Maisha hayawezekani bila wanasiasa?

Kama kuna 'kazi' ambazo zinanitatanisha ni zile zenye uhusiano wa moja kwa moja na kile kinachoitwa siasa. Kazi hizi zimepata umaarufu sana katika nchi za dunia ya tano ikiwamo Tanzania.

Kuna wanaoamini kuwa siasa ni porojo. Siasa ni usanii. Siasa ni uchezewaji wa wazi wa akili za watawaliwa. Udanganyifu. Utapeli wa wazi. Siasa. Sina hakika kama ninakubaliana na mawazo haya. Bado natafakari.

Kwamba siasa ina uhusiano na maendeleo yetu (hasa sisi wa dunia ya tano) hilo ni jambo la kufikirisha.

Siku hizi siasa imekuwa kama muziki wa Bongo Flava. Kila mtu anataka kujihusisha nayo. Wataalamu wa fani mbambali wenye ujuzi adhimu, wanazitosa ofisi zao na kukimbilia siasa. Tunawafahamu walimu wa Vyuo Vikuu ambao hata hawana haiba ya siasa, bado walidiriki kuzitosa ofisi zao. Kisa? Ulaji. Samahani siasa. Na idaidi yao haihesabiki.

Mtu unajiuliza mwananchi aliyesomeshwa kwa fedha ya walipa kodi fukara, na akawa mathalani daktari bingwa, ama mtaalam wa uchumi kwa mfano, anaachana na fani hizo na kujitokomea siasani. Kulikoni?

Kwa nini kila binadamu sasa hivi anaota kuwa mwanasiasa?

Umefika wakati wa kuhoji ni kwa kiasi gani hawa watu wanajielewa. Watu ambao wanazisaliti fani zao na kujiunga na kundi kubwa la wanasiasa.

Inakuwaje upoteze muda na fedha nyingi za walipa kodi kusomea kitu ambacho hutakifanyia kazi?

Halafu tujiulize, hivi bila hawa wanaoitwa wanasiasa maisha yangekuwaje? Bila Diwani. Bila Mbunge. Bila Mawaziri. Bila Raisi mwenyewe na kadhalika hivi tusingeishi?

Wanatusaidiaje hawa jamaa? Hivi ni kweli kwamba wao ndio hasa viongozi tunaowahitaji?

Angalia. Mbunge anachaguliwa. Anakuwa Mbunge. Jimboni haonekani. Maisha yake yote Dasalama. Familia yake iko huko huko Dasalam. Wapiga kura walie tu. Wakati mwenzao anabehua kwa shibe, wao wanakula miayo. Ajabu eti tunaambiwa kuwa ni wao eti ndio waajiri wake. Wanachoweza kufaidi ni kumsikia tu Bungeni (kwanza akiamua). Eti naye anadai kuwa anawawakilisha. Maswali yanayoulizwa yaleyale. Majibu yanayotolewa ni yale yale miaka nenda miaka rudi. Sina hakika kama kuna hata ufuatiliaji wa majibu yenyewe. Na ajabu hawa mabwana wanakaa wakila hela za mafukara kwa miezi wakijadili maamuzi ambayo tayari yanaeleweka!(Kama si kujadili maamuzi mbona sijawahi kusikia bajeti imekwama?)

Hao wakuu wengine wasiohudhuria bunge, tunaambiwa eti ni viongozi. Na ajabu viongozi wenyewe wanategemea ushauri wa watu wengine wa pembeni mwao ili mambo yaende. Kwa maana rahisi, hawa wanaoitwa viongozi, nao wanao viongozi wao! Kumbe? Sasa tunawahitaji wa nini hawa?

Hivi ingekuwaje bila wanasiasa? Watu ambao tunaambiwa wanachaguliwa kidemokrasia. Kenya na Zimbabwe wanatupa maana hasa ya hichi kinachonadiwa kwa jina la demokrasia. Ingekuwaje bila wanasiasa? Maana naona kama inatupotezea muda wetu bure!

Wakati wa kampeni wanasema watatupa maisha bora. Baada ya kampeni wanasema maisha bora mtajiletea wenyewe. Fanyeni kazi. Sijui kama utata huu nauona pekeyangu. Ingekuwaje bila siasa?

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mbinu za Kumfundisha Mtoto Kusoma Akiwa Nyumbani

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Fumbo mfumbie mwerevu

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)