Mbinu za Kujenga Ujuzi wa Mwanafunzi

PICHA: Shutterstock


Nakumbuka siku ya kwanza kusikia neno ‘cell’ nikiwa kidato cha kwanza haikuwa kazi rahisi kupata picha kamili. Mwalimu wetu aliandika ubaoni, ‘cell is a basic unit of life.’ Niliduwaa. Sikujua anamaanisha nini zaidi ya kutazama kamusi kujua maana ya maneno aliyoyatumia.

Mwalimu alirudia maneno hayo hayo kuweka msisitizo, na kisha akatafsiri kwa Kiswahili. Alisema, ‘maana yake ni hivi kuna kitu kidogo kisichoonekana kwa macho kwenye miili yetu kinachofanya tuishi. Mmeelewa?’  Kwa kweli hatukuwa na namna nyingine zaidi ya ‘kuelewa’ na tukaitikia, ‘ndiyo!’

Mwalimu alifurahi na akatupa muda tunakili sentensi hiyo kwenye madaftari yetu. Tulifanya hivyo ingawa ni wazi hatukuwa tukielewa anaongelea nini.

Kazi iliyofuata ilikuwa ni kukariri sentensi hiyo bila kuelewa ina maana gani. Tulifikiri kukumbuka ndio kuelewa.

Mtihani ulipokuja tulijibu vile vile bila kukosea na mwalimu alitupa alama za juu kwa kurudia kile kile alichokuwa ametukaririsha. Lakini ukweli ni kwamba hatukuwa tumeelewa ‘tulichomeza.’

Changamoto ya ufundishaji

Huu ni mfano wa namna ufundishaji unavyochangia kwa kiasi kikubwa kufanya maarifa yanayokusudiwa na mtalaa yakose maana kwenye maisha halisi ya wanafunzi.

Tunasoma vitu vingi tusivyoviona kwenye maisha yetu ya kila siku. Matokeo yake tunaishia kukumbuka na kufaulu mitihani kwa kiwango cha juu lakini thamani yetu kimaarifa ikibaki vile vile.

Tunamaliza shule lakini hatujui tunawezaje kutumia maarifa hayo kubadilisha maisha yetu kwa sababu ukweli ni kwamba hatuoni uhusiano wa wazi kati ya kile tulichojifunza shuleni na maisha yetu ya kila siku.

Ikiwa tunataka kubadili hali ya mambo, mahali pa kuanzia ni kuwekeza kwenye maandalizi madhubuti ya walimu. Kama nilivyoeleza kwenye makala yaliyopita, mwalimu ndiye anayebeba dhima ya elimu. 

Bila mwalimu aliyeandaliwa vyema, hatuwezi kuona matunda ya sera nzuri za elimu, mitalaa mizuri, madarasa bora na hata vifaa bora vya ujifunzaji na ufundishaji.

Mwalimu aliyeandaliwa vyema na kufuzu kazi ya kutafsiri mtalaa katika maisha ya mwanafunzi, anaweza kuibua na kuchochea udadisi kwa mwanafunzi wake.

Jitihada za wadau

Katika makala yaliyopita, tulitumia mfano wa mradi wa Next Generation Leaning (NGL) unaoendeshwa na Shirika la Opportunity Education Foundation kujifunza namna mwalimu anavyoweza kuifanya kazi hii kwa ufanisi.

Tuliona kanuni mbili. Kwanza, mwalimu anahitaji kumfanya mwanafunzi aone namna gani kile anachofundishwa darasani kinagusa maisha yake ya kawaida. Kujua uhusiano uliopo kati ya maudhui anayojifunza na maisha yake, kunamfanya athamini maudhui husika na hivyo kuwa na ari ya kujifunza.

Pili, mwalimu anahitaji kumjengea mwanafunzi uwezo wa kujiuliza maswali ya msingi kuhusu maudhui anayojifunza. Kanuni hii inamsaidia mwanafunzi kupunguza utegemezi kwa mwalimu na hivyo kujenga hali ya kujiamini kuwa anaweza kushiriki kwenye mchakato wa ujifunzaji.

Kukuza ujuzi

Kanuni ya tatu ni kumtarajia mwanafunzi kutumia maarifa yake kujitengeneza ujuzi. Mwanafunzi wa NGL si tu anahitajika kujibu maswali ya kufikirisha, bali kuonyesha ujuzi mahususi.

Mathalani, baada ya mwanafunzi kujifunza namna mimea inavyotengeneza sukari kwa kutumia mwanga wa jua, lazima aoneshe anavyoweza kutumia maarifa hayo kutatua changamoto anazokabiliana nazo katika mazingira yake.

