Namna mahitaji ya kihisia ya wenzi yanavyosababisha misuguano ya kimahusiano na ndoa

PAMOJA na dini nyingi kubwa kupiga marufuku talaka kwa waumini wake, takwimu rasmi za Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) zinaonyesha kwamba talaka nchini zimeongezeka kwa asilimia 49 katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2009. Kwa upande wa Zanzibar pekee, tunaambiwa, asilimia 95 ya migogoro 1,753 ya ndoa iliyosajiliwa kwenye Mahakama ya Kadhi nchini humo iliishia kwa talaka. Hali inatisha, au sio?

Katika hali halisi, shauri ya utamaduni wa kuyaonea aibu masuala ya kuachana, hali inaweza kuwa mbaya zaidi. Watu wengi wanaweza kuwa wanaugulia maumivu ya ndoa na kuamua ama kufa na tai shingoni, au kutafuta 'michepuko' ya hapa na pale katika jitihada za kupunguza maumivu.

Katika nchi za Ulaya, ambako kidogo kuna uhuru wa mtu kufanya atakalo ikiwa ni pamoja na kuomba talaka, hali ni tete zaidi. Kwa mfano, tunaambiwa, wakati idadi ya ndoa zinazofungwa mwaka 2010 ilipungua kwa asilimia 39 barani humo, talaka zimeongozeka kwa asimilia 200 katika kipindi cha mwaka 1979 mpaka 2010.

Takwimu hizi zinaonyesha namna taasisi ya ndoa inavyoendelea kupoteza umaarufu wake kwa kasi huku watoto wengi wakiendelea kuzaliwa nje ya ndoa. Katika nchi nyingi za Ulaya, asilimia zaidi ya 50 ya watoto wanazaliwa nje ya ndoa. Iceland oekee kwa mfano, asilimia ya watoto wanaozaliwa nje ya ndoa imefikia 66.9 mwaka 2012. Hapo hatujazungumzia mimba zilizotolewa pamoja na kukithiri kwa matendo ya uzinzi na uasherati ambayo ni matokeo ya michepuko ya wanandoa waliochoka maisha ya ndoa.

Ingawa jambo hili limekuwa likifanyiwa utafiti tangu zamani, kwa sasa limeanza kuvutia hisia za watafiti wengi zaidi kufuatia ongezeko hilo la talaka. Jambo linalohitaji majibu ya hakika na makini ni kwamba iweje wapenzi wanaoanza mapenzi yao kwa msisimuko kujikuta katika hali ya kuchokana na hata kuachana katika kipindi kifupi? Kwa nini wapenzi waliooana kwa 'harusi ya kufa mtu', kwa furaha na nderemo za matumaini makubwa, wajikute wakizozana kwa hasira na uchungu, wakipigana, kupishana, kuchokana na hata kufikia kuhisi suluhu pekee ni ama 'kuchepuka', 'nyumba ndogo' au kuachana rasmi? Tumekosea wapi? Kwa nini ndoa inazidi kuwa taasisi iliyo kwenye hatari ya kupotea?

Tafiti zinasemaje kuhusu mitazamo ya wanandoa wanaotengana?

Utafiti uliofanywa na Amato na Previti na kuchapishwa kwenye Jarida la Masuala ya Familia mwaka 2003, unaonyesha kwamba watu wengi wanaachana kwa sababu ya hisia za kukosekana kwa uaminifu, wenzi kushindwa kuwasiliana, hisia za kukosekana mapenzi na hivyo wenzi kujikuta wakijisikia watu wasio na furaha tena na mengine mengi.

Tafiti za awali zimefanya jitihada ya kujua sababu za kuchokana huko kwenye ndoa kwa kutazama makundi mbalimbali. Tukianza na jinsia, watafiti Levinger; Cleek & Pearson; Kitson; Bloom, Niles & Tatcher kwa nyakati tofauti walichunguza mitazamo ya  wanaume na wanawake kuhusu sababu ya migogoro. Wanaume wanaorodhesha sababu kama vile wanawake kuwa wazinzi na kutumia muda mwingi kazini kuliko nyumbani, kukosekana mawasiliano baina ya wenzi, kubadilika kwa vipaumbele, kama sababu kuu.

Wanawake kwa upande wao wanataja ulevi na uzinzi wa wenzi wao wa kiume; mwanaume kushindwa kuihudumia familia yake kifedha; udhalilishaji wa kihisia na kimwili hali inayosababisha furaha kutoweka na kutokuendana kitabia kama tatizo kuu.

Kadhalika, tafiti nyingine zilizofanywa na Kitson, Levinger na Goode kwa nyakati tofauti, zimejaribu kutazama uwezo wa kifedha na elimu katika matatizo haya.
Ndoa na mahusiano ni mada inayouza vitabu kwa wingi Picha: @bwaya

Kwa upande wa familia zenye uwezo kifedha na kielimu, matatizo yanadaiwa kusababishwa na utoto wa wenzi,  kwa maana ya uelewa wa kiakili wa wanandoa; ubinafsi wa mwezi mmoja wapo; kukosekana kwa mawasiliano; kubadilika kwa vipaumbele vya wanandoa; kukosekana mapenzi na madai mengi yasiyoisha ya mwenzi; kutokuendana kitabia na misuaguano ya kimsimamo.

Familia zenye uwezo duni wa kifedha na kielimu zinataja mambo yafuatayo kuwa chanzo cha migogoro; kudhalilishwa kihisia na kimwili, kukosekana kwa uaminifu (uzinzi); kutelekeza familia; matatizo ya kifedha na kazi, ulevi na ukatili/unyanyasaji wa kimwili.

Vile vile Kitson aligundua kwamba wenzi wanaoana wakiwa na umri mkubwa, misuguano hutokana na ulevi, kutokuwepo kwa hisia za kifamilia, migogoro inayotokana na malezi ya watoto na matatizo ya majukumu yanayotakiwa kutekelezwa katika familia. Kwa wenzi wanaooana katika umri mdogo, mambo kama kukosekana kwa uzoefu wa ndoa, mwenzi mwingine kutoka kirafiki na marafiki wengine, uzinzi na kushindwa kuwasiliana huchangia kuchokana.

Nini kiini kikuu cha matatizo haya yanayosababisha migogoro ya ndoa?

Hizi zinazoitwa "sababu za kuachana" na wenzi kwa hakika huwa ni matokeo ya tatizo kubwa (core problem) ambalo kwa kawaida, huwa limezama ndani mno kiasi cha kutoweza kuonekana kirahisi. Kwa lugha nyingine, kinachoonwa na wenzi kuwa ndilo tatizo  -uzinzi, ubinafsi, kutelekeza familia, kuwa na vimada, misimamo, kazi na kadhalika- huwa ni udhihirisho tu wa tatizo lisiloonekana.

Katika mtiririko wa makala zitakazofuata, tutajaribu kutazama, hatua kwa hatua, chanzo kikuu cha misuguano ya ndoa. Tutajaribu kuonyesha namna hitaji la kihisia (emotional need) lilivyo muhimu kwa wenzi na namna gani wenzi wanaposhindwa kutimiziana mahitaji hayo ya kihisia kwa wenzi wao, kwa kutokutambua au kutambua, husababisha matatizo ya hapa na pale ambayo yanapoachwa yakamea, yanaweza kusababisha utengano mkubwa unaoanzia kwenye hisia na kisha kuzorotesha mahusiano kwa kiwango tulichoona.

Tutajaribu kuonyesha namna mwanaume alivyo na hitaji kubwa la hadhi na mamlaka yake ya uanaume kutambuliwa na kulindwa, hitaji ambalo inapotokea halitimilizwi na mwanamke husababisha utupu unaweza kusababisha mwenzi kuwa tayari kufanya mambo yasiyofikirika kwa hali ya kawaida ambayo hatimaye huleta matatizo makubwa.

Vile vile tutaonesha namna wanawake kwa asili walivyo na hitaji kubwa la kujisikia salama kihisia kwa  kuonyeshwa wanapendwa na waume zao. Kadhalika tutaona namna wanaume wasio na muda wa kulishughulikia hitaji hili muhimu, hubomoa mahusiano yao wenyewe na kusababisha tabia ambazo hazikutegemewa kwa wake zao.

Mtu anaweza kujiuliza, "Kijana, kwa umri wako mteke, huna uzoefu wa ndoa, una mamlaka yepi ya kuandika mambo nyeti kama ya ndoa?"

Well, idadi ya miaka kwenye ndoa haiwezi kuwa pass ya kuyaelewa masuala ya kimahusiano na kwamba uzoefu bainafsi hauwezi kuwa generalized kwa watu wengine.

Ndio kusema kwamba, maandishi haya ni matokeo ya kusoma tafiti mbalimbali za kimahusiano, neno kwa neno, zilizofanywa na watu wanaoheshimika katika mambo ya kimahusiano na wala si mtazamo wala maoni yangu binafsi.

Hali kadhalika, ingawa kabati langu la vitabu laweza kuwa na vitabu vya waandishi mbalimbali kati ya 45 -50, sikumbuki idadi kamili ya vitabu nilivyowahi kuvisoma vinavyojadili uzoefu tofauti tofauti wa mambo ya mahusiano na ndoa.

Hapo utaniambia, "Bwana mdogo, uko kinadharia sana wewe! Haya mambo ni nyeti na yanahitaji uzoefu!" Well, ingawa kupitia vitabu na tafiti hizo nimeweza kupata kanuni za msingi zinazoongoza mahusiano ambazo zinapovunjwa, wenzi huwa katika hatari kubwa ya misuguano, sikuishia kwenye kanuni. Nilikwenda mbele zaidi.

Katika kujaribu kanuni hizo, nimekuwa nikizungumza na wanandoa niliwaona  mimi kuwa bora, angalau kwa macho. Nilifanya vivyo hivyo kwa ndoa nilizoziona kama zenye matatizo, angalau kwa wenzi wenyewe kukiri hivyo, kama jitihada za kujihakikishia kuwa angalau, kwa kiasi fulani nahalisisha kanuni hizo. Kwa njia hiyo, nimeweza kuthibitisha uhalali wa kanuni hizo katika mazingira ya Kiafrika.

Hata hivyo, si malengo ya makala hizi kumwambia msomaji nini anachopaswa kufanya. Hilo litakuwa kinyume kabisa cha malengo makuu ya blogu hii ambayo imelenga kutoa taarifa za jumla ambazo msomaji mwenyewe hupaswa kuzipima na kuona ikiwa zina msaada wowote kwake kufuatana na mazingira yake. Lengo la blogu hii halijawahi kuwa kumkaririsha msomaji 'mbinu', na itabaki kuwa hivyo.

Ingawa ni kweli haya yaliyoandikwa yalikuwa ni jitihada binafsi za kuboresha mahusiano yangu mwenyewe, upo uwezekano kuwa kanuni hizo kuweza kuwasaidia na wengine. Tafadhali fuatana nami katika mfululizo huu unaojaribu kuonyesha namna duara la mgogoro wa kimahusiano linavyofanya kazi na jinsi wenzi wanavyoweza kulivunja duara hilo kwa makusudi.

Twitter: @bwaya

Maoni

  1. Bahati mbaya sana wale tunaotarajia kuingia kwenye ndoa na wale tulioko kwenye ndoa hatujibidishi kufahamu ni kwa namna gani tunapaswa kuishi na wenza ili kuepuka migogoro au kutengana kabisa. Ni hivi majuzi nilikutana na marafiki zangu, ni wadogo zangu, kwa bahati nzuri wao wameshaoa, kaka yao bado. Lakini walinishauri nisioe kwani kwenye ndoa kuna matatizo mengi na wanajuta na hivyo kuwa rahisi pia kushawishi wengine wasiingie huko. Nilishirikishwa pia kuhusu wenzi waliokuwa mbioni kuachana kwa sababu ya migogoro isiyoisha. Ninachotaka kusema hapa ni kuwa, hili ni tatizo kubwa kwa jamii ya sasa, elimu hii ni ya msingi sana, ni hitaji la muhimu kabisa kwetu vijana. Panapo uwezo, nitawaongoza ndugu hao wapitie makala hizi kwa ajili ya kujiongezea ufahamu wa masuala ya kimahusiano.

    JibuFuta
  2. Albert, nimefurahi kukuona hapa. Karibu tujadili suala hili ambalo, kama ulivyoonesha mwenyewe, limekuwa tete mno na linadai majibu yanayoeleweka.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?