Ukitaka Kujifunza Waruhusu Watu Waone Usichokiona
UKIFUATILIA mazungumzo ya wa-Tanzania wengi kwenye mitandao ya kijamii, unaweza kuona namna watu wanavyojinasibu kujua. Mijadala mingi imejaa ‘ujuaji’ unaofanya watu wajigambe, wadhihaki wengine, watukane na wakati mwingine, kadri ya mamlaka yao, watake kulazimisha kile wanachokiona wao ndio kiwe ukweli usiopingika. 

Katika makala haya, ninajaribu kuonesha kuwa ili tujenge jamii ya watu wastaabu wanaoheshimiana lazima tuwe tayari kujifunza hata katika mazingira ambayo tunaamini tunajua.

Labda utaniuliza, una maana gani unaposema ‘ujuaji’? Je, kujua ni jambo baya? Nikujibu kabla sijafika mbali. Kujua si jambo baya. Kimsingi ili mwanadamu akabiliane na mazingira yake na awe salama, analazimika kujua mambo kadha wa kadha. Mwanadamu anahitaji kujua wapi anaweza kupata mahitaji yake, nani ni rafiki yake, nani ni adui yake, wapi kuna dalili za hatari na mambo kama hayo ambayo ni msingi wa usalama wake.

Aidha, tunafahamu pia kuwa mbali na kutaka kujua ili kujihakikishia usalama wetu wa kimwili, maarifa yanatuhakikishia usalama wa kisaikolojia. Chukulia pale unapogundua umekosea. Unajisikiaje? Hatupendi kuwa wajinga (wasiojua) ndio maana tunapohisi kuna jambo hatulijui tunajisikia vibaya. Hata pale tunapopata taarifa sahihi zinazothibitisha kuwa tulikuwa tumekosea, bado tunakuwa wagumu kukubali makosa yetu. Maana yake kujua ni hitaji muhimu la kisaikolojia alilonalo mwanadamu.

Shida inakuja pale tunapofikiri tuko sahihi na wengine wote wenye mtazamo tofauti na ule tulionao hawako sahihi. Mawazo kama haya ndiyo ninayoyaita ujuaji. Ujuaji ni ile tabia ya mtu kutaka kuonekana ana ufahamu wa mambo hata kama wakati mwingine yeye mwenyewe anajua hujui.

Mtazamo kama huu ni dalili za upungufu mkubwa wa uelewa. Kwanza, ni kutokana na ukweli kuwa binadamu pamoja na kupenda kufahamu mambo mengi, bado tunafahamu mambo machache mno. Lakini pia, ufahamu wetu kwa asili una tabia ya kutudanganya bila sisi kujua tumedanganyika. Nikupe mfano rahisi.

Ukitazama picha hii hapa pembeni, kwa haraka haraka unaweza kudhani unaona sura ya kijana wa ki-Hindi anayetazama kushoto na nywele zake ndefu amezitimua kwa nyuma. Unachokiona ni kitu sahihi. Hata hivyo, huo si mtazamo pekee kwa picha hiyo.

Ingawa ni kweli umeona uso wa kijana wa ki-Hindi, bado unaweza kuona kitu kingine ukiwa tayari na kuufungua ufahamu wako. Tazama kwa makini kuona kama unaweza kumwona mtu mfupi jamii ya Waeskimo aliyegeukia ubao akiandika kitu kwa mkono wa kulia. 

Tazama kwa makini. Nikusaidie kumwona. Uso wa yule kijana wa ki-Hindi sasa utazame kama kichwa cha mtu huyu mfupi aliyejifunika koti lenye manyoya mithili ya koti la ‘Father Christmas’, shingo ya kijana wa ki-Hindi sasa itazame kama miguu ya mtu huyu mfupi, na nywele za kijana wa ki-Hindi sasa zitazame kama ubao wa kuandikia. Je, umemwona? Kama bado, tazama kwa bidii.

Huu ni mfano unaoweza kutusaidia kuelewa namna gani jambo lile lile linaweza kuwa na tafsiri zaidi ya moja kutegemea na kile tunachokitarajia au kutaka kukiona. Ndivyo ilivyo katika maisha. Suala hilo hilo unaloamini liko vile unavyojua linaweza kuwa tafsiri tofauti ikiwa tu utafungua milango ya kujifunza zaidi.

Unapojadiliana na watu, usilazimishe kuwa sahihi hata kama unaamini uko sahihi. Kile unachokiona ni kwa mujibu wa taarifa ulizonazo na imani uliyonayo tayari. Wengine unaofikiri hawako sahihi nao wanaweza kuwa na taarifa tofauti na zile ulizonazo wewe. Ukilazimisha waone kile tu unachokiona wewe unakosea.

Kama nilivyotangulia kusema, tunalazimisha kuwa sahihi kuliko wenzetu kwa sababu tunafikiri bila kuwa sahihi hatuwezi kuwa na heshima. Tunatumia ‘ujuaji’ kama silaha ya kulinda heshima zetu. Lakini je, huwezi kuwa sahihi na mwenzako pia akawa sahihi? Hatuwezi kuwavumilia wenzetu kwa kuona kile tusichokiona?

Nikirudi kwenye picha niliyoitumia kwenye makala haya. Hakuna mtu anayeweza kudai kuwa kile anachokiona yeye ndicho sahihi zaidi kuliko wanachokiona wengine. Mazingira tuliyokulia, mambo tuliyozea kuyasikia yanaweza kufanya ikawa rahisi zaidi kuona kichwa cha kijana wa ki-Hindi anayetazama kulia. Lakini hiyo haifanyi wanaomwona kijana mfupi wa ki-Eskimo wasiwe sahihi.

Lugha sahihi tunayoweza kuitumia ni kwamba wanaomwona kijana wa ki-Hindi wako sahihi, lakini pia wanaomwona kijana mfupi wa ki-Eskimo nao wako sahihi. Hakuna walio sahihi kuliko wengine hata kama hawaoni kile wanachokiona wengine.

Siku nyingine unapojadiliana na wenzako masuala yoyote yale iwe ni imani/dini, siasa, utamaduni, taaluma zingatia kuwa unachokiona wewe sicho wanachokiona wenzako. Taarifa ulizonazo wewe, sizo alizonazo mwenzako. Upande unaoona kuwa ndio sahihi, kwa wengine ni upande usiosahihi. Ukizingatia hilo, hutalazimisha kuwa sahihi wakati wote na hivyo utakuwa mwepesi kuvumilia mawazo tofauti na yale uliyonayo.

Maoni

 1. Changamoto ya kizazi kinachojua kama kinajua kumbe hakijui kinachotakiwa kujua ni kupinga kile kinachotakiwa kujua kwa wanaojua.
  Hivyo kufanya wanaojua kutokuwa na nafasi kwenye fahamu zao.
  Najifunza mengi kwako
  Mwalimu wangu.

  JibuFuta
  Majibu
  1. Nakubali kuwa siwezi kuwa sahihi wakati wote. Lakini Mwl, yako mambo ambayo ni dhahiri kama ilivyo "2+2=4" na wala hayahitaji mijadala. Lakini mtu kwa makusudi kabisa pengine kwa sababu ya nguvu fulani aliyonayo hutaka kufanya" 2+2=3"
   Hapo ndipo shida huanza. Hawa, wana matatizo. Sio kwamba hawajui, la hasha, wanajua ila wanajifanya hawajui.

   Futa
 2. Titanium Straightener: A Perfect Combination Of The Best Batteries
  In its price of titanium simplest form, the tibia straightener is an active gr5 titanium form of titanium fidget spinner the naturally active micro touch hair trimmer Thiibean tooth comb, the thiibean titanium banger tooth comb and the

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Fumbo mfumbie mwerevu