UmahiriHisia (Emotional Intelligence) ni Nini?

Umewahi kujiuliza kwa nini, wakati mwingine, mtu mwenye akili nzuri, mwenye weledi na uelewa mpana wa mambo, hujikuta na majanga mengi linapokuja suala la namna anavyoishi na watu? Shida ni nini? Iweje mtu aelewe mambo mengine vizuri lakini asindwe mambo madogo kama kuwa msikivu, mvumilivu wa mawazo tofauti, mwenye subira hali inayoweza kumuingiza kwenye magomvi na watu?

Wengine tunafikiri tuna misimamo mikali, tumenyoooka na hatujali kutofautiana na nani lakini ukitazama vizuri hiyo inayoitwa misimamo mikali  ni changamoto za kihisia, uwezo mdogo wa kuelewa mitazamo ya wengine, na saa nyingine ni kiburi tu kuwa tunajua kuliko wengine, hawana wanachoweza kutuambia na kadhalika. 

Kinyume na tunavyoamini wengi wetu, hisia hubeba maamuzi yetu mengi na ukitazama matatizo yetu mengi ya kitabia unaweza kuona mchango mkubwa wa kushindwa kuzielewa na kuzimudu hisia zetu. Ingawa tunazipuuza, ukweli ni kwamba ukishashindwa kuzishughulikia hisia zako, uwezekano wa kukabiliana na matatizo mengi ya kimtazamo, kimaamuzi na kitabia unakuwa mkubwa. 

 

Hapa ninakuletea, japo kwa mukhtasari, elimu ya hisia, UmahiriHisia (UH) —emotional intelligence — ambao kimsingi ni uwezo kuelewa namna hisia zetu zinavyofanya kazi, kuzitambua kadri zinavyoitokeza, kuelewa nini kinazichochea, kuzirekebu (regulate), kuzimudu lakini pia kuelewa namna ya kuzitumia hisia hizi kuwasiliana na kuboresha mahusiano yetu na watu. 

 

Tafiti nyingi zinaonesha kuwa watu wenye kumudu hisia wana nafasi kubwa ya kufanikiwa kwenye shughuli zao kuliko watu wenye akili nyingi lakini wasiozielewa na kurekebu hisia zao. Hiyo, hata hivyo, haimaanishi hatuzihitaji akili bali kusema tunahitaji kujifunza zaidi namna ya kumudu hisia zetu ili, inshaallah, akili zetu zisitutie hasara. 

 

Hata utafiti niliouzungumzia hapa wa kupima subira kwa watoto —delayed gratification— kimsingi unatupa ushahidi mwingine wa faida kedekede za umahirihisia. Kwa mfano, mtoto aliyejifunza kumudu hisia zake anakuwa na uwezo wa kujizuia na hivyo kujiweka kwenye nafasi kubwa ya kufanikiwa kwenye maeneo mengi ya maisha yake kuliko mwenzake anayeendeshwa na hisia zake.

 

 

Daniel Coleman

UmahiriHisia (UH) ni uwezo unaofundishika wa kutambua, kurekebu na kumudu hisia zako unaoenda sambamba na kutambua, kuheshimu na kutumia vizuri uelewa huo wa hisia za mtu mwingine ili kuwasiliana naye, kuhusiana naye, na kutatua tofauti zenu bila kuingia kwenye migongano mikubwa isiyo ya lazima. 

UmahiriHisia ina mawanda mengi lakini Daniel Goleman aliyeitambulisha elimu hii ya ushunuzi wa hisia anautazama umahiri huu katika nyanja kuu tano muhimu —nitazieleza moja baada ya nyingine. 

 

1. Kuzitambua hisia zako mwenyewe—ikiwa ni pamoja na matokeo yake kwa wengine 

2. Kurekebu na kumudu hisia 

3. Kutambua na heshimu hisia za mwingine (ushirikeli) 

4. Kuchochea na kukuza motisha binafsi 

5. Kutumia hisia kwenye mawasiliano na mahusiano na watu

 

 

Mahiri tatu za mwanzo, yaani kutambua, kurekebu hisia  na kujenga motisha, kimsingi zinakuza uwezo wa kujitambua kwako, na mahiri mbili zinazofuata, yaani kutambua na kuheshimu hisia za wengine sambamba na mawasiliano zinakuza zaidi uwezo wako wa kuhusiana na kuwasiliana na watu wanakuzunguka. Kwa lugha nyingine umahirihisia ni uwezo unakusaidia kujitambua ili uweze kuwatambua wengine.

 

Kuepuka kukuchosha, nimegawa makala hizi katika vipande vitano vinavyoangazia suala moja baada ya jingine. Ukimaliza mfululizo huu, naamini, utakuwa umejifunza namna ya kufuatilia hisia zako kwa karibu, kuzirekebu kulingana na mazingira uliyomo, kuzisoma na kuziheshimu hisia za mwenzako, kuelewa ujumbe wake asiousema kwa maneno na pia namna ya kutumia uelewa huo wa hisia katika kuwasiliana na kuboresha mahusiano yako na watu.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia