Jifunze kusikiliza kuliko kusema

Kusema ni rahisi kuliko kusikiliza. Kumsikiliza mtu ni kazi ngumu. Hasa kama anayezungumza anaonesha kuwa na mawazo unayodhani yanatofautiana na mawazo yako ama pengine yanapingana kwa kiasi kikubwa na mawazo yako.

Kazi inakuwa kubwa kweli kweli hasa inapoonekana kama vile mzungumzaji ana uelewa mdogo kuliko wako. Yaani anapozungumza unahisi kama unaelewa anakokwenda, anachotaka kusema, anawaza nini na kwa nini anataka kusema hivyo anavyovisema. Unaelewa na unashindwa kujizua kuonyesha hisia hizo na hivyo unathubutu kuingilia sentensi zake.

Kumsikiliza mwenzio na kusoma mawazo ya mwenzio si kazi rahisi. Ni kazi ngumu kweli kweli.

Ni bahati mbaya sana kwamba wengi wetu tunapenda kusema. Tunapenda kusikilizwa. Tunapenda watu wengine wasikilize zaidi mawazo yetu kuliko sisi tunavyowasilikiza wao. Pengine ni kwa sababu ya ile hulka kwamba "Ninajua..."

Hatuwezi kuukana umuhimu wa sisi kujitahidi kujifunza kwa bidii kuwasikiliza wenzetu. Sababu ni kwamba vile tunavyovijua ni vichache mno ukilinganisha na vingine vinavyofahamika kwa watu wengine. Na kama ni hivyo basi unaona namna ambavyo ni muhimu kwetu kuwasikiliza watu wengine kuliko tunavyoweza kusema tunayoyajua. Na vivyo hivyo ni muhimu kwetu kusoma mawazo ya watu wengine kuliko tunavyoweza kudai kusomwa za wengine.

Kama unatabia ya kupenda kuzungumza zaidi uwapo na watu. Ama kuonyesha kwa namna fulani kwamba wewe unajua zaidi ya huyo anayeongea, pengine kwa kumkata kata kauli, kuingilia ingilia anachotaka kusema kabla hata hata hajamaliza, ni busara kuanza kubadilika sasa. Uanze na hatua ya kwanza kwa kukubali kwamba tabia hiyo itakujengea ukuta na watu wengine (hata marafiki) na hivyo kukupunguzia wigo muhimu katika kujifunza mambo mapya.

Jifunze kusikiliza kwa utulivu, na inapobidi kusema kwa tahadhari kuanzia dakika hii unapomaliza sentensi hii.

Maoni

  1. Kaka hongera kwa mada zenye ukweli,plz hebu nitumie email kwenye email yangu
    godlistensilvan@gmail.com

    JibuFuta
  2. Kwa uzoefu wangu mimi naona ni vizuri kusikiliza na pia kusikilizwa kwani sipendi kama namsikiliza tu mtu halafu yeye hanisikilizi mimi/wengine. Mfano mzuri watoto wadogo wao kila mara wanapenda sana kusikilizwa na ni rahisi sana kwa wao kuona/kugundua huwasikilizi. Pia wao pia ni wasikilizaji wazuri sana. Sikiliza na usikilizwe.

    JibuFuta
  3. Anony hapo juu asante kwa kutembelea kibaraza hiki. E-mail? Nitafanya hivyo hivi punde.

    @Yasinta. Ulichosema ni sahihi. Mawasiliano yananoga ikiwa kila upande unatamani kusikiliza zaidi upande wa pili kuliko kinyume chake. Inapendeza kama nini ikiwa ninapozungumza na mtu, ninachofanya kwa bidii ni jitihada za kumsikiliza anachotaka kusema zaidi (na sio kuwaza nimjibuje kwa kirefu) halafu na yeye hali kadhalika akifanya hivyo. Kwa hiyo mimi nadhani suala la mawasiliano lapaswa kuanza kwa mtindo wa wajibu zaidi kuliko matarajio. Kwamba mara nyingine hata kama ninayezungumza naye haonekani kunisikiliza basi tu maadam ninaelewa kuwa kumpa nafasi ya kusema ni wajibu wangu wa msingi, napaswa kumsikiliza.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Makundi Manne ya Tabia za Watoto Kitabia

Uislamu ulianza lini?