Kutumia UmahiriHisia (Emotional Intelligence) Kuelewa na Kuheshimu Hisia za Wenzako
Hivi huwa unajiuliza hisia zako zinawaathiri vipi watu wanaokuzunguka? Umewahi kujiuliza ni kwa kiwango gani, mathalani, wivu, husda, fedheha, majuto na hatia vinavyoathiri watu wanaokuzunguka?
Nimewahi kusikia watu wakijisifia kuumiza watu wengine.
“Sijali anajisikiaje shetani yule.”
“Kwanza nilikuwa nimekasirika. Usinisumbue.”
Haya ni maneno yanayotamkwa na mtu mwenye maumivu makubwa ya kihisia. Huwezi kuwa na umahirihisia ukiwa na maumivu yanayokufanya usijali mwenzako anajisikiaje.
UmahiriHisia unatuwezesha kuwa na uwezo wa kutafakari madhara ya hisia zetu kwa wengine. Kutokujali watu wanaathirika vipi na hisia zako, kujali tu hisia zako na kushindwa kuwaza wengine wanakuonaje, wanakuchukuliaje, uwezekano ni mkubwa kuwa una ulemavu wa hisia —hujali na wala hujisumbui kufikiri madhara ya tabia zako kwa wengine.
Kujifunza kufuatilia mwangwi wa hisia zako kwa wengine ni sehemu muhimu ya darasa la umahirihisia. Mahusiano yako na watu yanahitaji uwe na kioo kinachokuonesha mwangwi wa tabia zako kwa watu. Ukishakosa kioo hicho uwezekano wa kuharibu na kufanya maamuzi ya kijinga kwa kisingizio cha ‘this is who I am and I have no regrets’ ni mkubwa. Watu wa hivi mara nyingi ni wabinafsi wenye kiwango kidogo sana cha umahirihisia.
Uwezo huu, katika mukhtadha ya makala haya, unaitwa Empathy—ushirikieli, uwezo wa kumheshimu mtu kwa kiwango kinachokufanya utake kuelewa anachopitia, anachofikiri, anavyotafsiri mambo, na kubwa zaidi anavyojisikia bila kujaribu kumpuuza, kumtafsiria hisia zake kwa namna unavyotaka ajisikie wala kujaribu kumbadilisha afikiri kama wewe, aone kama wewe, ajisikie kama wewe.
Uso wa kila unayekutana nae hubeba mawimbi yenye ujumbe unaoelezea kinachomsibu. Kama tulivyokwisha kulieleza hili kwenye makala iliyopita kuhusu msamiati wa hisia, mawimbi haya yanaweza kubeba ujumbe wa kupoteza, kufurahia, kutishwa, kuumizwa, kukerwa, kushangazwa, kufedheheshwa, kuhurumiwa, kuomba msaada na kadhalika. Uwezo wa kuyasoma mawimbi haya, kuyaheshimu na kuchukua hatua stahiki kufanyia kazi ujumbe wake ndio unaoitwa ushirikieli (empathy).
Uso wenye furaha, kwa mfano, humaanisha hali ya kuridhika, utulivu na kukaribisha mahusiano. Uso wenye huzuni una masikitiko, unahitaji faraja na wakati mwingine huonesha kuelewa shida ya mwingine. Uso wenye wasiwasi umebaini hatari, hali ya kushindwa na hivyo unahitaji msaada. Uso wenye hasira humaanisha kukorogeka kwa mambo, mtu ameibaini hatari na kajiandaa na mapambano. Uso wenye kukerwa huonesha kutokupendezewa na jambo na hivyo kukosa uvumilivu na pengine huhitaji kueleweka. Uso wenye mshangao huonesha hali ya kutokutarajia, kutokuamini kilichotokea, na pengine hitaji la udasisi na kujifunza. Uso wenye dharau unajisikia kutwezwa na unahitaji mipaka.
Bahati mbaya, wengi wetu ama hatuna uwezo wa kuyasoma mawimbi hayo na kuyaelewa, lakini wakati mwingine hata tukiyasoma mawimbi hayo tunakuwa wachoyo wenye ujasiri wa kutokujali na wakati mwingine kupuuza. Uwezo huu wa kusoma mawimbi yanayobebwa na hisia za watu tunazaliwa nao. Mtoto ana uwezo mkubwa wa kuhisi kinachoendelea kwenye maisha ya mama yake hata mama asiposema kwa maneno. Kwa kuutazama uso wa mama yake, mtoto ana uwezo wa kuielewa furaha yake, matumaini yake, huzuni yake, na maumivu ambayo wakati mwingine mama hawezi kuyasema.
Uwezo huu, kwa kiasi kikubwa, unahusishwa na hitaji la kimaumbile la mtoto kujihakikishia usalama wake. Katika miaka ya mwanzo, kwa mfano, mama ndiye mtu muhimu anayeamua kiwango cha usalama anachojisikia mtoto (secure base). Kwa sababu hiyo, mtoto hulazimika kuusoma kwa makini uso wa mama kujua mtu huyo muhimu zaidi kwake anaendeleaje. Uso wa mama unapoonesha ‘makasiriko’, mtoto hupatwa wasiwasi asijue nini kimeharibika. Hali hii ikiendelea kwa muda inaweza kumfanya mtoto akatafsiri ufubavu huu wa uso wa mama kama ishara ya kukosekana usalama anaouhitaji. Ikiwa kuwa zawadi kubwa ya kimalezi mama anaweza kumpa mwanae ni kuwa na uso uliochanua, wenye uchangamfu na matumaini. Uchangamfu wa mama hutafsirika kama usalama kwa mtoto. Mtoto anayejisikia salama huwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na utulivu wa nafsi unaojenga tabia njema.
![]() |
Mama akicheza na kichanga chake |
Kadri tunavyokua, kwa sababu mbalimbali, uwezekano wa kuupoteza unakuwa mkubwa. Tunaanza kuwa watu tusioweza kuelewa hisia za mtu zinahitaji nini kwetu bila kusubiri mtu aseme kwa maneno. Hata hivyo, ukiwa na utulivu wa nafsi, ukawa na hisia mwanana na watu wanaokuzunguka, hutokosa kuwa makini kufuatilia mawimbi yanayosomeka kwenye nyuso za watu na kuuelewa ujumbe uliobebwa na mawimbi hayo. Ukiliweza hili utaongeza uwezekano wa mahusiano yako na watu kuimarika na huo ndio umahirihisia.
Ukiacha mawimbi yanayosomeka usoni mwa mtu, kuna mengi asiyoweza kuyasema wazi unayoweza kuyabaini ukichukua hatua moja zaidi ukazungumza naye. Ukiwa na utulivu, ukawa msikivu bila kuharakisha kuelewa unachokisikia, utagundua kila kinachozungumzwa na mtu hubeba hisia fulani. Huwezi kuwa na umahirihisia bila kujijengea uwezo wa kuzielewa hisia hizi na kuzifanyia kazi. Tulisema uwezo huu unaitwa ushirikieli.
Watu tunaokutana nao maofisini, barabarani na kwingineko wanaweza kuwa na vifua vilivyojaa hisia mbalimbali bila kusema. Unaweza kuzungumza na mtu asiyesema lakini anayeteseka na hisia za husda, wivu, kiburi, fahari, hatia, fedheha na nyingine nyingi.
Naweza, kwa mfano, kuzungumza jambo linaloonekana la maana kikaoni lakini nyuma ya hilo ninalosema kuna husda, kwa maana kwamba najiona mnyonge, natishika wengine wakifanya vizuri. Sisemi wazi lakini ukinisikiliza huoni nikifurahia mema ya wengine.
Kadhalika, naweza kuzungumza nikiwa na wivu, kwa maana ya kujiona kama mtu asiyesalama mikononi mwa mtu nimpendaye, mtu aliyehatarini kupoteza, asiyepata anachostahili shauri ya ushindani huo unaomnyima utulivu.
Kuna hili la kiburi. Unaweza kumsikiliza vizuri mtu anayezungumzia jambo lake unaweza ukaona anavyojiweka kwenye upekee, ubora kuliko wengine na wakati mwingine akijikweza aonekane ndiye anayestahili zaidi kuliko wengine. Kuna mstari mwembamba sana kati ya kujisikia fahari na uwezo wako na kiburi. Ufahari unanifanya nifurahie mafanikio yangu na mema yanayonikuta lakini haunichochei kujichukulia kuwa bora ninayefaa na kustahili kuliko wengine.
Naweza pia kuonesha hisia za majuto, hali ya kusikitikia maamuzi niliyoyafanya au kushindwa kuyafanya na matokeo yake bila kupoteza matumaini. Naweza kuwa na hatia, hali ya kujiona mkosefu niliyekwenda kinyume na matarajio niliyokuwa nayo. Naweza kujisikia fadhaa, hali ya kufedheheka na kujiona dhalili, kujisikia aibu mbele za watu kufuatia maamuzi mabaya yasiyolingana na heshima ninayotaka kuwa nayo mbele za macho ya watu.
Ukizielewa hisia hizi kwenye mazungumzo ya mtu, ukazitumia kama taarifa muhimu zinazoongoza namna unavyozungumza naye kumsaidia kuishinda hali yake pasipokumfanya ajione mnyonge, wewe tunasema una umahirihisia —uwezo wa kubaini hisia nyuma ya maneno na matendo ya mtu, kuzibaini na kuzitumia kama rejeo la kuelewa mwenzio anapitia nini, yanamsibu masuala yepi na hivyo kukuza mahusiano yenu. Uwezo huu tunajifunza kama hivi na kwa kiasi kikubwa unategemea kiwango cha utulivu na umwanana wa nafsi ulichonacho
Ushirikieli ni ushahidi mzuri kuwa wewe una afya njema ya akili na unampenda mtu, unamchukulia kama binadamu anayestahili heshima na staha hata katika mazingira ambayo anakuwa amekosea, amekuudhi au anafikiri tofauti na wewe. Ingawa katika jamii inayoamini ubabe, vikumbo na kudhibitiana, ushirikieli unaweza kuwa msamiati usiowezekana, bado tunaweza kujifunza kuheshimu na kujali hisia anazopitia mtu mwingine.
Unapokuwa na ushirikieli, inakuwa rahisi kuwa mtu asiyehukumu kwa wepesi, anayekimbilia ‘kuelewa’ jambo asilolielewa, msikivu na mwenye uwezo wa kutenda matendo ya hisani na staha kwa wengine.
Kufanyia kazi unachojifunza
Nikuulize, mazingira yapi yamewahi kukuta ukajiona kabisa huwezi kujali hisia za mwenzako? Pamoja na alichofanya, maumivu aliyokusababishia, unadhani ungeweza kufanya nini tofauti kujaribu kuelewa hisia zake?
Kuna mazingira mtu anakukosea kama mwitikio wa kile ulichomtendea. Muhimu kutafakari makosa yako kabla hujaamua kumuumiza zaidi. Ushirikieli (empathy) una nguvu ya kukuchochea kurudia maneno anayosema mwenzako kama namna ya kujaribu kuelewa malalamiko yake. Hata pale unapolazimika kumuwajibisha, unafanya hivyo bila kisasi, chuki na ubabe.
Maoni
Chapisha Maoni