Wajibu wa Mzazi Kama Mwalimu wa Kwanza wa Mtoto

Tafiti nyingi za mazingira ya kujifunzia zimeendelea kusisitiza kuwa elimu bora kwa mtoto huanzia nyumbani. Kuwepo kwa mazingira rafiki ya kielimu nyumbani kunampa mtoto nafasi ya  kukua kiufahamu na humuandaa vyema kujifunza kabla hajaanza shule rasmi.

Kimsingi, mzazi ndiye mwalimu wa kwanza anayemwezesha mtoto kujifunza vizuri. Mtoto hujifunza kutembea, kuongea, kujilisha, kazi za nyumbani na kadhalika kwa msaada wa mzazi. Ikiwa mzazi atatambua wajibu wake kama mwalimu wa mtoto na akautekeleza ipasavyo, kazi ya mwalimu shuleni hurahisishwa.


Tutazame maeneo manne muhimu yanayoweza kukusaidia wewe kama mzazi kutekeleza wajibu wako kama mwalimu wa mwanao katika mazingira ya hapo hapo nyumbani.

Mfatufie vifaa vya kujifunzia

Mtoto anahitaji kuchangamshwa kiakili, kimwili, kihisia na kimahusiano tangu anapozaliwa. Anapochangamshwa mapema, ufahamu wake hujiweka tayari kujifunza hata kabla hajakutana na mwalimu wake shuleni.

Ili aweze kuchangamshwa ipasavyo, anahitaji vifaa muhimu vya kujifunzia. Kwa mfano, unaweza kuhakikisha mtoto anapata rangi na penseli za kuchorea, makaratasi na madaftari ya kuandikia, CD/DVD za katuni na hadithi mbalimbali, majarida na vitabu vya watoto, kamba za kuruka, vizibo/vifaa vya kuhesabia pamoja na vifaa vingine anavyoweza kuvitumia kuifanya akili yake ijifunze ubunifu.

Wazazi wengi, hasa wa mijini, hutumia fedha nyingi kuwanunulia watoto vifaa vilivyotengenezwa tayari kama ‘magari’, mipira, ‘ndege’, ‘simu’, ‘samani za nyumba’ na kadhalika. Hata hivyo, vifaa hivi vina hatari ya kumnyima mtoto fursa ya kukuza ubunifu na kupata ujuzi wa kutengeneza vitu vinavyoendana na mahitaji yake.

Mletee malighafi rahisi kama maboksi, mkasi na gundi yatakayomsaidia kutengeneza vitu halisi anavyovihitaji. Kwa kufanya hivi, mtoto hukuza uwezo wa kufikiri na kuhalisisha kile anachokifikiri.
Mtoto akijifunza kuandika. Picha @Jielewe

Mjengee hamasa ya kujielimisha

Hamasa ni nguvu inayomsukuma mtu kuwa tayari kuweka juhudi katika kutimiza malengo aliyojipangia. Mzazi, kama mwalimu wa kwanza wa mtoto, unao wajibu wa kumjengea mwanao hamasa kubwa ya kutaka kujifunza.

Kwa mfano, ili kukuza hamasa yake, waweza kumjenga kisaikolojia aweze kuamini kuwa anao uwezo na anaweza. Imani kuwa anaweza ni muhimu sana na itakuwa nguzo yake anapojifunza.

Waweza pia kumpa mifano ya namna elimu na maarifa vinavyoweza kumsaidia mtu kutatua matatizo yanayomkabili. Mwonesha fursa zilizoko mbele yake kwa kuzihusianisha na mafanikio yake darasani. Mpe mifano ya wanasayansi maarufu waliogundua mambo makubwa yaliyobadili maisha ya watu.

Msimulie habari za wanasheria maarufu watetezi wa haki za watu wanyonge, madaktari wanaookoa maisha ya watu, walimu, wabunifu wa majengo maarufu, mainjinia wa barabara, waandishi wa habari na kada nyinginezo. Masimulizi haya hujenga hamasa kubwa inayomwongezea mtoto shauku ya kuelimika.

Wakati mwingine masimulizi yanayotanguliza fedha dhidi ya maarifa yanawakatisha tamaa watoto kujibidiisha kielimu. Ikiwa unataka mwanao apende elimu mwoneshe vile elimu hiyo ilivyo muhimu pengine kuliko pesa.

Fuatilia maendeleo yake

Mtoto anahitaji kile anachokifanya kitambuliwe na kimfurahishe mzazi wake. Anapojua kuwa unafuatilia mafanikio yake, atajitahidi kujibidiisha zaidi ili aendelee kujiletea sifa. Mpe fursa ya kujisikia fahari kwa kutambua jitihada anazofanya katika masomo.

Fanya mawasiliano na walimu wake shuleni kujua anaendeleaje. Anapogundua unafuatilia yanayoendelea shuleni kwake, atajua unamthamini na atahamasika kufanya utambue anavyoweza.

Ni kweli wakati mwingine waweza kukutana na taarifa usizozipenda shuleni. Labda kiwango chake cha kufaulu hakifanani na matarajio yako. Hakuna sababu ya kumkatia tamaa. Badala ya kumsimanga na kumwonesha namna alivyo ‘kilaza’, onesha imani kubwa uliyo nayo kwake. Mhakikishie unajua anavyoweza kufanya vizuri zaidi.

Kadhalika, tambua maeneo mahususi aliyoonesha uwezo wake na ikiwezekana shiriki shughuli zake nyingine anazozipenda. Anapoona unathamini mambo anayoyapenda hata kama si ya kitaaluma, hatakuwa tayari kukuangusha kwa mambo anayojua unayatarajia kwake ikiwemo taaluma. 

Wakati mwingine watoto hushindwa kufanya vizuri kwa sababu hatuwapi msaada wanaouhitaji. Jenga utaratibu wa kumsaidia kitaaluma. Kaa nae jioni, uliza amepewa kazi gani ya kufanya nyumbani. Mpe msaada lakini usimlemaze akawa tegemezi. Kwa kufanya hivyo, utamfanya awe na shauku kubwa ya kukuthibitishia alivyo na uwezo.

Mzoeze kufuata ratiba ya siku

Familia nyingi hazina mazingira yanayomwezesha mtoto kujifunza kwa utulivu. Mfano ni pale watu wazima wanaoishi na mtoto wanapotumia muda mwingi kutazama televisheni na kusikiliza redio kwa namna inayowazuia watoto kufanya kitu kingine tofauti.

Katika mazingira mengine, watoto hupotelea kwenye michezo mingi isiyodhibitiwa huko mitaani tena bila uangalizi wa wazazi. Mambo haya hayawezi kumsaidia mtoto kujifunza. Hakikisha mazingira ya nyumbani kwako yanampa mtoto fursa ya kujisomea bila usumbufu.

Vile vile, msaidie kupangilia mambo yake kulingana na umri. Utamaduni wa ratiba unajengwa. Anaporudi kutoka shuleni,  kwa mfano, ajue atacheza kwa muda gani, ataoga saa ngapi, wakati upi atafanya kazi za nyumbani, kufanya ibada ya pamoja, kusimuliwa hadithi ya kitandani na kulala.

Sambamba na ratiba isiyobadilika badilika, fanya juhudi za kumpunguzia majukumu mengine yanayoweza kuwa kikwazo cha kujifunza. Ingawa kushiriki kazi za mikono ni muhimu  sana kwa ukuaji wa mtoto, jitahidi kutambua ni wakati gani kazi hizi zaweza kuwa kikwazo.


Msingi wa elimu bora hauanzii shuleni na mtoto hawezi kupenda shule hivi hivi bila juhudi zako mzazi. Ukitimiza wajibu wako, utashangaa atakavyojifunza kwa urahisi.

Soma Jarida la Maarifa kwenye gazeti la Mwananchi kila Jumanne kwa makala kama hizi. Niandikie kwa bwaya@mwecau.ac.tz

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia