Jinsi ya kumsikiliza mwenzio

Tulikwisha kuangalia kwa utangulizi umuhimu wa kusikiliza. Kwamba watu tunaozungumza nao wanaweza kuwa hawajui yale tunayoyajua ama hata kwa kiwango chetu. Lakini je, tunajua kila kitu? Jibu ni wazi kwamba si kweli. Wapo watu wengi wanaojua kuliko sisi katika maeneo kadha wa kadha. Watu hao hawana alama usoni inayowaonyesha weledi wao. Bahati mbaya ni kwamba wajuao huonekana kama vile hawajui. Kwa hivyo, kwa sababu hiyo ya kutoweza kumtambua ajuaye kwa kumwangalia tu, basi hiyo iwe ni sababu tosha ya kukushawishi kuwasikiliza watu wanaokuzunguka.

Tufanyeje kusikiliza kwa makini? Tutumie mbinu gani?

Hapa tutataja kadhaa, ambazo hata hivyo si msahafu. Tuzijadili kuona kama zaweza kufaa kutufanya kuwa wasikilizaji wazuri zaidi.

Mawasiliano ya kweli baina ya watu wawili yana hatua tatu:

1. Kusikiliza: Maana yake kufanya jitihada za dhati kujaribu kusikiliza kile hasa kinachosemwa na mwenzio.
2. Kuelewa: baada ya kufanya jitihada za kusikiliza kinachosemwa, sasa unajitahidi kupata maana hasa iliyolengwa. Unahama kutoka kusikiliza, mpaka kujaribu kumwelewa msemaji.
3. Kupima: Ukiisha kujiridhisha kuwa umemwelewa msemaji, sasa unafanya bidii ya kupima ulichoambiwa. Hapo unaangalia kama kilichosemwa kinaleta maana kwako bila kulazimika kumwonyesha msemaji kwamba sasa unapima maneno yake.

Jinsi ya kusikiliza vyema:
1. Jitahidi kumakinika kwa msemaji. Onyesha kwa uso, mwili na mkao wako kuwa unamsikiliza anayesema. Ni wazi kuwa mtu anyeangalia wapita njia wakati anajua yupo anayesema naye, hana sifa ya usikilizaji mzuri.
2. Hakikisha kuwa akili yako yote iko katika kile kinachosemwa. Usiache akili yako ikawa inapita pita kwingine wakati kuna binadamu anasema na wewe. Hiyo si haki.
3. Usiingilie sentensi zake wakati anasema. Wengine wanasema kumkata kauli. Mwache aseme anachosema kwa uhuru. Subiri amalize ndipo uulize kama kuna sehemu ya kuuliza. Ni wazi mtu anaposema hufurahi sana anapoona kwamba amepata nafasi ya kusema kwa ukamilifu kile anachotaka kukisema. Kuingilia maana yake ni kuonyesha kwamba kusikilizi ila unatafuta kukosoa, ama unajifanya mjuaji.
4. Hakikisha unamaliza kusikiliza kabla hujaanza kusema! Huwezi hata siku moja kusikiliza kama mwenzetu unafikiria tu cha kusema wakati kuna mtu anasema tayari.
5. Sikiliza mawazo makuu yanayojitokeza katika maongezi. Haya ni mawazo ambayo yanaonekana kuwa ndiyo lengo hasa la msemaji. Huweza kusemwa mwanzoni kabisa mwa mazungumzo ama mwishoni ama hata kurudiwa rudiwa. Fungua masikio yako yote jamaa anapotumia maneno kama “Ninachotaka kusema ni kwamba…” au “ Kumbuka bwana…” ama “Cha muhimu ni…”
6. Uliza usikoelewa. Kama huna hakika kwamba umeelewa kilichosemwa, uliza. Unaweza kurudia kilichosemwa na mzungumzaji wako kwa maneno yako mwenyewe ili kuhakiki kwamba si tu ulisikiliza kwa makini bali pia ulielewa. Kwa mfano “ Kwa hiyo umesema kwamba …..” Kama umekosea atakurekebisha.
7. Toa mrejesho. Kaa mkao wa kuchangamka na mwangalie msemaji machoni. Tingisha kichwa hapa na pale kuonyesha kwamba unaelewa. Tabasamu panapostahili, cheka ikibidi ama tulia kufuatana na mtiririko wa msemaji. Hayo yote ni kuonyesha kwamba unamsikiliza na kumwelewa. Itasikitisha kama msemaji anakusimulia jambo la huzuni halafu mwenzetu unabaki kutabasamu.

Kumbuka, mawazo kuzunguka mara karibu nne kuliko maneno yanayosemwa mdomoni. Kwa kujizoeza, hali ukisikiliza, basi utaweza kufikiri zaidi kile unachokisikia, na kukielewa na hivyo kuonyesha wazi kwa msemaji kwamba unakifuatilia kwa kutoa mrejesho unaofaa.

Maoni

  1. Bro Bwaya huko juu ile mbaya,nikweli kwamba wapo watu wengi ambao wanakuwa na matatizo kama hayo ya kuwasikiliza watu na kuwaelewa,mimi binafsi nilikuwa najiuliza sana kuhusiana na suala hlo,juzi kati nilikuwa na chat na washkaji flani hv wa kenya,wakawa wanadai eti sisi ni watanzania ni wagumu kuelewa,nikagundua kuwa kuwa,kuna mtu anakuwa muelewa kwenye baadhi ya maongezi,kwahyo unapaswa kuwa makini unapokuwa unawasiliana na mtu.kwangu maoni ni hayo tu.

    JibuFuta
  2. Shayo Karibu sana katika kibaraza hiki. Asante kwa maoni mazuri. Ni kweli kwamba kusikiliza na kuelewa, kama ulivyotoa mifano, ni kazi ngumu. Karibu tena na tena.

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?