Namna ya Kutambua Kazi ya Wito WakoKuna mawazo yanapandikizwa kwenye fahamu za vijana kuwa mafanikio hayaji bila mtu kufanya aina fulani ya kazi. Wahubiri wa mawazo haya wanapima tija na heshima ya kazi kwa mizani ya kipato.

Mtazamo huu,  kwa kiasi kikubwa, unachochewa na mfumo wa kibepari unaotukuza faida anayopata mtu binafsi dhidi ya manufaa mapana ya jamii. Katika mfumo huu, mtu anaweza kufanya kazi yoyote almuradi inamnufaisha yeye binafsi.

Mawazo kama haya ya kuweka mbele fedha, kwa kweli, yanakwenda kinyume na utamaduni wetu wa kijamaa unaopima ufanisi wa mtu kwa kutazama mchango alionao katika kuwasaidia wengine.

Tunafahamu, kwa mfano, wazee wetu wengi waliitumikia jamii yetu kwa uadilifu lakini walistaafu wakiwa watu wanaoishi maisha ya kawaida. Heshima yao haikuwa namna walivyojitengenezea himaya zao za kimaslahi, bali namna walivyoweza kutumikia wito wao.

Kizazi hiki cha sasa kinaanza kuupa mkono utamaduni huo. Vijana wa mjini wanasema, ‘sasa tunapambana na hali zetu.’ Kila mtu anapigania maslahi yake kwa kutumia njia zozote halali na haramu.

Mwelekeo huu umefanya watu wavamie kazi zisizo za wito wao kwa sababu tu zina harufu ya kuwaharakishia mafanikio ya kifedha. Watu hawa hujikuta wakifubaza uwezekano wa kufanikiwa kinyume na matamanio yao. Sababu ni kufanya kitu sahihi lakini kisichokuza ile mbegu inayoishi ndani yao.

Katika makala haya, naiita mbegu hii wito, na ninapendekeza mbinu nne unazoweza kuzitumia kuibaini na kuikuza kupitia kazi unayoifanya.

Kitu gani kinakugusa?

Kila mtu analo eneo la maisha linamvutia kulifuatilia kwa karibu. Kuna kitu ambacho ukikisikia kinazunguzwa mahali moyo wako unasisimka. Unapokuwa kwenye mazungumzo na watu wengine, masikio yako yanasikia kitu hicho hata kama watu wengine hawakisikii. Unanunua vitabu, unafuatilia televisheni na mitandao na karibu kila unachokifanya kinazunguka zaidi kwenye eneo hilo hilo.

Unapoendelea kusoma hapa tayari kuna kitu kinakujia kichwani. Inawezekana ni matatizo fulani ya watu, hitaji fulani unalofikiri jamii yetu inalo au ubunifu fulani unaoamini bado jamii haijauona.

Pia, huenda ni masuala ya teknolojia. Inawezekana ni mfumo fulani wa maisha, imani au fikra katika jamii unazofikiri ungepewa nafasi ungezibadilisha. Chochote kile kinachogusa fikra zako, hicho ndicho kinachoweza kuwa wito wako. Ukifanya kazi zinazogusa eneo hilo unaweza kufanya vizuri zaidi.

Unajitambulisha na kitu gani?

Kwa kawaida, kuna vitu tukivifanya vikaleta matokeo fulani tunajisikia fahari. Kila mtu ana eneo lake akilifanya vizuri anajisikia kuridhika.  Kuna watu wanajisikia fahari wanapotetea haki za watu; wengine kufundisha; wengine uandishi; kubuni vitu vipya; kuongoza wengine; kushauri, kuendesha biashara, kutaja kwa uchache.

Kile kinachokuletea ufahari, mara nyingi, utapenda kujitambulisha nacho. Utatumia muda mwingi kukielewa kuliko unavyofanya kwenye maeneo mengine.

Nina rafiki yangu daktari mzuri lakini mara zote hujitambulisha kama mwandishi. Mazungumzo yake mengi hujikita kwenye uandishi kuliko udaktari na sisi tunamtambua kama mwandishi kuliko daktari. Hii ndiyo sifa ya wito. Unaweza kufanya kazi nyingine lakini kinachokupa hali ya utoshelevu kikawa kitu kingine kabisa.

