutufundisha kufikiri sawa sawa. Kwamba tunafundishwa kukariri, kukumbuka na kurudia rudia yale yale tunayofunindishwa madarasani. Hatufundishwi zaidi ya nadharia za mambo yanayojulikana tayari. Hatufundishwi kuyatazama mambo kwa macho ya kutafuta kujua yasiyojulikana. Matokeo yake, tunaambiwa, hata wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu, wamekuwa wakipata taabu kujifunza namna sahihi ya kufanya tafiti kama sehemu ya Shahada zao.

Nini sababu ya hali hii?

Mwonekano nje ya ukumbi wa Diamond Jubilee jioni hii. Picha: @bwaya
Wengine wanasema, hatujaweka msisitizo kwenye sayansi, kwa maana ya kutafiti. Kutafuta majibu ya matatizo yetu kwa njia za kisayansi.
Inasemwa, hali iko hivi kwa sababu shule zetu hazijawezeshwa. Resources. Siku zote wimbo umekuwa ni ule ule kwamba "Serikali, serikali, serikali", "Shule zetu hazina maabara...wala vifaa",  "Kukosekana kwa maabara, maana yake ni kupungua kwa uwezo wa kutafiti, na hivyo kukosekana kwa uwezo wa kuelewa matatizo yetu kwa kina na kuyapatia ufumbuzi".

Madai haya yanaweza kuwa na ukweli kwa kiasi fulani. Tumekuwa tukifundishwa Sayansi kama historia ya yaliyofanywa. Msisitizo haujawa kwenye kuyaelewa mazingira yetu na kubaini matatizo halisi yanayotukabili na kuyatafutia ufumbuzi, na badala yake, tumekuwa tukisomeshwa mambo yasiyotuhusu moja kwa moja.

Young Scientists Tanzania inajaribu kufanya nini?

Young Scientists Tanzania, taasisi inayohimiza tafiti kwa vijana, kwa ushirikiano na Serikali, inajaribu kuziba pengo hilo. Tangu kuanzishwa kwake, mwaka 2011, Young Scientists Tanzania imekuwa ikihamasisha wanafunzi kufikiri kwa bidii yale wanayofundishwa, na kuona namna wanavyoweza kuyatumia kujaribu kutatua matatizo yanayowazunguka kwa njia za kisayansi.
Maandalizi ya sehemu ya maonyesho Diamond Jubilee. Picha: @bwaya

Tunapozungumzia Sayansi, hatuna maana tu ya masomo yale yaitwayo ya sayansi, bali, elimu ya kubaini kanuni, kwa kutumia tafiti zilizopangiliwa kwa utaratibu unaoeleweka, ili kumwezesha mtafiti kukusanya takwimu zitakazomwezesha kufikia hitimisho linalokubalika. Kwa maana hiyo, historia pia yaweza kuwa aina moja wapo ya Sayansi, kama ilivyo Fizikia.

Kwa kutumia mfumo wa mashindano yanayoanzia kwa ngazi ya shule na baadae taifa, wanafunzi wanawezeshwa kufikiri kwa makini namna ya kufumbua matatizo yao, kwa lengo la kushinda, lakini wakati huo huo, wakibadili fikra zao kwa sayansi na tafiti.

Young Scientists Tanzania, imeweza kuwafanya wanafunzi kufanya tafiti kwa kutumia vifaa rahisi, mara nyingine bila kulazimika kwenda maabara. Na inapobidi kutumia vifaa ambavyo havipatikani mashuleni, wanafunzi wamekuwa wakihimizwa kupata msaada kwenye taasisi za kitafiti vikiwemo Vyuo Vikuu ili kuweza kufanya majaribio hayo. Kwa jinsi hiyo, kujenga kiungo kati ya shule na taasisi za utafiti.

Inashangaza kuona namna wanafunzi wanavyoweza kufanya mambo makubwa, wakipewa nafasi ya kufanya hivyo. Na mara nyingi, wanafunzi hawa, wamekuwa wakifanya yale ambayo walimu wao, hawajawahi kufikiri kuyafanya. Walimu wanajikuta wakigeuka kuwa wanafunzi kwa wanafunzi wao wenyewe. Enzi mpya.

Maonyesho ya wiki hii Diamond Jubilee

Alama za makundi manne ya tafiti. Picha: @bwaya
Katika kuhakikisha kuwa hilo linafanyika, tangu mwezi Februari mwaka huu, wanafunzi wa shule nyingi za sekondari hapa nchini, kwa msaada wa walimu wao wamekuwa wakifanya tafiti kujaribu kuja na majibu ya matatizo yanayozikabili jamii zao. Wiki hii ni kilele cha shughuli hizo kwa maonyesho ya kitaifa yatakayokuwa yakifanyika kuanzia kesho tarehe 13 mpaka tarehe 14, 2014, katika ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Wanafunzi kutoka kwenye shule zaidi ya 100, katika mikoa 20 ya Tanzania, watashiriki maonyesho hayo ambayo hatimaye yatasailiwa na waamuzi waliobobea katika makundi manne makubwa:
1) Sayansi asilia, kemikali na hisabati  2) Sayansi viumbe na ekolojia  3) Sayansi ya jamii na tabia  4) Teknolojia.

Maonyesho haya, na shughuli nzima kwa ujumla, imedhaminiwa na BG Tanzania, na Irish Aid kama wafadhili wakuu.

 Twitter: @bwaya

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi