Kukosoa, kutafuta makosa, si tabia njema

Siamini kwamba ukosoaji ni asili ya mwanadamu.

Kufikiria kinyume (negative). Kwamba watu wote wanakosea isipokuwa wewe. Kwamba watu wote wamepotea isipokuwa wewe. Kwamba watu wote wanahitaji msaada isipokuwa wewe.

Kufikiria ubaya zaidi wa jambo kuliko uzuri wake. Kufikiria udhaifu kuliko ubora wake. Kufikiria uharibifu zaidi kuliko uboreshaji. Kwamba unaweza kusoma kitabu cha mwandishi fulani, si kwa sababu unataka kujifunza, bali kupekua wapi kakosea. Kwamba unaweza kuzungumza habari za mtu, si kwa nia ya kujenga, bali kwa nia ya kumtafutia makosa yake.

Kwamba watu wanaweza kukwambia jambo zuri na la manufaa, lakini wewe ukalichukulia kwa mtazamo hasi. Ukakosoa.

Kwa nini iwe rahisi zaidi kufikiria udhaifu/ubaya wa mtu/suala kuliko kufikiria uzuri wake? Hivi mwanadamu anavutiwa na nini kutafuta kasoro?


Je, kutafuta/kupekua kasoro ni asili ya mwanadamu ama ni tabia inayojiotea kulingana na mazingira ya mhusika?

Maoni

  1. Kuna ile wanasema mkanyage bahati mbaya akuumize makusudi.Kwa sasa binadamu tunaangalia mabaya zaidi ya mazuri.

    Tunaumizana makusudi.

    JibuFuta
  2. Kwanza kabisa hakuna ukweli wala uwongo. Kwa hiyo naweza nikasema ni kweli kutafuta kasoro ni asili ya binadamu maana kuna wakati utakuta mtu anatafuta kila njia ili ampe mwingine kasoro au akipe kitu kasoro

    JibuFuta
  3. @Edigio, nakubaliana na wewe kabisa kwamba binadamu tunaumizana kwa makusudi. Je, kwa nini tunaumizana kwa makusudi? Ingekuwaje kama kila mtu angekuwa anatafuta kumfurahisha mwenzie na sio kumuumiza?

    @Yasinta: Asante kwa wazo lako kwamba hakuna ukweli wala uwongo. Nakubaliana na wewe. Lakini je, kwa sababu inaonekana kila mtu ni mtafuta kasoro maana yake ni kwmaba hiyo ndiyo asili yetu?

    Asanteni kwa mchango

    JibuFuta
  4. Bwaya habari za siku.Ulichokisema ni kweli watu wengi tumelelewa katika kuutafuta udhaifu au makosa ya mtu na ndiyo tunachokina zaidi kuliko uimara wake.Hiyo siyo asli ya mwanadamu ila ni malezi ambayo tumefundishwa na wazazi nyumbani,walimu mashuleni na jamii iliyotuzunguka.
    Vitabu vya dini vinatuambia tumeubwa kwa mfano wa Mungu,sasa Mungu huyo ambaye ametuumba mbona haangalii kasoro zetu??
    Hii inaonesha kuwa tabia ya kukosoa ni ya kufundishwa na wanadamu wenzetu tena wake wasiojiamini na wenye kutazama mambo kwa upande mbaya.

    JibuFuta
  5. Nuru karibu tena. Niliyakosa mawazo yako kwa muda mrefu. Karibu tena tuendelee kubadilishana mawazo humu.

    Nakubaliana na mawazo yako kabisa kwamba inawezekana ni malezi. Je, ni aina gani ya malezi inayotufinyanga kuwa watu wa kutazama mambo kwa upande mzuri? Ungetoa miano iliyo bayana ingekuwa vyema zaidi kwa faida ya wasomaji wengine.

    Nashukuru kwa kutupa sababu nzuri kwamba kuwa "too negative" si asili ya mwanadamu hata kama binadamu wote wanaonekana kuwa hivyo.

    JibuFuta
  6. Ndugu bwaya na wengine.Ndugu bwaya ameniuliza ni aina gani ya malezi ambayo inatufinyanga tuwe tunatizama mambo kwa upande mzuri?lakini nadhani alikuwa akimaaanisha kutizama mambo kwa upande hasi/mbaya,kama nitakuwa nimekosea nitaomba anisahihishe.Kutizama mambo kwa mkabala hasi ni jambo ambalo tumekuwa tukifundishwa kila siku na watu ambao kwa namna moja au nyingine tumepita katika mikono yao kimalezi,na mbaya zaidi ukipita mikononi mwa wasiojiamini ndiyo hatari zaidi.Chukulia mfano mtu ameamaka asubuhi akajiandaa kwenda kazini akavaa nguo zake safi na akapendeza,njiani anakutana na watu wanamwagia sifa kedekede kuwa kapendeza sana hadi anajisikia vizuri ghafla anatumiwa ujumbe mfupi kwenye simu yake toka kwa mpenzi wake kuwa ameuvunja uhusiano wao,mtu huyu hili jambo la kukataliwa ndilo ambalo litachukua nafasi kubwa sana katika mawazo yake kuliko kule kusifiwa lakini angeweza kufikiria jinsi watu walivyokuwa wakimsifia jinsi alivyopendeza na akapata nafuu,lakini kwa sababu umefundishwa kuwa kukataliwa ni kubaya then ndilo litakalo kuwa kichwani haikuwahi kutokea hata siku moja ukafundishwa kusifiwa nako ni kuzuri zaidi.Mfano mwingine katiak kuelezea namna ya kuangalia mambo kwa mkabala hasi ni pale mtu anaposifiwa kwa kujenga nyumba nzuri,badala ya kusema asante nimejenga nyumba ile nzuri ili nikae pazuri yeye utamsikia akisema kakibanda tu kale,ukweli hatujawahi kufikiri mambo kwa upande chanya.Hatujawahi pia kuambiwa kukosea ni kuzuri zaidi kwani ndiyo unapopata nafasi ya kujifunza,tumeambiwa kukosea ni kubaya sana,mfano tunauona tulipokuwa wadogo siku tukipata maksi nzuri darasani wazazi wetu walitumwagia sifa nyingi na siku tukapata maksi za chini tuliadhibiwa sana hatukuwa kuambiwa kuwa tumefeli labda kwa sababu tumezidisha michezo ila tuliadibiwa,hali hii na nyinginezo za kufanana ndizo zinazopelekea watu wengi tukawa tunatazama mambo kwa mkabala ambao ni hasi.

    JibuFuta
  7. Nuru,

    Nilichelewa kuuona mchango huu mzuri. Asante kwa kuelewa kosa la kiuchapaji. Haraka haraka haina uhariri.

    Mjadala unaendelea.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?