Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -2

PICHA: Shutterstock


Katika makala yaliyopita tuliona mbinu tatu unazoweza kuzitumia kuelewa mambo unayojifunza. Kwanza, ni ‘njaa’ inayokusukuma kuelewa. Unapokuwa na ari ya kuelewa jambo, mara nyingi, utahamasika kulielewa bila kutumia nguvu nyingi.

Pili, tuliona ni muhimu kutengeneza picha kubwa ya jambo unalojifunza kabla hujaanza kujifunza undani wa mambo madogo madogo ndani ya picha hiyo.

Kwa mfano, unaposoma aina za vyakula, lazima kwanza uelewe vyakula. Uelewa wa jumla wa vyakula utakurahisishia kazi ya kuchanganua aina zake kwa sababu tayari unayo rejea utakayoitumia kuelewa zaidi.

Mbinu ya tatu ni kukihusisha kitu unachokisoma na mambo unayoyafahamu tayari. Unaposoma aina za vyakula, kwa mfano, lazima uwe unafikiria vyakula mbalimbali unavyovifahamu katika mazingira yako.

Unapojaribu kuhusianisha kile unachokisoma na maisha yako ya kila siku, unaurahisishia ubongo wako kazi ya kupokea kuliko kuingiza kitu kipya kisichohusiana kwa vyovyote vile na kile kilichopo kwenye ufahamu tayari.

Katika makala haya, tunaendelea na mbinu nyingine tatu zinazoweza kukusaidia kuyaelewa na kuyamiliki maarifa.

Jitathmini kadri unavyosoma

Nakumbuka kuna wakati tulikuwa tukisoma darasani usiku. Mwenzetu mmoja alitoka nje kujinyoosha apunguze usingizi kabla hajaendelea na mkesha.

Bwana mmoja aliyekuwa anapenda masihara aliamua kwenda kubadilisha ukurasa wa kitabu ambacho mwenzetu huyu alikuwa anakisoma. Baada ya dakika kadhaa, mwenye kitabu alirudi na kuendelea kusoma kwenye ukurasa ule ule uliobadilishwa bila yeye kujua.

Ndivyo wanavyosoma wanafunzi wengi. Wanatumia muda mrefu kusoma bila kutathmini kile wanachokisoma. Hili ni kosa kubwa kwa mtu mwenye kiu ya kuelewa.

Bila kufanya tathmini, unaweza kuingiza mambo mengi kichwani lakini hujui yanakwenda kuhifadhiwa kwenye eneo gani ubongoni mwako. Kama tulivyosema, ni vyema kinachoingia kwenye ubongo wako kielekezwe kwenye eneo linalohusika ili iwe rahisi kukitumia.

Jifunze kujifanyia tathmini kadri unavyosoma. Jiulize namna gani kile unachokisoma kinahusiana na mambo unayoyafahamu.

Tuchukulie unasoma aina za vyakula vinavyosaidia kujenga mwili. Kadri unavyosoma yaliyoandikwa, unahitaji kujiuliza namna gani hicho unachokisoma kinaleta maana.

Je, kinafanana na kitu gani unachokijua tayari? Kama tulivyokwisha kusema, maarifa tunayojaribu kuyaelewa yanahusiana na mambo tunayokutana nayo kila siku. Kama huuoni uhusiano huo maana yake ufahamu wako haupati kitu. Rudia tena.

Lakini pia, kadri unavyosoma jiulize namna gani hicho unachokisoma kinatofautiana na kile unachokijua. Mambo gani unayoyasoma yanayopingana na yale unayoyafahamu tayari?

Ipo kanuni ya ujifunzaji inayosema, ‘kama unachokisoma hakijakufanya usielewe, basi huelewi.’ Maana yake ni kuwa kuelewa ni matokeo ya kuondoa hali ya kutokuelewa inayojitokeza kadri unavyoingiza maarifa mapya kwenye ufahamu wako.

Kwa hiyo unapoendelea kusoma, ni muhimu kutathmini namna gani maarifa hayo mapya yanavyokosoa uelewa uliokuwa ili ubaini maarifa mapya unayoyapata.


Tumia vyanzo tofauti

Wanafunzi wengi hupenda njia ya mkato katika kujifunza. Wanapopata maandishi rahisi yanayowasaidia kujibu mtihani, mfano madesa, wanaishia hapo. Mazoea haya, hata hivyo, huwafanya ‘waegeshe’ maarifa kwa sababu inakuwa vigumu kuyaelewa kwa undani wake.

Ikiwa unapenda kuwa na uelewa mzuri wa jambo unalojifunza, ni muhimu ujenge mazoea ya kutumia vyanzo tofauti vya maarifa. Kwa mfano, soma vitabu vingi vinavyoelezea jambo hilo hilo. Baada ya kusoma kitabu cha kwanza, tafuta kitabu kingine kinachoelezea kitu kile kile.

Uzoefu unaonesha kwamba wakati mwingine unaposoma jambo lile lile kwenye kitabu kingine, akili inaweza kukudanganya kuwa tayari unaelewa na hivyo huna sababu ya kuendelea. Usidanganyike.

Ukweli ni kwamba kila kitabu kina namna tofauti ya kuelezea jambo hilo hilo. Kupitia tofauti hizi za uwasilishwaji wa maarifa, uelewa wako utaimarika zaidi.

Lakini pia, katika kusoma vitabu vilivyoandikwa na waandishi tofauti uwezekano ni mkubwa utakutana na mkanganyiko wa maarifa. Kile ulichokisoma kwenye kitabu cha awali sicho kinachoonekana kwenye kitabu cha pili.

Mkanganyiko wa namna hii si jambo baya. Mkanganyiko ni afya katika kujifunza. Bila mkanganyiko itakuwa vigumu kupanua uelewa wako.

Unapokutana na mikanganyiko chukulia hiyo kama fursa ya kubaini maeneo unayohitaji kupata msaada wa mwalimu wako au mwanafunzi mwenzako mwenye uelewa zaidi.

Uzuri ni kwamba siku hizi teknolojia imerahisisha ujifunzaji. Ukiingia kwenye mtandao wa YouTube, kwa mfano, unaweza kupata video mbalimbali zinazofafanua jambo ulilolisoma kwenye vitabu. Katika kutazama video hizi, uelewa wako utaimarika zaidi kwa sababu mule utakutana na michoro, maelezo ya picha ambayo kwa hakika yataimarisha uelewa wako.

Sambamba na kutumia vitabu na namna nyingine za kuhifadhia maarifa, usiache kumsikiliza mwalimu. Mwalimu hufundishwa namna ya kurahisisha maarifa yaendane na mazingira yako.

Kazi ya mwalimu ni kupunguza ugumu wa lugha ya vitabuni ili iendane na lugha unayoielewa zaidi. Mwanafunzi mwenye tabia ya kumsikiliza mwalimu kwa makini, kwa kiasi kikubwa, anajipunguzia kazi ya kutafsiri maarifa ambayo wakati mwingine yanawekwa kwenye isiyoeleweka kwa urahisi.

Wafundishe wengine

Kama tulivyotangulia kusema, huwezi kuwa na uelewa mzuri wa jambo kama bado hujalifanya liwe sehemu ya maisha yako. Usipoweza kuyamiliki maarifa unayojifunza, hayatakusaidia.

Ili uweze kuyamiliki maarifa, lazima ufanye kazi ya kuyatumia katika maisha yako halisi. Hatua ya kwanza ya kutumia maarifa yako ni kuwafundisha wengine.

Unapowafundisha watu wengine unafanya mambo mawili kwa pamoja. Kwanza, unalazimika kutafuta lugha nyepesi kuelezea jambo ambalo wakati mwingine ulitumia siku nzima kulieleza. 

Huwezi kumfundisha mtu kwa kutumia maneno yale yale yaliyotumika kwenye kitabu. Lazima utatumia maneno yako mwenyewe yatakayomsaidia mwenzako kuelewa. Kufanya hivi kutakusaidia wewe mwenyewe kuelewa kwanza.

Pili, katika kuwafundisha wengine utabaini maeneo ambayo bado hukuyaelewa vizuri. Haya ni maeneo ambayo pengine hukutumia muda wa kutosha kuyaelewa au yalikuwa na ugumu zaidi ya maeneo mengine.

Kupitia kuwafundisha wengine utaweza unajirahisishia kazi ya kuyaelewa maeneo hayo ‘korofi’ na kuyashughulikia kwa wakati.


INAENDELEA

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Fumbo mfumbie mwerevu