Kutumia UmahiriHisia (Emotional Intelligence) Kuelewa Unavyojisikia

Katika utangulizi wetu, nilieleza maana ya umahirihisia na nyanja zake tano. Nilieleza kuwa, ingawa umahirihisia una nyanja hizo tano, ukiyatazama vyema mawanda yake, unaona kuna maeneo makubwa mawili. Eneo la kwanza, ni utambuzi kwa maana ya kuelewa hisia zako, kuzifuatilia na kuzirekebu kwa maana ya kujifunza namna ya kuzimudu zisikuingize kwenye matatizo. 

 

Eneo la pili linategemea eneo la kwanza, kwa maana ya uwezo wa kutumia utambuzi huo wa hisia kuelewa namna ya kuelewa, kutambua na kuheshimu hisia za wengine kwa minajili ya kuboresha mahusiano yako na watu.

 

Katika sehemu hii ya pili, ninajielekeza kueleza kwa ufupi jinsi gani umahirihisia unaweza kukuzaidia kuzielewa na kuzirekebu hisia zako.

 

 

Umewahi kukutana na mtu mwenye uwezo mzuri wa kusoma ujumbe unaobebwa na uso wa mtu? Ukitabasamu, mwingine anaishia kwenye uso huo wenye tabasamu lakini yeye ana uwezo wa kujua kuwa pamoja na tabasamu lako, kuna kitu hakiko sawa. Unashangaa pamoja na kicheko chako, atakuuliza, “Mwenzangu uko sawa? Nakufahamu. Niambie nini kimetokea!” atakuuliza. Unashangaa.

 

Hawa ni watu wenye uwezo mkubwa wa utambuzi wa hisia, uwezo wa kusoma ujumbe uliojificha kwenye uso wa mtu. Ingawa sote tunazaliwa na uwezo huu wa kusoma ujumbe unaobebwa na uso wa mtu, kadri tunavyokua, kwa sababu mbalimbali, wengi wetu tunaupoteza na kuishia kuwa watu wa kutegemea maneno yatuambie mtu anapitia hali gani. 

 

Mihemuko

 

Hiki ninachojaribu kukieleza kitaalam kinaitwa mihemuko (ama emotions kwa Kiingereza). Kwa kawaida, hata mtoto mchanga huzaliwa na mihemuko kumuwezesha kujihami na mabadiliko yanayoendelea kwenye mazingira yake lakini pia kuwasiliana na wanaomzunhguka.

 

Mihemuko iliyofanyiwa tafiti zaidi ipo sita: 

Furaha 

Huzuni 

Woga 

Hasira 

Maudhi/kukerwa 

Mshangao 

Hebu tazama picha ifuatayo kuhusianisha na hiki ninachokieleza.  Unaweza kubaini mihemuko hiyo?  Unadhani ina maana gani? 

 

MihemukoMsingi (Basic Emotions)

Mihemuko hii, kimaumbile, inatuwezesha kuwasiliana na mazingira yetu kwa maana ya kuelewa kinachoendelea kwenye mazingira yetu na hivyo kutuchochea kuchukua hatua muafaka. Kadhalika, mihemuko hii hutusaidia kutuma ujumbe wa ishara kwa wengine ili nao wachukue hatua. 

 

Hasira, kwa mfano, inatusaidia kujilinda na kupambana pale inapobidi; huzuni (hutusaidia kujipooza tunapopoteza kitu cha thamani); furaha (hutuchangamsha na kukaribisha mahusiano); woga (hutusaidia kujihami na hatari); maudhi/kukerwa (hutusaidia kulinda tunachokiamini na kujitenga na tusichokipenda; mshangao (hutuma ujumbe wa udadisi, hali ya kutaka kujua kisichotarajiwa au kueleweka) nk.

 

Hisia

 

Tofauti na mihemko,  hisia ni namna tunavyoitikia na kujenga tafsiri ya mihemuko hiyo. Ingawa kuna mazingira ambayo hisia zinaweza kuonekana usoni,  hisia (feelings) si lazima zionekane usoni. 

 

Tofauti na mihemuko tunayozaliwa nayo, hisia tunajifunza kulingana na mazingira ya kimalezi, dini, tamaduni na namna tunavyotafsiri matarajio na hatua zinazochukuliwa na watu hasa wale tunaowaheshimu kama vile wazazi, marafiki, na watu wengine wanaogusa maisha yetu.

 

Hisia zipo kwa makumi. Hapa nina mifano michache:

 

Upendo

 Fahari

Hatia 

Majuto 

Fedheha 

Wivu 

Husda 

Chuki

 

Unadhani kwa nini sina picha inayoelezea hisia hizi? Safi. Si lazima zionekane usoni mwa mtu ingawa zinaweza kuonekana katika mazingira fulani fulani. 

 

Je, hisia hizi zina maana gani?  Unaweza kukumbuka tangu umeamka asubuhi hisia ipi imetawala siku yako zaidi? Unasoma makala haya hivi sasa una hisia gani? 

 

Nifafanue. Ukishaelewa kilichochochea hisia hizo, unaweza kuona, hakuna hisia mbaya. Kila hisia unazokuwa nazo kwa namna fulani zinakusaidia. Shida ni kuzidisha na ukizidisha unaingia kwenye matatizo na nafsi yako lakini pia inaweza kukugombanisha na watu. 

 

Ukitazama hisia ya fahari, kwa mfano, utaona hisia hii huja kama matokeo ya kufanya vizuri, kupata kile ulichokitarajia. Unajisikia fahari kufurahia matokeo ya kazi yako. Ikizidi nayo inaleta tatizo. Fahari inageuka kuwa kiburi. 

 

Husda, hisia nyingine, kuja ukitiwa unyonge na anayekuzidi. Husda hukufanya ujione huwezi shauri ya kujilinganisha lakini inaweza kuwa kichocheo cha kupambana. Ukizidisha husda unaweza kutengeneza tatizo la chuki.

 

Wivu, kwa upande mwingine, huja ukishahisi hustahili ulichonacho na pengine kuna tishio la kukikosa. Wivu huleta umiliki na hali ya kutaka pawepo mipaka kwenye kile unachoamini ni himaya yako. Kwa kawaida, wivu huenda sambamba na hisia za upendo. Unayempenda, kwa namna fulani, unakuwa na wivu naye unapohisi unashindana na mtu mwingine kummiliki.

 

Upendo ni hisia inayokuja unapojisikia salama kwa mtu. Unapojiridhisha na usalama huo, upendo hukusukuma kujitoa kwake na kadhalika na kadhalika.

 

Hatia hukukumbusha kosa, hukuonesha ulichofanya si sahihi. Mtu asiyejisikia hatia anaweza kufanya vitu vinavyoweza kuwashangaza watu. Unasikia hatia kukumbushwa kuzingatia matarajio ya watu wengine kwako. Hatia hujenga uwajibikaji.

 

Fedheha ni mashtaka ya ndani yako kukumbusha kulinda tunu ulizonazo na kujitathmini kwa miwani ya utakavyoonekana kwa wengine. Tunaogopa kufedheheka ndio maana wakati mwingine tunapambana kuwa watu bora. Tunagopa aibu.

 

Kufanyia kazi unachojifunza

 

Ukijifunza msamiati wa hisia, unakuwa umeanza rasmi darasa la umahirihisia. Nikukuuliza unajisikiaje sasa hivi utajibuje? Unajisikia vibaya? Unajisikia vizuri? Unajisikia kuchoka? Hapana. Jifunze kutumia msamiati sahihi kuelezea vile unavyojisikia. 

 

Badala ya kusema najisikia vibaya, sema najisikia kufedheheka. Najisikia furaha. Najisikia huzuni. Najisikia aibu. Unapotumia msamiati sahihi kuelezea hisia zako, maana yake unatambua hisia zako. Usiishie kutambua tu hisia, lakini jiulize nini kimechochea hisia hizo? Kwa nini unajisikia hatia? Kwa nini unajisikia husda? Hisia zako zinakuambua hitaji gani?

 

Kadhalika, ni muhimu kujifunza namna ya kusoma kwa usahihi ujumbe unaobebwa na nyuso za watu. Unakuwa mtu asiye na umahirihisia kama mtu anaweza kuonesha hisia fulani na wewe huna msamiati wa hisia hiyo. Unapokosa msamiati kile anachojisikia mwenzako, ni vigumu kuchukua hatua muafaka za kuufanyia kazi ujumbe anaotajia uupate. 

 

Nikuulize, kwa mfano, katika mazungumzo na mtu, unaona uso wake ukibadilika na kuonesha woga. Utafanya nini na ujumbe huo?

 

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Haiba ni nini?

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?

Tabia za Mtoto wa Miaka 0 – 3 Kimahusiano na Kihisia