Jiulize, kitu gani ukikifanya vizuri unajisikia fahari? Je, watu wanakusifia na kukutambua kwa kitu gani? Ukiweza kuuoanisha uwezo huo na kazi unayoifanya itakuwa rahisi kupata mafanikio makubwa zaidi.

Unayatazamaje mafanikio?

Mafanikio ni dhana pana isiyo na jibu moja. Kila mtu ana namna yake ya kutafsiri kile kinachoitwa mafanikio. Wapo wanaochukulia mafanikio kama uwezo wa kujikusanyia mali. Hawa huridhika wanapokuwa wamefikia kiwango cha kujitosheleza na vitu vinavyowawezesha kuishi maisha mazuri.

Wengine mafanikio yao ni umaarufu katika jamii. Vitu vinavyowafanya wajulikane ndivyo wanavyovichukulia kama mafanikio. Wengine wanakwenda mbali zaidi. Hawaridhiki na fedha wala umaarufu bali mamlaka. Wasipopata madaraka yanayowapa nguvu ya kuwatawala wengine, bado hawajisikii kufanikiwa.

Pamoja na hao, wapo pia wanaopima mafanikio yao kwa namna wanavyotatua matatizo ya watu wanaowazunguka. Hawa, hawaishii kuridhika na maisha mazuri bali kuona  maisha yao yanagusa watu wengine.

Tafsiri ya mafanikio uliyonayo, ni kiashiria kimojawapo cha wito ulionao katika maisha. Wito wako hutengeneza mtazamo fulani wa mafanikio. Ukiweza kuoanisha tafsiri uliyonayo ya mafanikio na kazi unayoifanya uwezekano ni mkubwa kuwa kufanya vizuri zaidi.

Maamuzi gani unayafurahia?

Kipimo cha juu cha wito ni aina ya maamuzi unayoyafanya. Kuna nyakati unaweza kufanya maamuzi ambayo si kila mtu anaweza kukuelewa lakini wewe mwenyewe ukawa na amani na kile unachokifanya.

Kuna kijana aliwahi kuacha kazi yenye kipato kikubwa ili akafanye kitu alichoamini kinabeba thamani yake. Aliacha kazi ambayo watu wengi wangetamani kuipata na akaenda kuanzisha biashara. Mtu wa namna hii kwa vyovyote anakuwa na wito wa ujasiriamali ndani yake. Ili wito huo ukamilike inakuwa ni lazima afanye maamuzi magumu.

Jiulize, umewahi kufanya maamuzi gani yaliyobadili mwelekeo wa maisha yako? Ikiwa kuna maamuzi unatamani kuyachukua ukiamini yatabadili maisha yako, huo inawezekana ndio wito wako.

Wito hubeba mafanikio yako

Mafanikio katika kazi mara nyingi hujipua kama mbegu inayoota kwenye wito alionao mtu. Kila mtu ana mbegu yake. Kwa mfano, hata tungependa kujiajiri si kila mtu anaweza. Wapo watu ambao hata wangewezeshwa kujiajiri bado hawatafanya vizuri. Kujiajiri si wito wao.

Kadhalika, si kila mtu anaweza kuajiriwa. Kuna watu wana wito ndani yao wa kutengeneza mifumo inayoajiri watu wengine. Wito wao ni kusimamia mawazo yao na kuyageuza kuwa ajira. Ndio maana ni muhimu kuutambua wito wako.


Unapoutambua wito wako unajiweka kwenye nafasi ya kujitoa kikamilifu kwenye eneo lililobeba thamani yako. Hutajaribu kufanya vitu vingi kwa sababu unajua iliko thamani yako na wapi pa kuelekeza nguvu zako. 

Maoni

  1. nimejielewa zaidi..Asante sana.

    JibuFuta
  2. Ujumbe umetembea katika hisia zangu. Mi ni mwalimu mwanafunzi katika masomo ya chemistry & biology. Lakini naishi na ndoto za kuwa muigizaji na mtunzi wa vitabu vya stori kama tamthiliya na makala mbalimbali. Tayari nimeanza michakato ya kukamilisha ndoto hizo, ualimu ninaosomea nataka kuutumia namna hii sasa sijui nitakuwa upande gani baada ya kuoanisha ninachosomea na ndoto zangu!

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Fumbo mfumbie mwerevu