Hali halisi katika shule zetu ni tofauti. Mwalimu humtarajia mwanafunzi kukusanya na kukariri maarifa. Kipimo cha ujifunzaji ni kwa kiwango gani mwanafunzi huyu anajua kutoa maelezo sahihi ya nadharia za kitaaluma.

Mwanafunzi anayesoma mada ya Uchafuzi wa Mazingira, kwa mfano, anatarajiwa kukusanya, kukariri na kuelewa maelezo mengi kuhusu uchafuzi wa mazingira.

Mwanafunzi huyu mwenye taarifa nyingi kuhusu uchafuzi wa mazingira bado anaweza kuvumilia kuishi na takataka zilizo karibu na makazi yake bila wasiwasi. Kwa mtindo huu, uelewa wa uchafuzi wa mazingira hajaweza kumsaidia kuona tatizo na kulitatua.

Kwa mwanafunzi huyu uchafuzi wa mazingira ni ‘mambo ya shule’ yasiyohusiana na maisha yake halisi ambayo hata hivyo yanaweza kumsaidia kufaulu mitihani yake vizuri.

Katika zama hizi za ukuaji wa mawasiliano, maarifa ya kila namna yanaweza kupatikana. Mtu yeyote mwenye ujuzi wa namna ya kutumia mtandao wa intaneti anaweza kutafuta na kupata chochote anachotaka kujifunza.

Kuendelea kusisitiza kwenye kumbukumbu ya maarifa kimsingi si kumtendea haki mwanafunzi. Maarifa hayapaswi kuwa lengo la elimu. Tunahitaji kuongeza thamani kwa kwenda mbele ya maarifa.

Ujuzi ni maarifa yanayozalisha

Badala ya mwalimu kumjazia mwanafunzi maelezo mengi, anahitaji  kulenga katika kukuza uwezo wa mwanafunzi kutumia maarifa anayoyapata katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto halisi zinazomkabili.

Uwezo huu unaitwa ujuzi. Mtu mwenye ujuzi kwa hakika anaweza kufanya vitu vinavyoonekana kama ushahidi kuwa amejifunza maudhui fulani.

Kwa mfano, katika kufundisha mada ya uchafuzi wa mazingira, mwalimu asiishie kumjaza mwanafunzi nadharia na maelezo mengi yanayohusiana na uchafuzi.

Badala yake, aende hatua moja mbele kwa kumjengea mwanafunzi uwezo wa kuona matatizo yanayofanana na kile anachojifunza na kujaribu kutafuta majibu yanayolingana na kiwango chake cha uelewa. Huko ndiko kutumia maarifa kujipatia ujuzi, kanuni muhimu sana ya mradi wa NGL.

Mwalimu wa NGL, kwa mfano,  mbali na kuhakikisha mwanafunzi anahusianisha kile anachojifunza na maisha yake, anatarajiwa kukuza ujuzi wa mwanafunzi kwa kufundisha katika namna inayochochea utafutaji wa majibu.

Ufanisi wa somo unapimwa kwa namna mwanafunzi anavyoweza kutazama nje ya darasa na kubaini matatizo yanayoweza kutatuliwa kwa kutumia maarifa aliyonayo.

Mwanafunzi ashirikiane na  wenzake

Tunafahamu kuwa wanafunzi hutofautiana uwezo. Wapo wanafunzi wenye uelewa mkubwa wa mambo kuliko wengine.

Kadhalika, kila mwanafunzi ana namna yake bora zaidi ya kujifunza. Wapo, kwa mfano, wanaojifunza kwa kusikia, wengine kwa kutazama, wengine kwa kufanya.

Kwa kuzingatia ukweli huo, mradi wa NGL unayo kanuni ya nne inayomtaka mwalimu kumwezesha mwanafunzi kujifunza akishirikiana na wenzake.

Kupitia majadiliano, mwanafunzi anapata nafasi ya kusikiliza uzoefu na uelewa wa wenzake ambao kwa hakika unaweza kuwa tofauti na wa kwake.

Pia, kwa kuwa majadiliano haya yanafanyika katika mazungumzo ya kawaida na marafiki, mwanafunzi anakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kufurahia kile anachokisoma.

Ingawa walimu wetu wamekuwa wakifundishwa mbinu hii ya kuwashirikisha wanafunzi katika ujifunzaji, mara nyingi utekelezaji wake umekuwa na changamoto nyingi.

Walimu wengi, kwa mfano, hupata shida kujua ni wakati upi mwanafunzi ashirikiane na wenzake na anaposhirikiana na wenzake afanye nini. Matokeo yake walimu huendelea kutumia mbinu za kimazoea zinazowanyima wanafunzi fursa ya kushiriki kwenye mchakato wa ujifunzaji.


INAENDELEA

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia