Mambo Yanayoweza Kumvutia Mwanamume kwa Mwenzi Wake -1

Swali hili huulizwa na karibu wanawake wote wanaotamani kuwa na uhusiano wa kudumu na wanaume. Kwamba mambo yepi hasa yanayoweza kumvutia mwanaume pale anapoanzisha uhusiano na mwanamke.
Ingawa zipo tofauti ndogo ndogo miongoni mwa wanaume, kwa ujumla, uchambuzi wa tafiti mbalimbali za mahusiano unabainisha mambo kadhaa yanayowaunganisha wanaume wengi kimahitaji. Tuyatazame katika mfululizo wa makala hizi.



Kutambuliwa uwezo wake

Mwanaume anatamani kujisikia ni shujaa asiyeshindwa. Fahari ya mwanaume siku zote ni uwezo anaoamini anao unaomfanya mara nyingine awe tayari kufanya mambo yanayoweza kuhatarisha maisha yake kwa lengo tu kuthibitisha kuwa wanaweza. Ndio kusema kutambuliwa uwezo wake ni hitaji la msingi.

Kama unatamani mwanaume umpendaye aanze (aendelee) kuvutiwa na wewe, chukua hatua ya kubaini vitu vya pekee alivyonavyo na onesha  kwa dhati kuwa unavitambua. Kwa kawaida kila mwanaume anayo maeneo yake anayoyaweza vizuri kuliko wengine.
Inawezekana ikawa ni uwezo fulani wa kipekee ambao si wanaume wengi wanao. Huenda ni tabia fulani maalum ama ujuzi, maarifa na sifa nyingine za kipekee unazojua anazo. Inawezekana ni uaminifu wa muda, kujali familia yake, kuwahi nyumbani na kushiriki kazi za ndani, ufuatiliaji wa mambo kwa karibu, bidii ya kazi, ucha Mungu na mengineyo kama hayo. Chukua hatua ya kumfanya afahamu unauelewa uwezo alionao.
Katika mazingira yetu ya ki-Afrika, wakati mwingine tunaogopa kuwatambua watu kwa sifa zao nzuri hata kama tunazitambua sifa hizo. Wakati mwingine tunafikiri kile chema anachokifanya mtu ni wajibu wake usiostahili kutambuliwa.
Hata haivyo, ni vyema kama mwanamke ujifunze kusema wazi kwa moyo wa dhati, kwa kurudia rudia, kuwa unatambua uwezo wa mume wako. Ukifanya hivyo utamfanya ajiamini zaidi, awe na moyo wa kuchangamka zaidi na atajaa nguvu za kufanya vizuri zaidi ili awe shujaa wako.

Anahitaji kuheshimiwa

Heshima ni hitaji kubwa kwa binadamu yeyote anayejitambua. Tunapenda watu watufikirie katika hadhi ya juu. Ndio maana mtu yeyote anayetufanya tujione hatuna hadhi tunazozitaka, ni rahisi kutofautiana naye. Hii ni hulka ya kawaida ya binadamu.
Kwa mwanaume hitaji la kuheshimiwa ni kubwa zaidi. Tunapozungumzia heshima kwa mwanaume, katika mazingira yetu, tunamaanisha hali ya kutamani kujiona yu na hadhi ya juu, yu na mamlaka zaidi pengine kuliko mwanamke. Kinyume chake ni kudharauliwa, kuwekwa katika mazingira ya kujiona hana hadhi, hana mamlaka, asiye na kauli wala uwezo kufanya lolote bila mwongozo wa mwanamke.

Kwa wanaume wengi, heshima ni namna unavyoongea nae, maneno unayoyatumia katika kueleza mawazo yako, ishara za mwili wako katika mazungumzo, kumpa nafasi ya kwanza katika maamuzi na mambo kama hayo.

Heshima, vile vile, ni kumstahi mwanaume unayempenda hata anapokosea. Kosa linapotumika kama sababu ya kufanya vitendo vinavyodhalilisha hadhi yake ni kujipunguzia alama. Ndio kusema, staha ni kuongea naye kwa nidhamu hata katika mazingira ambayo ni dhahiri yeye ndiye mkosaji.

Kadhalika, heshima ni kuwa tayari kumtunzia hadhi yake kwa watu wengine. Kumjengea taswira inayomwongezea thamani yake kwa watu unaojua anawaheshimu. Kuonesha fahari yako kwake unapoongea na watu wengine kwa kauli, matendo na hisia kunaongeza alama za sifa anazozitafuta.


Anatamani kusikilizwa, sio kukosolewa

Wanaume wengi hawapendi kukosolewa hata kama hawasemi. Unapomkosoa mwanaume unamfanya apoteze hali ya kujiamini na hivyo hujisikia kama mtu anayeongozwa. Si wanaume wengi hufurahia kuongozwa. Kinyume na kumkosoa, ifanye sauti yake isikike.


Tuchukulie mfano kuwa mwenzi wako amekuja na wazo la kufanya jambo fulani analodhani ni muhimu mlitekeleze. Kwa mwanamke msomi mwenye uwezo wa kuchambua mambo, wakati mwingine ni rahisi kubaini kwa haraka hitilafu ya pendekezo analolitoa.

Kwa haraka, unaweza kuonesha upinzani wa wazi wazi kuwa kinachopendekezwa hakina mashiko. Si wanaume wengi wanaweza kuvumilia kuonekana wana mawazo yasiyo na mashiko hata kama ni kweli.


Hulka ya mwanaume kutamani kuwa na sauti, inaweza kumfanya mwanaume aamue kusisitiza wazo lake akiamini ana haki ya kuungwa mkono. Si busara hata kidogo kumpinga wazi wazi kwa lugha inayolenga kuonesha mapungufu yake. Kufanya hivyo kunamnyong’onyeza, hali ambayo hatakubali itokee.

Ikiwa unataka kukamata moyo wa mwanaume, jifunze kushuka na kumtanguliza katika maamuzi. Linda hadhi ya mume wako kwa kuonesha heshima kwa mawazo yake. Ukiweza kugusa moyo wake kwa kuonesha umuhimu wa anachokisema, itakuwa rahisi kutoa pendekezo lako kwa namna ambayo ni rahisi kupokelewa.

Soma sehemu ya pili inayoendeleza makala haya.
Twitter: @bwaya

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia

Pay $900? I quit blogging