Furaha ni uamuzi wako mwenyewe, amua

KILA mtu angependa kuwa mwenye furaha. Wapo wanaamini kuwa lengo la maisha ya mwanadamu hapa duniani ni kuitafuta furaha. Kwamba purukushani zote hizi katika maisha zina lengo la kuisaka furaha. Fikiria vitu kama pesa, elimu, ndoa nzuri, familia, umaarufu na kila kilichojema ambacho mwanadamu hukitafuta kwa bidii lengo ni kuitafuta furaha.

Vitu kama dini kimsingi lengo ni hilo hilo -furaha. Kwamba dini inakuwa ni kimbilio rahisi katika kuyasahau matatizo tunayokumbana nayo hapa duniani kwa mawazo kwamba tuendako ni bora kuliko hapa. Matokeo yake tunakuwa na matumaini zaidi. Tunakuwa wenye furaha.

Lakini ni bahati mbaya sana kwamba watu wengi hatuna furaha. Tunatafuta elimu tukidhani tunaweza kupata furaha lakini si hivyo inavyokuwa.(Inasemekana kwa kadiri unavyokuwa na elimu ndivyo unavyozidi kuziona kasoro katika maisha yanayokuzunguka na hivyo kukupungizia furaha)

Tunatafuta pesa, kwa matumaini hayo hayo, lakini hata tunapokuwa nazo bado hazitupi furaha. Tunapata mahusiano tunayodhani yanaweza kutuahidi furaha lakini sivyo inavyokuwa. Tunahama kutoka dini moja kwenda dini nyingine, lakini furaha yenyewe hatuipati. (Ukichunguza majina ya madhehebu yetu utaona namna ambavyo majina yao yamebuniwa kwa namna inavyoonyesha kwamba ukijiunga nayo basi kila kitu kitakuwa bara-bara) Tunasafiri kutoka mahali pamoja kwenda pengine, lakini hatupati furaha ya kweli. Tunakuwa maarufu mahali tunapoishi na hata ulimwengu mzima lakini sivyo inavyo kuwa.

Je, tufanyeje tuwe na furaha? Je, tumekosea wapi hata tusipate furaha tunayoitaka manake hata tukiipata inakuwa kwa kiwango cha chini kuliko matarajio halisi? Wapi lilipo tatizo? Siku njema.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?