Kanuni za Kuongeza Ushawishi wa Hoja Zako

Kwa nyakati tofauti kila mmoja wetu hutamani kuwa na ushawishi kwa wengine. Ni kawaida, kwa mfano, kutamani hoja tunazozitoa zipokelewe na wale tunaowatumia ujumbe husika. Ili ujumbe upokelewe, inahitajika nguvu inayoweza kuwasukuma wengine kuupenda, kuubali na ikiwezekana kubadilika kwa sababu ya ujumbe husika. Nguvu hii inaitwa ushawishi.

Kwa hakika ushawishi ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Viongozi, kwa mfano, wanatamani kuwa na ushawishi kwa wafuasi wao. Mzazi, kama kiongozi wa familia, angependa kuwa na ushawishi kwa mwanae. Kwa ujumla,urafiki, siasa, mahusiano ya jamii, kazi na maeneo mengine mengi yanadai ushawishi.

Ikiwa unatamani kuwa na ushawishi, makala haya yanaangazia kanuni kadhaa za kuwasilisha ujumbe wako ili kuoongeza uwezekano wa wengine kukubaliana nao.

Ushawishi unachukua sehemu kubwa mahusiano yetu. Picha: Joan Cassidy


Jenga uhalali wako

Ni vizuri kutambua kuwa wewe kama msemaji wa ujumbe unayo nafasi kubwa sana ya ushawishi pengine kuliko ujumbe wenyewe. Wasikilizaji wako hawawezi kuzingatia ujumbe kama hawajakuchukulia kwa uzito wewe uliye na ujumbe. Hivyo, kabla hujatumia nguvu nyingi kwenye ujumbe unalazimika kujenga uhalali wako.

Kujenga uhalali ni kuwaaminisha wale wanaokusikiliza kuwa unaelewa kile unachokisema na hubabaishi. Ni hivyo kwa sababu, kwa kawaida, watu huheshimu weledi. Kama unazungumzia mambo ya uchumi, kwa mfano, watu wangependa kujiridhisha kuwa unaufahamu uchumi vilivyo na hivyo unalazimika kuwahakikishia kuwa unao utaalamu wa kina kwa kile unachokizungumza.

Tutumie mfano wa ujumbe wenye mrengo wa kisiasa au kidini (ambavyo kwa kawaida vina kawaida ya kugusa hisia za wanaokusikiliza kwa kiasi kikubwa). Katika kujenga uhalali wako kama mwenye ujumbe, ni muhimu kujitambulisha kama mchambuzi wa masuala ya kisiasa au kiimani. Utambulisho wa namna hiyo huongeza imani ya wanaokusikiliza kuliko unapojitambulisha kama mwananchi wa kawaida.

Lakini pia waweza kuonesha waziwazi msimamo wako wa kisiasa au kidini kwa wanaokusikiliza lakini kwa kuthibitisha pasipo shaka kuwa unao uelewa wa kina wa kile unachokisema. Wata hawatashindwa kukusikiliza kwa sababu tu wamejua unasimamia upande upi. Muhimu ni weledi na kuonesha ujuzi wa kile unachojitambulisha nacho.

Kingine katika kujenga uhalali ni kuwaondolea wasikilizaji wako mashaka ya mgongano wa maslahi na kile unachokisema. Ni vigumu, kwa mfano, mtu anayefahamika kuwa mpiga debe wa bidhaa fulani kuchukuliwa kwa uzito unaostahili ikiwa atabainisha ‘anawamba ngoma’.

Turudie mfano wa awali wa ujumbe wenye mrengo wa kisiasa au kidini. Kuondoa hisia za mgongano wa maslahi, waweza kuchagua kufanya jitihada za kujitenga na upande wowote. Ukifanya hivi unatuma ujumbe kwa wanaokusikiliza kuwa huna maslahi na hivyo unachokisema ni kweli. Kuaminika kunaongeza ushawishi wako kuliko pale unapofahamika kama mtu anayesimamia ilani/misimamo ya upande fulani.


Jambo la tatu linaloongeza ushawishi wako ni mwonekano unaokubalika na wasikilizaji. Namna unavyoonekana  kwa watu hukupa nafasi kubwa ya kiushawishi ikiwa utakidhi matarajio ya wanaokusikiliza. Kwa mfano, ikiwa wasikilizaji wako wanatarajia uonekane katika mavazi fulani, litakuwa ni kosa kubwa kuonekana tofauti. Mavazi unayovaa, lugha unayotumia, namna unavyoongea, matumizi ya lugha ya ishara, vyote hivi kwa pamoja vinabeba ujumbe mzito kuliko hata ujumbe wenyewe.

Unavyouweka ujumbe wako

Tafiti zinaonesha kuwa hata wasikilizaji wasioelewa kile unachokisema wanazo mbinu za kuamua ujumbe gani wanaweza kuuchukua na upi wakuachie wewe msemaji. Moja wapo ya mbinu hizo ni kujiridhisha kuwa ujumbe husika haulengi kuwadhalilisha na kuwabadilisha. 

Upo ukweli kuwa binadamu hatufurahii pale tunapogundua kuna mtu anafanya bidii ya kutaka kutubadilisha. Hatupendi kubadilishwa kwa sababu kulinda hadhi zetu. Kwa kulitambua hilo, unahitaji kuwaheshimu wasikilizaji wako kwa kutokuonesha wazi wazi nia ya kuwabadilisha watu  vinginevyo, wataupuuza mapema kabisa.

Sambamba na kuwaheshimu wasikilizaji wako, ni vyema kuwa na ujumbe ulio dhahiri unaojenga matarajio chanya ili kuongeza hamasa ya kupokelewa na kufanyiwa kazi. Ni vyema kutambua kuwa ujumbe hasi unaojenga hofu na kukatisha tamaa haupewi nafasi kuliko ujumbe unaotia moyo. 

Ingawa ni kweli kuwa ujumbe hasi hugusa hisia za watu kirahisi sana, si mara zote hofu huambatana na utendaji kwa sababu watu wana kawaida ya kuvutiwa na kuufanyia kazi ujumbe unaojenga taswira chanya ya kile kinachowezekana na kamwe sio kile kisichowezekana.

Nimefanya utafiti mdogo wa kulithibitisha hili kupitia blogu yangu. Wakati mwingine niliandika ujumbe kwa lugha inayojenga hatia zaidi kwa msomaji, na mara nyingine nimeandika ujumbe unaojenga matumaini. Mara zote, nimeona, makala zenye ujumbe wa matumaini na kuonesha inavyowezekana zimekuwa zikisomwa mara dufu ya zile zenye kujenga taswira ya hatia. 

Maana yake ni kuwa watu wana kawaida ya kupenda kusikia matumaini kuliko kunyong'onyezwa. Ndio maana kampeni za elimu dhidi ya VVU/UKIMWI zilizojikita katika kujenga hofu huwa hazifanikiwi mara hofu hiyo inapoondoka kwa watu. Ndio kusema, ujumbe unaojenga uwezo kwa wananchi kujiamini dhidi ya ngono zembe na faida zake unaweza kuleta matokeo mazuri kuliko kusisitiza hofu dhidi ya VVU/UKIMWI.

Vile vile, ni muhimu kuelewa watu hawana tabia ya kupenda hoja zinazohitaji nguvu nyingi kuzielewa na zisizokidhi mahitaji yao halisi. Hoja ngumu inayoonesha tofauti kubwa ya kimtazamo na kiuelewa kati yako na wasikilizaji, hujenga upinzani wa kimya kimya na juhudi za maksudi za kutotaka kuielewa. 

Ikiwa lengo ni kujenga ushawishi kwa wanaokusikiliza, ni muhimu kufanya jitihada za kurahisisha hoja zako na kuzioanisha na mahitaji halisi ya wasikilizaji. Kwa kufanya hivyo, unawavutia wasikilizaji kula kile wanachojua wanakihitaji kwa sababu, kwa vile kinavyoonekana, kinafanana nao.

Itaendelea wiki ijayo

Maoni

 1. PROMO DELIMA
  poker online terpercaya | poker online | Agen Domino | Agen Poker | Kumpulan Poker | bandar poker | Judi Poker | Judi online terpercaya | bandar qiu | situs judi online

  Ayo segera daftarkan diri anda dan bergabunglah bersama kami !!
  Delimapoker.com Situs Agen Poker Online Terpercaya di Indonesia akan melayani Anda dengan profesional, memproses depo/wd dgn cepat. Come join and be a winer with us !!

  Untuk info selanjutnya silakan chat ke :
  Livechat_____: delimapoker
  BBM__________: 7B960959
  Facebook_____: delimapoker
  Phone number_: +85595678845
  pendaftaran___

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3