Lugha ya Ubabe Hupunguza Ushawishi Wako






Niliwahi kusoma barua ya mfanyakazi mmoja kwa bosi wake. Ingawa alikuwa na madai ya msingi aliyoyaelekeza kwa mkuu wake huyo wa kazi, kwa maoni yangu, alikuwa ametumia lugha isiyo na staha. Kwa kufikiri kuwa maneno aliyokuwa ameyatumia yangepunguza ushawishi wake, nilimshauri angebadili lugha kuifanya iwe rafiki zaidi. Hata hivyo, hakukubaliana na maoni yangu. Miezi michache baadae, barua ile ilimgharimu kazi.

Wengi wetu huchukulia kirahisi suala la lugha. Tunafikiri kwa sababu tunazo hoja na tunafahamu kile tunachokitetea ndio ukweli wenyewe, basi tuna hiyari ya kutumia lugha yoyote. Hatujali kuchagua maneno ya kusema. Tunasahau kuwa maneno yetu yana athari kubwa katika mawasiliano kama ilivyotokea kwa mfanyakazi yule.

Lakini ukweli wa mambo ni kuwa lugha, mbali na ujumbe, hubeba hisia. Kuna maneno ukimwambia mtu hata kama una hoja hatakuelewa. Nakumbuka siku moja nilimsikia mkubwa wa ofisi mmoja akitoa maelekezo kwa watu waliokuwa chini yake. Nilishangaa. Mkubwa yule, pengine shauri ya mamlaka yake, aliongea kama mtu anayezungumza na watoto wadogo ambao, hata hivyo, nao wanastahili heshima. Nilifikiri ilikuwaje mtu anaweza kuwakosea adabu watu anaotarajia ndio watekeleze maagizo yake.

Kwa upande mwingine nilimwelewa. Mkubwa huyu, kama wengi wetu, aliamini ubabe una nasaba na ushawishi. Kwamba ili watu watambue madaraka yake, ilikuwa ni lazima kwake kuwafokea na kuwatisha. Inaelekea kwa uelewa wake, aliamini vitisho na kelele vingesaidia kuongeza ushawishi wake. Alichosahau, mkubwa huyu, ni kwamba lugha ya ubabe hupunguza ushawishi.

Pengine unajiuliza ushawishi maana yake ni nini? Ushawishi ni uwezo wa kumfanya mtu mwingine, kwa hiyari yake mwenyewe, akubaliane na mtazamo wako. Maana yake ni kwamba unapofanikiwa kubadilisha mawazo ya mtu mwingine bila kumlazimisha hapo unakuwa umeweza kumshawishi.

Katika jamii yetu, mambo kadhaa yanaweza kuongeza ushawishi wa mtu. Mosi, maarifa. Mtu anayeaminika kuwa na taarifa sahihi –au ujuzi na uzoefu wa jambo fulani, anakuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na ushawishi zaidi kuliko mtu asiye na maarifa. Mwalimu wa shule, kwa mfano, ana uwezekano mkubwa wa kuwa na ushawishi kwa wanafunzi wake kuliko mwanafunzi kwa mwalimu wake. Kinachompa mwalimu nguvu ya kubadili mawazo ya mwanafunzi wake ni yale maarifa aliyonayo.

Lakini pia, hadhi ya mtu katika taasisi au jamii. Mtu mwenye nafasi au madaraka katika taasisi, kwa mfano, ana uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na ushawishi kuliko mtu wa hadhi ya chini.  Tunafahamu, kwa mfano, kiongozi wa taasisi huwa na uwezo mkubwa wa kubadili mitazamo ya wafanyakazi wake kwa sababu tu ya nafasi aliyonayo. Sambamba na madaraka, hadhi ya mtu pia inaweza kujengwa na uwezo wa kifedha. Sauti ya tajiri, mathalani, husisika zaidi kuliko sauti ya mtu asiye na kitu.

Hata hivyo, kuna uwezekano wa mtu mwenye nafasi ya kuwa na ushawishi kwa watu akajikuta akikosa ushawishi. Sababu moja kubwa inaweza kuwa uwezo mdogo wa kuwasiliana vyema na watu. Kama nilivyotangulia kusema, lugha ina nguvu ya kugusa hisia za mtu. Lugha inayobeba ujumbe wako ni lazima iguse hisia za mtu. Huwezi kumshawishi mtu anayejisikia kuonewa na kudhalilishwa hata kama ni kweli unachoongea kina hoja ya msingi.

Jamii yetu, kwa bahati mbaya, imetuaminisha ubabe na kiburi ndiyo silaha ya ushawishi. Tunafikiri tunapotumia lugha inayoonesha mamlaka yetu, lugha ya majigambo na ubabe basi tutakuwa na ushawishi zaidi kwa watu. Tunasahau kuwa majivuno, kiburi na ubabe, mara nyingi ni dalili za magonjwa ya nafsi yanayohatarisha ushawishi wetu.

Na ilivyo ni kwamba watu wababe, kisaikolojia, huwa ni watu wanyonge sana ndani yao. Ule udhaifu wanaojisikia ndani yao, ombwe la nafsi ndani yao, huwafanya watafute namna ya kuuficha.  Maneno ya kujikweza, kejeli na ubabe mara nyingi hulenga kufunika udhaifu wanaojisikia ndani yao.

Ndio kusema ikiwa tunataka kuwashawishi watu, kwanza kabisa, tunahitaji kushughulika na udhaifu unaosumbua nafsi zetu. Tunahitaji kupambana na ombwe la heshima tunalojisikia ndani yetu. Tukifanikiwa hilo, itakuwa rahisi kutumia lugha ya unyenyekevu na uungwana kwa watu.

Lugha ya unyenyekevu ile inayotambua nafasi na heshima za wengine. Lugha ya namna hii ndiyo inayoweza kugusa mioyo yao na kuwafanya wajisikie kuthaminiwa. Watu hawa wanaopoamini wamethaminiwa wanakuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kukupa nguvu ya kuwashawishi.

Maana yangu ni kwamba badala ya kutumia lugha zinazowafanya watu tunaowashawishi wajione dhalili, tunahitaji kujifunza namna ya kuwa wanyenyekevu kwa maneno yetu tukitambua kuwa ubabe haujawahi kuongeza ushawishi wa mtu katika mioyo ya watu.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Haiba ni nini?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Uislamu ulianza lini?