Waajiri Wanatarajia Nini kwa Waombaji wa Kazi?

Taarifa ya Utafiti wa Ajira na Kipato ya mwaka 2012, iliyotolewa na Idara ya Takwimu ya Taifa mwezi Julai 2013, inaonyesha kwamba nchi yetu ina waajiriwa rasmi 1,550,018. Kati yao, asilimia 64.2 wameajiriwa katika sekta binafsi na waliobaki (asilimia 35.8) wameajiriwa katika sekta ya umma.

Aidha, taarifa inasema ni asilimia 24.8 pekee ya wafanyakazi hawa, wanapata kipato cha kuanzia Tsh 500,001 kwa mwezi [vipato vya wafanyakazi wengi (asilimia 54.4) ni chini ya Tsh 300,000 kwa mwezi.]

Nafasi za kazi zisizojazwa

Takwimu za taarifa hiyo zinathibitisha kwamba moja wapo ya changamoto zinazokabili soko la ajira hapa nchini, ni kukosekana kwa waajiriwa wanaokidhi matarajio ya ajira. Kwa mfano, wakati kwa mwaka 2011/12 zilikuwepo nafasi za kazi 126,073 nchini kote, ni wafanyakazi wapya 74,474 tu waliweza kuingia kwenye soko la ajira kwa kipindi hicho. Kadhalika, takwimu hizo hizo zinaonyesha kuwa nafasi za kazi zipatazo 45,388 hazikuweza kujazwa katika kipindi hicho.

Pamoja na ukweli kuwa uwezo wa waajiri kuajiri wafanyakazi wapya unategemea sana fedha na maandalizi mengine muhimu, lakini upo ukweli kuwa watafuta kazi wengi hawaonekani kuwa na sifa zinazotarajiwa na waajiri ikiwemo uzoefu kazini.


Kukoseka kwa ujuzi unaokidhi matarajio

Katika kulithibitisha hilo, Baraza la Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA) kwa ushirikiano na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) lilifanya utafiti kujua mitazamo ya waajiri juu ya wahitimu wa vyuo vikuu. Matokeo yalionesha kuwa waajiri hawana imani na weledi na ujuzi wa wahitimu hawa. Madai yao ni kuwa zaidi ya nusu ya watafuta kazi wenye shahada, hawana sifa za kuwawezesha kuajirika. Tanzania, kwa mfano ina asilimia 39 tu ya wahitimu ya vyuo vikuu wenye ujuzi unaokidhi vigezo vinavyohitajika na wajiri wao. 

Kwa matokeo hayo, inavyoonekana, mbali na ukosefu wa ajira, nchi yetu inakabiliwa na tatizo kubwa la watu wanaotafuta kazi, kwa maana ya kuamini wanazo sifa za kupata kazi, lakini kwa upande mwingine, hawaajiriki hata kama kazi hizo zipo. Lakini ieleweke kwamba hapa tunazungumzia kazi zinazohitaji ujuzi wa kusomea.



Kwa upande mwingine, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, katika watu wenye uwezo wa kufanya kazi zozote zile ikiwa ni pamoja na zile zisizohitaji ujuzi rasmi, watu wapatao 2,409,862 wanafanya kazi chini ya uwezo unaotarajiwa kwao katika nchi hii. Hiyo ikiwa na maana kuwa watu wengi wanapoteza muda makazini na hufanya kazi kwa kiwango kidogo mno kuliko ilivyowapasa kufanya.

Tatizo la kutokuajirika

Kwa kawaida imezoeleka kwamba ukosefu wa kazi hutokea katika mazingira ambayo mtu anayeamini kuwa anazo sifa za kuajiriwa, na anayetafuta kazi, anashindwa kupata kazi hiyo.


Kwa mfano, mhitimu wa sayansi ya siasa, mwenye ufaulu mzuri na mwenye nia ya kuajiriwa, anaposhindwa kuajiriwa, tunaweza kusema mhitimu huyo anakabiliwa na tatizo la ukosefu wa kazi. Ikitokea mtu mwenye sifa hizo hizo hatafuti kazi, hatuwezi kusema anakabiliwa na ukosefu wa kazi.

Hata hivyo, mtu anayetafuta kazi na hapati, bado anaweza kuwa na sifa za kuajirika, ikiwa atakuwa na ujuzi, uelewa na sifa zinazomfanya awe katika nafasi ya kuajiriwa kirahisi. Sambamba na hilo, kuajirika ni kuwa na uwezo wa kupata mafanikio katika ajira aliyonayo mtu, kwa maana ya kujinufaisha mwenyewe, mwajiri wake, jamii na uchumi kwa ujumla.

Mtu asiyeajirika, ni yule ambaye, mbali ya kutokuwa na kazi au kushindwa kupata ajira, hana ujuzi wa kiutendaji anaopaswa kuuonyesha kwa mwajiri ili si tu aweze kupata kazi, bali adumu katika kazi hiyo kwa muda mrefu (ikiwa atapenda) bila hofu ya kuikosa kazi hiyo.


Kwa maneno mengine, mtu asiyeajirika, anaweza kuwa na kazi, lakini hawezi kujihakikishia kazi hiyo kwa muda mrefu na hana uwezo wa kuthubutu kuhama kutoka kazi moja kwenda kazi nyingine kukidhi mahitaji yake.

Katika mazingira ambayo asilimia 64.2 wameajiriwa katika sekta binafsi, ambazo mara nyingi huwa ni ajira za muda/mkataba, unaweza kuona athari za kuwa na watu ambao, kwanza hawana ujuzi unaowawezesha kupata kazi, lakini pia hawawezi kuonyesha weledi na ufanisi kazini, na hivyo wanakuwa katika hatari ya kukosa ajira katika kipindi ambacho wangependa kuendelea na ajira hizo.

Kukosekana kwa ujuzi usiotarajiwa

Tafiti nyingi za kazi na ajira zinaonyesha kwamba pamoja na umuhimu wa kuwa na cheti chenye alama za juu, waajiri wengi hawatilii mkazi sana na alama nzuri za darasani. Badala yake, wengi wao huhitaji kuona ujuzi usiotarajiwa na watafuta kazi wengi ambao ndio unaotafsika katika uwezo halisi wa kutumia maarifa na uelewa wa darasani katika kutatua changamoto halisi za kazi.

Kwa maana nyingine, mwajiri anakutarajia wewe unayetafuta kazi uwe na uwezo wa kuhusisha na kuzitumia nadharia, maarifa na kanuni za kitaaluma ulizozisoma darasani katika kufumbua matatizo yanayomkabili ofisini kwake. 


Ndio kusema, kimsingi, mwajiri anahitaji kuona ujuzi mwepesi (soft skills) ambao kimsingi ndio unaomsaidia kuongeza ufanisi wa kazi zake. Ujuzi huu, hata hivyo, ni nadra kupatikana kupitia mfumo rasmi wa kitaaluma. Mtafuta kazi analazimika kuutafuta kwa jitihada zake binafsi.


Inaendelea
Twitter: @bwaya

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi