Unatafuta Kazi? Sifa Sita Unazozihitaji

Katika makala yaliyopita tuliona takwimu zinazothibitisha kuwa tatizo la ajira ni zaidi ya kukosekana kwa nafasi za kazi. Ingawa watafuta kazi wengi hufanya juhudi za kuthibitisha kuwa wanao ujuzi rasmi waliousomea darasani, si waajiri wengi wanathamini alama za darasani zinazoonekana kwenye vyeti vya waombaji hao.
Badala yake, mwajiri kwa kawaida hutafuta ujuzi ambao mara nyingi mtafuta kazi hautegemei. Ujuzi huo, tulioupachika jina la ‘ujuzi mwepesi’, ni pamoja na ule uwezo wa kutumia maarifa ya jumla ya darasani katika kufumbua matatizo halisi yanayomkabili mwajiri katika eneo lake la kazi.

Kwamba waajiri wanatafuta ujuzi ambao si mara nyingi hupatikana darasani, ndio sababu matangazo mengi ya nafasi za kazi hayaweki msisitizo mkubwa katika sifa za kitaaluma anazohitajika kuwa nazo mwomba kazi bali ‘ujuzi mwepesi’ tutakaoujadili katika makala haya. 
Je, mwajiri hutarajia ujuzi gani kwa mwombaji wa kazi? Tutazame mifano michache.
Ubunifu
Mwajiri mzuri anategemea kuona namna gani mwajiriwa anaweza kufikiri nje ya mazoea. Huu ni uwezo wa kufikiria majibu yasiyozoeleka ya changamoto zilizozopo ili kuongeza ufanisi wa kazi. Ubunifu ni pamoja na namna mwajiriwa anavyoweza kutumia raslimali chache zizizopo kuleta matokeo yanayozidi matarajio.
Kwa mfano, unapoweza kutumia Tsh 100 kuleta matokeo yale yale ambayo yangeweza kuletwa kwa kutumia Tsh 1,000, hapo unakuwa umelazimika kufikiri nje ya sanduku la mazoea. Kwa kuweza kutumia raslimali kidogo kuleta matokeo makubwa unakuwa umemnufaisha mwajiri wako, jambo ambalo kwa hakika ni kipaumbele kikuu cha waajiri wengi.

Uongozi
Uongozi ni uwezo wa kuwaonyesha njia na kuwahamasisha wengine kufikia malengo mapana ya mwajiri. Kuwa kiongozi maana yake unaweza kujisimamia mwenyewe na kuwasaidia wengine pia kuelekea kule kunakotarajiwa na mwajiri.
Uongozi si sawa na madaraka. Hizi ni dhana mbili tofauti lakini zenye uhusiano wa karibu. Waweza kuwa na madaraka rasmi kazini lakini katika utendaji usiwe na chembechembe zozote za kiongozi.
Uongozi ni uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kwa ushirikiano na wengine pasipo kusimamiwa kwa karibu na wakubwa wenye madaraka ya kikazi. Uongozi ni pamoja na namna unavyoweza kufanya majukumu mengine kwa moyo wa hiari na kujituma ili kufikia malengo mapana ya mwajiri. Huhitaji kukasimiwa urasimu wa madaraka  kuweza kutekeleza hilo.
Mahusiano bora na wengine

Kwa kawaida, kazi nyingi zenye kuleta tija zinahitaji ushirikano wa karibu wa watu mbalimbali. Ili kuleta ufanisi, kunahitaji uhusiano mzuri wa kikazi baina ya mwajiriwa na watu wengine. Bila mahusiano mazuri na wengine, pengine kwa sababu ya ile hulka ya kupenda kuwazidi wengine, ufanisi wa pamoja wa kazi husika unaweza kuwa mashakani.

Namna gani mwajiriwa anaweza kusaidiana na wengine kufanikisha malengo ya mwajiri pasipo ushindani usio na tija, hayo ndiyo mahusiano ya kikazi.

Mawasiliano

Hakuna mahusiano na wengine pasipo mawasiliano. Mambo mengi katika kazi yanalazimu wafanyakazi  kufanya mawasiliano yasiyo rasmi kwa kutumia maandishi au mazungumzo yam domo. Mfano kuna nyakati mwajiriwa atalazimika kuwasilisha taarifa au maoni yake kwa wakubwa wake wa kazi. Kadhalika, atalazimika kuwasiliana na wale anaofanya nao kazi. Hapa ndipo uwezo mzuri wa kuwasiliana unapohitajika.

Ingawa matumizi ya lugha yanatofautiana baina ya mazingira ya kazi, bado ni wazi katika mazingira mengi ya kikazi tunalazimika kuelewa namna nzuri ya kuwasiliana na watu. Uwezo wa lugha una nafasi kubwa katika kazi.

Nidhamu ya kazi

Ufanisi katika kazi, kwa kiasi kikubwa, unategemea nidhamu. Namna gani mwajiriwa anaheshimu kazi yake kwa kuwahi kazini, kuwasilisha mrejesho wa kikazi kwa muda hiyo ndiyo inaitwa nidhamu ya kazi.

Kadhalika, nidhamu ya kazi ni pamoja mpangilio mzuri wa jumla wa majukumu ya kila siku unaotanguliwa na utunzaji wa muda. Mwajiri mzuri hatarajii mtu anayeweza kufanya kazi kizembe bila kufuata taratibu za kikazi zilizowekwa.

Uzoefu


Namna gani mwajiriwa anaonesha ushahidi kwamba anao uwezo wa kufanya kazi inayokusudiwa, huo ndio uzoefu. Mwajiri yeyote makini angependa kuona uthibitisho dhahiri kwamba mwombaji wa kazi au mwajiriwa anao uwezo wa kumudu majukumu anayoyaomba kwake au yale aliyoyakabidhiwa.

Uzoefu huu unaweza kupatikana kupita kazi ulizopata kuzifanya kabla ya ajira husika iwe kwa ajira rasmi au kwa kujitolea. Kwa mtafuta kazi asiye na historia ya kuajiriwa, anahitajika kujifunza kutafuta fursa za kujitolea kufanya kazi zinazofanana na ajira anayoitamani wakati akiendelea na masomo au katika kipindi cha mpito anaposubiri kuajiriwa.


Tunavyoweza kuyaonesha haya

Ingawa ni kweli kuwa nchi yetu inakabiliwa na ukosefu wa ajira, bado ni wazi waajiriwa wengi hawaajiriki kwa maana ya kukosa weledi na ujuzi unaowawezesha kuajiriwa na kudumu katika ajira zao. Ujuzi huu, kama tulivyoona, si mara zote unaweza kupatikana kupitia mfumo wa mitihani na vyeti. Ni muhimu kufanya jitihada za makusudi kujinoa kwa lengo la kujiongeza kiujuzi.

Katika kufanya maombi ya kazi na hata pale tunapotekeleza majukumu yetu kazini tunawajibika kuthibitisha kuwa ni kweli tunao ujuzi huu mwepesi. Katika makala zijazo, tutazungumzia kile 
kinachoweza kufanyika katika kuwasaidia watafuta kazi kujiongezea ujuzi huu tulioupitia hapa kwa haraka na, kadhalika, namna ya kuandika barua na maelezo binafsi (wasifu)
yanayoonyesha haya tuliyoyajadili kwa kifupi.

Fuatilia Jarida la Ajira na Kazi ndani ya gazeti la Mwananchi kila Ijumaa kwa makala kama hizi. 

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia