Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3


PICHA: thesouthern.com


Siku moja nikiwa kwenye maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanafunzi wa shahada za awali waliingia kufanya mtihani wa muhula wa mwisho wa masomo.

Wakati wanaingia, mmoja wao alijigamba kwamba hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kukanyaga maktaba tangu amejiunga na chuo hicho miaka mitatu iliyopita.

Nilishangaa inawezekanaje mwanafunzi wa chuo kikuu kujisifia jambo la fedheha kama hilo.

Hata hivyo, majigambo hayo yanawakilisha mawazo ya wanafunzi wengi wanaofikiri uwezo mkubwa wa kiakili maana yake ni kutokusoma sana. Wanafikiri mwanafunzi anayejituma kusoma kwa upana, kwenda maktaba na  kutumia muda mwingi kwenye masomo huyo ni ‘kilaza’ (hana uwezo).

Hata pale mwanafunzi mwenye bidii anapofanya vizuri, ataitwa kila aina ya majina ya kejeli kwa lengo la kumkatisha tamaa. Wengine watasema ‘ametumwa na kijiji’, ‘msongo’ na majina mengine ya dhihaka.

Kejeli kama hizi husababisha baadhi ya wanafunzi kutokutaka kuonekana wanasoma lakini wakisoma sana ‘mafichoni’. Ikitokea wanafunzi hawa wasioonekana wakisoma hadharani wanafaulu inajengeka dhana nyingine bandia kwamba mwanafunzi ‘mkali’ huwa hasomi sana.

Lakini pia, walimu nao kwa kiasi fulani huchochea mawazo haya. Mwalimu anapouliza maswali yanayomtaka mwanafunzi arudie kile kile alichojifunza anakuza imani potofu kwamba hakuna haja wala sababu ya kusoma mambo  kwa kina.

Inapotokea mwanafunzi anayesoma mambo kwa juu juu na bado anafaulu pengine kuliko mwenzake anayejituma, inajengeka dhana kwamba hata mwanafunzi asipohudhuria vipindi darasani; hata asipokwenda maktaba kujinoa; hata asipoelewa kwa undani bado hatapata hasara. Tutarejea suala hili katika makala zinazofuata.

Natambua kwamba wapo wanafunzi wenye uwezo kuliko wenzao. Uwezo mkubwa huwawezesha kutumia muda mfupi kujifunza jambo na kulielewa kwa kina. Lakini, hata hivyo, hiyo haiwezi kumaanisha kuwa uelewa wa mambo huja bila jitihada.

Nimesoma na watu wengi kwa ngazi zote za elimu. Nawafahamu wanafunzi waliokuwa wazuri sana kwenye masomo. Wanafunzi hawa, mara nyingi, walikuwa na tabia inayofanana. Walijituma zaidi katika masomo kuliko wanafunzi wasio na uwezo.

Hawa ndio wanafunzi ambao hawakuthubutu kukosa kipindi darasani, walisifika kwa nidhamu ya muda, hawakukosekana maktaba na muda mwingi waliutumia kwenye mambo yanayohusiana na masomo.

Tafsiri yake ni kwamba uelewa hauji kienyeji kama wanafunzi wengi wanavyopenda kuamini. Kuelewa kunazaliwa na jitihada za kutosha katika kufuatilia jambo kwa kina na upana wake.

Kwa hivyo, ni dhahiri kwamba mbinu zozote za kuelewa masomo haziwezi kuzaa matunda ikiwa mwanafunzi hatabadili mtazamo na kuanza kuheshimu nafasi ya jitihada katika kujenga uelewa wake.

Kujifunza kabla hujafundishwa

Mwanafunzi wa kawaida husubiri mwalimu afundishe kitu ndipo aanze kukisoma. Hawezi kujaribu kujifunza kitu yeye wenyewe bila msaada wa mwalimu au mwanafunzi mwenzake. Usomaji wa namna hii hupunguza uwezekano wa kujenga uelewa wenye tija kwa mwanafunzi.

Ili kujenga uelewa mzuri wa masomo, ni muhiu ujizoeze kumtangulia mwalimu. Kabla hujafundishwa kitu, kisome mwenyewe kwanza.

Faida ya kusoma kitu kabla hujapata msaada wa mtu anayejua zaidi yako ni kuitengenezea akili yako mtaji wa kufikiri. Unaposoma mwenyewe unaishughulisha akili yako kujaribu kufanya mambo tuliyokwisha kuyajadili kwenye makala zilizopita.

Itakapofika wakati wa kufundishwa, mwanafunzi aliyejenga msingi atakuwa na muda wa kufikiri zaidi kuliko mwenzake anayekwenda kusikiliza kwa mara ya kwanza.

Pia, kadri mwalimu anavyofundisha utajua kipi unakielewa, kipi ni kipya na hivyo kukuweka kwenye nafasi ya kupata msaada mzuri zaidi ukiwa darasani. 

Soma kwa kufuata mpangilio

Mojawapo ya tabia za wanafunzi wa kawaida ni kutokuwa na utamaduni wa kusoma. Muda mwingi wanautumia kufanya mambo mengine yasiyohusiana na masomo wakiamini wana muda wa kutosha kufanya hivyo siku za mbeleni.

Mazoea haya huzaa tatizo la kuja kulazimika kusoma mambo mengi kwa wakati mmoja pale wanapolazimika. Mwalimu akitangaza jaribio, au mtihani unapokaribia, huo ndio unakuwa wakati wa kujifunza mambo mapya.

Mara nyingi mtu anaposoma mambo mengi kwa wakati mmoja huishia kusoma kijuu juu. Katika mazingira ambayo mwalimu naye hatauliza maswali ya uelewa, mazoea haya hushamiri na kugeuka kuwa tabia isiyo na tija kwa mwanafunzi.

Ikiwa una nia ya kuwa mwanafunzi mwenye kuelewa mambo kwa upana, usiwe na tabia ya kusubiri wakati fulani ndipo uanze kusoma usiku na mchana. Kusoma kuwe tabia endelevu isiyohitaji kushtukizwa na mitihani.

Ili ufanikiwe, jenga tabia ya kusoma mambo kidogo kidogo kwa kuyagawanya kwa muda mrefu. Mfano, badala ya kusoma mada nzima kwa siku moja, unahitaji kujipa muda wa kutosha kusoma mada ndogo ndogo kwa ratiba utakayojipangia.

Kuna faida nyingi za kufanya hivi. Kwanza, utakuwa na muda wa kutosha kujitathmini hatua kwa hatua na hivyo kubaini maeneo  unayohitaji kuweka nguvu zaidi.

Pili, utakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kutumia vyanzo mbalimbali kusoma kitu kile kile bila kuwa na wasiwasi na muda ulionao. Tulishaeleza kwamba ukifanya hivi unaongeza uwezekano wa kupanua uelewa wako vizuri zaidi.


Fanya maswali yanayofikirisha

Kufanya maswali ni mbinu muhimu inayokuza uelewa wako. Unapofanya maswali unakuwa unatumia maarifa mapya katika kutafuta majibu.

Hata hivyo, si kila maswali yanaweza kukuza uelewa wako. Kuna maswali mengine yataishia kukufanya ukumbuke tu kile ulichokisoma. Maswali haya yanakusaidia kujenga kumbukumbu lakini yanaweza yasisaidie kukuza uelewa wako.

Nakumbuka nilipokuwa sekondari tulizoea kwenda kwa mwalimu mmoja wa tuisheni aliyetufundisha majibu ya maswali ya mitihani iliyopita. Tulitumia muda mwingi ‘kumeza’ majibu ya maswali hayo hata kama hatukuwa tunaelewa.

Mitihani ilipokuja na maswali yenye mitego tusiyoifahamu, mambo yalikwenda mrama kirahisi. Hapo unaweza kuona kwamba wakati mwingine unaweza kufanya maswali mengi kama njia ya kukwepa usomaji mpana. Huwezi kujenga uelewa mpana kwa njia hii.

Ili tabia ya kufanya maswali ikusaidie, hakikisha unaposoma unatumia maarifa unayoyafahamu tayari. Soma kwa upana, kisha fanya maswali yanayohusiana na kile ulichosoma.

Pia, ni muhimu pia kufanya maswali yasiyo na jibu moja au yanayohitaji njia tofauti kufikia jibu husika. Maswali ya namna hii yanakujenga kufikiri kwa upana ili kutafuta mifano hai inayopatikana katika mazingira yako.

Ni dhahiri huwezi kuwa na majibu yote kwa kila swali. Jambo la kuzingatia ni kwamba kufanya maswali ni sehemu ya tathmini binafsi ya maendeleo yako. Unapokosa majibu, rudi kwenye vitabu na vyanzo vingine vya maarifa. Vitabu visipokupa majibu, mtumie mwalimu au mwanafunzi anayeelewa eneo hilo kuliko wewe.

Maoni

  1. PROAKUN.WIN | AGEN BANDARQ | QQ ONLINE | DOMINOQQ | BANDARQ ONLINE | JUDI ONLINE TERBAIK DI INDONESIA, adalah Website Rekomendasi Situs Situs Terbaik dan Ternama dengan Hasil Winrate Teringgi Terbaik Di Indonesia.

    Agen BandarQ
    QQ Online
    DominoQQ
    BandarQ Online
    Judi Online

    JibuFuta
  2. ดูหนังออนไลน์ฟรี หนังออนไลน์ที่คมชัดเต็มระบบ ทั้ง 4K HD สนุกง่ายๆ กับ Parasite ชนชั้นปรสิต (2019)

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Pay $900? I quit blogging

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini