UmahiriHisia (Emotional Intelligence) Unavyosaidia Kurekebu na Kumudu Hisia

 Tunaendelea na elimu ya hisia. Katika makala yaliyopita, tumejifuza msamiati wa hisia. Mbali na kutofautisha mihemuko na hisia, tumedadisi namna hisia, katika ujumla wake, zinavyobeba ujumbe.  Kila hisia huja na ujumbe fulani. Umahirihisia ukuwezesha kutafakari ujumbe unaobebwa na hisia zako. 

 

Katika makala haya, ningependa tutafakari kwa pamoja namna ya kuzikebu na kuzimudu hisia zetu. Nianze na swali. Unakumbuka mazingira umewahi kujikuta ukifanya maamuzi mabaya kwa sababu hujipa muda wa kupooza hisia zako?  Unakumbuka kusema jambo ukiwa na hasira, kwa mfano, halafu baadae ukajutia? Unamwandikia mpenzi wako maneno makali shauri ya hisia za wivu lakini baadae ukishapoa unagundua hukuwa na sababu ya kusema ulichokisema?

 

Napenda nukuu moja ya mama anayeitwa Maya Angelou, “Watu wanaweza kusahau ulichokifanya. Watu wanaweza kusahau ulichokisema. Lakini watu hawawezi kusahau ulivyowafanya wakajisikia.” Unaweza kuona uzito wa hisia katika kumbukumbu zetu? Tunakumbuka zaidi hisia kuliko jambo. 

 

Tunapozungumzia uwezo wa kumudu hisia tunahitaji kushughulikia ukweli wa kimaumbile kuwa hisia hutuvaa kwanza kabla hatujafikiri na kuyachambua mazingira yaliyochokoza hisia zetu. Kimaumbile, tunahisi kisha tunafikiri. Unahisi kwanza kisha unafikiri. Tazama mchoro wa kwanza hapa chini. 

Mchoro unaoonesha uhusiano wa fikra na hisia



Kabla sijawaza kinachonikasirisha, mathalani, hatua ambayo inanihitaji kushirikisha sehemu ya ubongo inayofikiri, tayari ninakuwa nimeshakuwa kwenye mazingira ya kuchukua hatua —kushambulia, kujitetea, kusema maneno makali na kadhalika na kadhalika—hatua ambazo zina uwezekano mkubwa wa kuleta madhara ndani ya muda mfupi hata kabla sijaanza kutafakari. 

 

UmahiriHisia ni kutambua kuwa, katika mazingira kama haya, uwezo wangu wa kufikiri vizuri na kufanya maamuzi unakuwa umedumazwa kwa muda. Kwa nini? Sehemu ya ubongo inayoniwezesha kufikiri na kuchambua mambo (cortex) inakiwa imezubaishwa kwa muda na amygdala —kijisehemu kinachoratibu hisia na kuchukua hatua nyakati za dharura hususani unapokuwa na hisia za woga, hofu, msongo na sononi. 

 

Kinachokutofautisha na mtu asiye na uwezo wa kumudu hisia ni angalau kukumbuka kupooza hasira zangu kabla sijachukua hatua yoyote ninapokuwa kwenye mazingira yasiyoleta hatari ya moja kwa moja na papo kwa papo. Tazama picha ifuatayo kuelewa zaidi.  

 

Unapozidiwa na hisia (una hasira, una msongo wa mawazo au umependa kupindukia) sehemu ya ubongo inayokusadia kufikiri hufubazwa. 

Nikirejea swali nililoanza nalo hapo awali, ikiwa umewahi kufanya maamuzi mabaya kwa sababu hujipa muda wa kupooza hisia zako, huo ni ushahidi mzuri wa namna amygdala ilitafsiri mazingira hayo kama hatarishi na hivyo ilikusaidia kuchukua hatua bila kusubiri ufikiri.

 

Ingawa hisia hutawala tabia zetu, hata hivyo, bado tunaweza kuzimudu tukizielewa. Tunamudu hisia kwa kujifunza kutumia vyema ufahamu wetu kuzielewa hisia, kuelewa zinavyofanya kazi, mazingira yanayozichochea na matokeo ya hisia hizo kwa wengine. 

 

Uelewa wa hisia ni nyenzo muhimu ya kumudu tabia inayotawaliwa na hisia. Nikielewa kwa nini hisia fulani hujitokeza zaidi wakati fulani, ni rahisi kwangu kutokupelekeshwa nazo na inanisaidia kujua namna ya kukwepa mazingira yanayochochea hisia hizo. Kwa mfano, ninaelewa hasira niliyonayo ni mwitikio wangu kwa hali fulani na ikinivaa inalenga kunichochea niwe mbinafsi nitake kupambana na anayenikasirisha—nikielewa hivyo naamua kunyamaza au kuondoka kwenye mazingira ninayojua yamenikasirisha. 

 

Ninapojisikia hatia au huzuni, naelewa sababu ya mimi kuwa na huzuni ni baya lililonitokea. Najisikia hatia, kwa vile kuna kosa nimelifanya na hatia inalenga kunikumbusha kujirekebisha. Uelewa huo unanisaidia kutokuzidisha hisia hizi na kutafuta namna bora zaidi ya kuzi-experience bila kuniletea madhara. Ukiweza kufanya hivyo, maana yake umejifunza umahirihisia—emotional intelligence.

 

Katika kujifunza kumudu hisia, jambo la kutafakari ni pale unapojikuta katika mazingira ambayo unakuwa umechokozwa na tayari hisia zako zinakuwa zimechemka. Chukulia mazingira ambayo mtu anakutukana, anakudhalilisha, anasema maneno yanayotweza ufahamu wako na utu wako, na kimaumbile unajikuta ukiwa umekasirika, umehuzunika na umefedheheka. Unafanyaje kama mtu mwenye UmahiriHisia? 

 

Mazingira kama haya ni rahisi kukupandisha jazba na kukuchochea kupambana kwa hasira, kiburi, dharau, majivuno. Ukifanya hivyo unaweza kuridhika kihisia lakini ukadharaulika, ukajishushia heshima na hata kujiweka kwenye mazingira yanayokuingiza kwenye matatizo zaidi. 

 

UmahiriHisia ni kukumbuka kuwa ukishazidiwa na hisia, uwezo wako wa kufikiri unakuwa umezubaishwa kwa muda na hivyo uwezekano wa kufanya maamuzi yenye madhara unakuwa mkubwa. Kujitenga na mtu anayekuchokoza inaweza kuwa namna nzuri ya kuonesha UmahiriHisia. Lakini kujifunza kuchukua hatua zisizoleta madhara kwako na kwa mtu mwingine, kama vile kusema unavyojisikia bila kutumia lugha kali, inaweza kuwa vizuri zaidi.

 

Kufanyia kazi unachojifunza

 

Umejifunza msamiati wa hisia, na sasa umejifunza kuwa usipokuwa mwangalifu, kwa maana ya kuingia hatua ya pili ya somo la umahirihisia unaweza kujikuta ukihamaki na kufanya maamuzi yasiyoonesha kuwa una umahirihisia.  Je, unaweza kumudu vipi hisia kama upendo? Ule usemi wa penda kwa kutumia akili una maana gani kwa somo tulilojifunza? 

 

Unafanya nini unapokuwa na hisia kama huzuni, majuto, wivu, husda, majonzi, woga na kadhalika? Jibu ni kujifunza namna bora ya kushughulikia ujumbe wa hisia hizo kwa namna isiyoleta madhara kwako na yeyote anayekuzunguka. Umahirihisia ni kujifunza kuufanyia kazi ujumbe unaobebwa na hisia ulizonazo bila kuleta madhara. 

 

Kadhalika, ni muhimu kujifunza namna ya kurekebu hisia za mwenzako kwa kujiuliza nini hasa kimechochea hisia zake na wewe unaweza kufanya nini kumsaidia kuzimudu? Mwenzako anajisikia wivu. Jiulize umefanya nini kinachochea wivu wake? Je, maneno unayoyatumia kufurahia mafanikio yako hayaleti hisia za unyonge (husda) kwa mwenzako? Unafanya nini kufurahia mafanikio yako bila kumtia unyonge mwenzako? Huo ndio umahirihisia. 

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia