Kutumia UmahiriHisia (Emotional Intelligence) Kuimarisha Mahusiano
Tunamalizia safari yetu ya kujifunza umahirihisia. Tumeangazia maeneo makubwa manne. Kwanza, uelewa wa hisia na sababu zake. Pili, tulitazama namna ya kurekebu hisia zetu. Kisha tukatazama namna tunavyoweza kujenga motisha na hamasa ya kufikia malengo yetu. Kisha tukaangalia namna umahirihisia unavyotuwezesha kuwasiliana na watu pasipokuzalisha migogoro isiyo na sababu.
Maeneo haya manne ya umahirihisia, yanatafsirika katika mahusiano yetu na watu —namna tunavyowachukulia wasioamini tunachokiamini, namna tunavyowajibu wasiofikiri kile tunachokifikiri, namna tunavyotatua migogoro na maamuzi tunayochukua pale tunapojisikia kuonewa.
Msingi wa mahusiano yenye tija na watu ni uwezo wako wa kujitambua, kutambua namna hisia na tabia zako zinavyoathiri wengine, namna unavyomudu hisia zako lakini pia kiwango chako cha upendo kwa watu. Mtu mwenye #UmahiriHisia hagombani kirahisi. Ukigombana naye anajua namna ya kujinasua na kukuachia ugomvi wako, anajua kukutanisha na ujinga wako, akakuacha ukigombana na kivuli chako, anajua kumaliza tofauti bila kuacha maumivu.
Kadhalika, mahusiano, kwa kiasi kikubwa, yanajengwa na mawasiliano. Kuna tabia ukiwa nazo wakati wa mazungumzo zinaweza kutuma ujumbe hasi kuwa hujali, husikilizi, huna haja ya kuelewa hali inayoweza kuleta kiambaza kikubwa cha mawasiliano. Tukizungumzia umahirihisia, tunazungumzia pia namna unavyoweza kumfanya ajisikie kuthaminika, kusikilizwa na kueleweka.
Tuone, kwa ufupi, baadhi ya tabia zinazoweza kujenga kiambaza cha mawasiliano na hivyo kuharibu mahusiano yako na watu:
Kukosa usikivu
Unazungumza na mtu na huonekani kuwa naye kiakili na kihisia. Upo lakini haupo hata kama husemi. Unapapasa simu, unapepesa macho kuwaangalia wanaopita au kuendelea na shughuli nyingine.
Kujikweza
Mwenzako anakusimulia jambo lake, lakini kwa kufikiri unachangia hoja, unaleta simulizi lako linalowaondoa kwenye jambo alilokuwa analizungumza. “Hilo mbona dogo sana? Sikiliza kilichonitokea mimi uone.”
Kushauri
Saa nyingine hata hujaombwa maoni, unadakia juu juu jambo la mtu na maelezo ya nini kifanyike au swali lenye ushauri, “Nadhani hapa ukafanye…” “Kwa nini hukufanya…” “Ulikuwa unafikiri nini kufanya hiki ulichofanya…”
Kufariji kwa kupuuza hisia
Tunahitaji faraja lakini ndio upuuze hisia za mtu? Mtu tayari ana hisia hata ukimwelekeza kuzipuuza anazo. “Usiogope. Usijisikie vibaya. Jikaze kiume.”
Huruma inayotia unyonge
Huruma sawa lakini ndio umhurumie mtu mpaka ajione habari yake imeisha? “Masikini pole jamani. Dunia kweli haina huruma kweli. Keshakuharibia maisha hapo.” “Halikuwa kosa lako kabisa. Sema mtu mwenyewe ndio kawa shetani kabisa.”
Kuelimisha
Unajipa kazi ya ualimu kwa tatizo la mtu. Unataka kuonekana unajua, una uzoefu na mwenye shida hana uelewa: “Mungu anajua kwa nini unapitia hili.” “Mungu amemchukua marehemu kwa wakati wake.”
Maswali mengi
Unauliza maswali yanayochonoa jambo mtu hajawa tayari kukuambia. “Unaendeleaje na masimango ya wakwe?” “Hebu niambie huyu ni mwanaume wa ngapi kukuacha?” “Ulijisikiaje alipokuwa anakulazimisha?” Magonjwa yetu mengi na ugomvi mwingi unaotusumbua ni kilio cha nafsi iliyokosa mtu wa kuisilikiza na kujaribu kuielewa. Ukiweza kumsikiliza mtu, ukajali anachokisema, unatibu mengi yanayowazuia kuzungumza.
Kufanyia kazi unachojifunza
Matokeo makubwa ya umahirihisia ni namna unavyohusiana na watu. Namna gani unafikisha ujumbe kwa mtu, hata katika mazingira magumu, huo ni umahirihisia. Namna gani unamkosoa mtu bila kutweza utu wake? Je, unaweza kuzungumzia kosa la mtu na bado ukamwonesha kuwa yeye bado ni binadamu anayestahili staha?
Unawezaje kumwomba mtu kitu bila kuonekana unashinikiza? Kuna lugha ukitumia unaonekana unadai unachostahili, hali inayoweza kumvunja moyo huyo unayemwomba akupe unachohitaji.
Je, huwa unakumbuka kushukuru unapotendewa jambo? Unatumia maneno gani katika kusindikiza shukrani zako? Haya ni baadhi tu ya maeneo yanayoweza kuonesha umahirihisia wako. Habari njema ni kwamba umahirihisia ni safari endelevu. Tunajifunza kila iitwapo siku.
Maoni
Chapisha Maoni