Namna Michezo Inavyomsaidia Mtoto Kujifunza

Wazazi wengi wanaichukulia michezo ya watoto kama shughuli isiyo na maana. Kimsingi, ipo imani inajengeka kuwa kucheza ni kupoteza muda. Matokeo yake wazazi hujitahidi kuwazuia watoto wasicheze kwa matumaini ya kuwasaidia wapate muda wa kufanya mambo ya maana zaidi kama vile kusoma na kukamilisha kazi za shule.

Pamoja na umuhimu wa kufanya hivyo, hata hivyo, michezo  inabaki kuwa shughuli yenye umuhimu mkubwa katika ukuaji wa jumla wa mtoto kimaarifa, kimahusiano, kimwili na kihisia.

Katika mipaka ya makala haya, michezo tunaweza kusema ni shughuli zisizo rasmi anazozifanya mtoto kwa lengo la kufurahi na kuburudika. Mfano wa shughuli hizi ni kubembea, kuteleza, kuogelea, kuendesha baiskeli, kucheza mdako, ‘rede’, mpira, kukimbia, kuruka na kuvuta kamba, nyimbo, maigizo na kadhalika.

Tutazame maeneo matano muhimu yanayoonesha namna michezo inavyoweza kumsaidia mtoto kujifunza.

Kupanua ufahamu wa mtoto

Kukua kwa akili ya mtoto kunategemea kwa kiasi kikubwa namna anavyoweza kucheza. Kwa kawaida, utimamu wa akili ya mtoto mara tu anapozaliwa hupimwa kwa kiwango chake cha kushughulisha viungo vya mwili wake.

Kupitia michezo, mtoto hutumia akili kujifunza namna ya kutatua changamoto zinazomkabili. Kwa mfano, anapojifunza kuruka kamba, inabidi aelewe namna kutua kwa miguu yake kunavyotakiwa kupishana na kamba inayopita chini. Zoezi kama hili mbali ya kumsaidia kuchangamsha viungo vyake, pia linamkuza kiufahamu.

Kadhalika, kwa kucheza, mtoto hujifunza dhana mbalimbali zinazoweza kumsaidia kuyaelewa mazingira yake. Kwa mfano, anapocheza mdako na wenzake, anajifunza kuhesabu, kukadiria umbali na muda, kupanga mbinu za kushinda na kadhalika. Haya yote yanakuza ufahamu wake.

Huimarisha mwili wa mtoto

Kucheza kunamhitaji mtoto atumie viungo vya mwili. Ili acheze ‘rede’ kwa mfano, ni lazima aruke, akimbie kukwepa au kuufuata mpira, lazima atumie mikono yake kujaza mchanga kwenye chupa na vitendo vingine vinavyofanyika kwa haraka, ambavyo kwa kweli ni kufanya mazoezi ya mwili.

Tafiti nyingi zimeonesha namna kutokucheza kunakokwenda sambamba na utazamaji wa televisheni  kunavyoweza, kwa kiasi kikubwa, kuchangia kuongeza tatizo la uzito mkubwa wa mwili kwa watoto. Kucheza ni hatua ya kukabiliana na tatizo hili na kunasaidia kupunguza uwezekano wa magonjwa yanayosababishwa na kukosa mazoezi. Ili iwe na msaada, hata hivyo, michezo hiyo ni muhimu ihusishe kwa kiasi kikubwa viungo vya mwili.

Hukuza uwezo wa kuwasiliana

Michezo ni mawasiliano. Ili waweze kucheza vizuri, watoto hulazimika kujadiliana mambo ya msingi kama aina ya mchezo utakaochezwa, jukumu la kila mmoja, kanuni zitakazoongoza mchezo na kadhalika.

Aidha, ni kawaida watoto kupenda kuimba, kueleweshana, kuhojiana na hata kujieleza pale kanuni zilizowekwa zinapovunjwa na mmoja wao. Haya yote huwasaidia kujifunza wenzao wanavyoongea, wanavyotumia maneno, wanavyojieleza pale wanapokosea na hivyo kukuza uwezo wao wa kuelewa kanuni za lugha.

Hujenga urafiki na wenzake

Kucheza hujenga uwezo wa watoto kushirikiana, kufanya kazi pamoja, kufanya maamuzi yanayokubalika na pande zote, kutatua migogoro, na wakati mwingine kujifunza kukosa kile wanachokitamani. Haya ni maeneo muhimu yanayokuza uwezo wa kujenga maelewano.

Kwa kawaida, si kila kanuni inayoongoza mchezo hukubaliwa na watoto wote. Mazingira hayo si tu huhitaji uwezo wa kushawishi wengine lakini pia huwa ni fursa ya kumfundisha mtoto kujifunza kuyaona mambo kwa macho ya wengine.

Ili kukuza uwezo huu, inashauriwa wazazi wawaruhusu watoto kucheza wenyewe bila kuwaingilia. Wanaporatibu michezo yao wenyewe wanapata fursa ya kufanya maamuzi yao, kwa uhuru, na hivyo kujua kitu gani kinawaunganisha pamoja, na malengo yapi wanaweza kuyafikia kwa pamoja kama marafiki wanaoelewana.

Huimarisha uhusiano na mzazi

Unapokuwa tayari kushiriki michezo inayoongozwa na mwanao unamfanya aamini unajali na kuheshimu mambo yake na hivyo atajisikia kuhamasika zaidi kuwa karibu na wewe.

Fikiria mwanao anataka mcheze mchezo wa kujificha na kutafutana. Kwako uliye mtu mzima, kukimbizana na mtoto kwaweza kusiwe shughuli yenye maana yoyote. Lakini kwake, hiyo ndiyo lugha anayoielewa vizuri zaidi. Unapokubali kutumia muda wako kucheza naye, anakuheshimu kwa kujua umefanya hivyo kwa ajili yake.
Uhusiano wa karibu wa mama na mwanae. Picha: Christine Missanga 

Kadhalika, unapocheza na mwanao, unajifunza namna nzuri ya kuwasiliana naye. Katika kucheza si rahisi, kwa mfano, ujikute unatoa maagizo na amri zenye kuonesha mamlaka. Badala yake utalazimika kujua kusema nae kwa lugha ya kirafiki hali ambayo hujenga mahusiano ya karibu na mwanao.

Unavyoweza kumsaidia

Hakikisha mtoto anakuwa salama pale anapocheza. Weka mazingira rafiki nyumbani ili aweze kucheza bila kuhatarisha usalama wake. Kwa mfano, waweza kuondoa vifaa vyenye ncha kali, vinavyovunjika kirahisi, vinavyoweza kumwangusha ili kupunguza hatari ya mtoto kuumia anapocheza.

Kadhalika, ni vizuri kumpangia mtoto muda maalum wa kucheza. Katika umri wa kati ya mwaka mmoja na sita, michezo ni hitaji la msingi sana kwa mtoto. Mruhusu afurahie michezo. 

Hata hivyo, ni vizuri kudhibiti michezo inayomfanya mtoto ajenge utegemezi wa kitabia, inayomfundisha ubabe, ugomvi, ukatili kwa mwamvuli wa kumfurahisha. Hapa kuna michezo ya kidijitali inayopatikana kwenye simu, televisheni, kompyuta na vifaa vingine vya kiteknolojia. Pamoja na uzuri wa michezo hii, kwa kweli, haisaidii sana kumjenga mtoto kiakili, kitabia na kimwili.

Ni muhimu kuchukua tahadhari unapocheza michezo yenye ushindani na mtoto. Mpe nafasi ya kushinda kadri inavyowezekana ili kukuza kujiamini kwake. Si muhimu, kwa mfano, unapocheza na mwanao mpira au mchezo wa bao umfunge kila mara. Hata hivyo, waweza pia kumfundisha kushindwa bila kuathiri mtazamo wake pale inapobidi.

Soma Jarida la Maarifa la gazeti la Mwananchi kila Jumanne kwa makala kama hizi. 

Maoni

 1. Ni Elimu nzuri sana lakini inasikitisha sana miaka hii wazazi/walezi wengi wanatumia vitu kama televiheni na hizi simu kama ndio vitu vya watoto kuchezea badala ya kucheza nao. Na hii inasababisha watoto wengi kuwa wazembe na pia kuongezs uzito kwa kuwa muda mwingi huwa wanakaa tu...

  JibuFuta
 2. Ni Elimu nzuri sana lakini inasikitisha sana miaka hii wazazi/walezi wengi wanatumia vitu kama televiheni na hizi simu kama ndio vitu vya watoto kuchezea badala ya kucheza nao. Na hii inasababisha watoto wengi kuwa wazembe na pia kuongezs uzito kwa kuwa muda mwingi huwa wanakaa tu...

  JibuFuta
 3. Ni sahihi kabisa Yasinta. Wakati mwingine tunawapa hivyo vitu kwa sababu hatuna muda wa kutimiza wajibu wetu. Tubadilike.

  JibuFuta
 4. Kibaya zaidi ni kuwa, tuna muda mwingi sana wa kucheza na simu kuliko kucheza na watoto. Pengine kuna wakati watoto wanatamani wangekuwa simu janja kwa nmna zinavyopendwa kuliko watoto wanavyopendwa. Au kutembelea mitandaobya kijamii mara nyingi inavyowezekana kuliko kufuatilia maendeleo ya mtoto.

  Inaweza kuwa rahisi sana kwa mzazi kutokukosa hela ya kununua inteneti lakini akakosa hela ya kutimiza mahitahi ya kawaida ya mtoto. Mambo haya ni ya kawaida sana kwenye wakati huu wa mahaba na simu janja.

  Tubadilike!

  JibuFuta
 5. Pia, kuna haja ya kuwa makini pale watoto wanapocheza wenyewe. Dunia imebadilika sana na kila siku kuna mambo ya kushangaza kweli kweli.

  Uhuru wa habari, simu janja na kukosekana kwa wajibu wa dhati wa wazazi kwa watoto,kumewafanya watoto wajifunze ama walazimike kujiingiza kwenye tabia ovu kabisa.

  Watoto wanapocheza wenyewe wanaweza kuwa na hatari ya kuambukizana tabia na maadili mabaya. Wazazi hawana budi kuzingatia hili pia. Pengine kuna haja ya kujifunza aina ya marafiki wanaocheza na watoto. Vinginevyo, hasara ya michezo ya watoto inaweza kuwa kubwa kuliko faida.

  Katika muktadha huu, pengine wazazi tujitafakari kuhusu muda sahihi wa kuwa mbali na watoto hususani pale tunapoamua kuwapeleka shule za kulala.  JibuFuta
 6. Uko sahihi kabisa Bw. Albert. Tahadhari uliyoitoa ni ya msingi.

  JibuFuta
 7. Uko sahihi kabisa Bw. Albert. Tahadhari uliyoitoa ni ya msingi.

  JibuFuta
 8. Uko sahihi kabisa Bw. Albert. Tahadhari uliyoitoa ni ya msingi.

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Fumbo mfumbie mwerevu

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging