Unafiki na kutokujiamini kwetu

Unafiki ni hali ya kukuficha kwa makusudi kile kilichomo mawazoni/moyoni kwa lengo la kumwonyesha mtazamaji kuwa anachokiona ndicho, wakati ukweli wa mambo ni kwamba anachokiona ni tofauti sana na uhalisia.

Unafiki ni kama kuvaa gamba lisilo lako. Kubadili rangi ya mwonekano wako. Kuwa "artificial". Unafiki ni kinyume cha uhalisi. Kwamba naweza kuigiza mwonekano fulani ambao kimsingi si wangu katika hali halisi. Naweza kumtabasamulia mtu, wakati ukweli wa mambo ni kwamba ndani yangu nasikia kinyaa.

Naweza tembelewa na mtu, rafiki yangu mathalani, na ukweli ni kwamba nina kazi nyingi za kufanya lakini kwa kutaka kumridhisha rafiki yangu huyo, basi namwonyesha kufurahia ujio wake ingawa moyoni (ukweli wenyewe) ni kwamba namwona kama mpotezaji mkubwa wa muda wangu.Simwambii jinsi alivyoharibu ratiba yangu. Ila usoni anaona ninavyofurahia kuja kwake kiasi kwamba anaendelea kubaki. Na hata anapoaga, naweza kumwomba aendee kubaki, kumbe moyoni nikimsema kwa kukosa kwake busara.

Nakaribishwa chakula nile, lakini nakataa ingawa ni kweli naumwa njaa. " Ah nimeshiba bwana...nimekula sasa hivi" wakati moyoni unaomba akubembeleze zaidi ili ule. Bahati mbaya jamaa wala hawabembelezi, wanaendelea kukata mlo. Wenzetu wabaki kusindikiza matonge kwa macho. Mifano iko mingi sana. Na pengine hata wewe ndugu msomaji unayo mingine mingi mizuri zaidi.

Sasa nikuulize: ni mara ngapi umekuwa mnafiki? Unafiki una kazi gani?(humaanisha nini katika namna tunavyowasiliana na watu)
Je, unafiki unakubalika kwa mtu anayejielewa nafsi yake (self-concept)?
Je, unafiki unaweza kutupa habari ya namna mtu anavyojichukulia mwenyewe (self-esteem)?

Nakupa wito wa kujielewa ili uwaelewe na wanaokuzunguka.

Maoni

 1. Bwana; Kwa mtazamo wangu naona hiyo ya kukutaa chakula wakati una njaa inawezekana sababu ya aibu na pia kama ulivyosema kutaka kubembelezwa. Na hilo la ujio wa rafiki ni yale yale ya muda. yaani kama kungekuwa na ule uratibu wa kupeana habari kesho nakuja saa moja basi tungeweza kuwaambia rafiki zetu aise mwenzako kesho muda huo nina kazi njoo muda fulani. Pia labda kwa sababu ya UPENDO, mila na desturi basi amekuja na wewe unaonyesha furaha tu wakati hupendi. Lakini ungemwambia ukweli kila kitu kingeenda safi wewe ungekuwa na furahi na pia rafiki angekuwa na furaha. sijui kama nimeeleweka!!

  JibuFuta
 2. Kama ulivyosema Kaka Bwaya. Unafiki una sehemu kubwa ya maisha na si kuwa ni utamaduni, bali ni desturi za wengi. Tumelelewa katika maisha ambayo kwa namna moja ama nyingine yanapalilia unafiki na unapoamua kuwa mkweli na muwazi na ama kuweka unafiki pembeni, wapo wanaokuangalia vibaya wakidhani ni mkatili kwa kuyonesha hali halisi ya hisia zako. Unajua mwisho wa unafiki ni nini? UMBEA NA SHUTUMA BAADA YA MHUSIKA KUONDOKA kwa kuwa huwezi kumwambia akiwepo.
  Ni mambo yaliyotuweka tulipo kama nchi na twaweza kubadilika na kunufaika

  JibuFuta
 3. Nimepita hapa leo jioni.
  Bado natafakari. Nitatoa mawazo yangu kesho asubuhi.

  JibuFuta
 4. Naam yatupasa tujielewe vyema ili kujijengea mustakabali mpya wa maisha,ukijielewa utajua nini kinachokuzunguka, na utaelewa namna ya kukabiliana nacho, ni muhimu sana kujielewa na kujitambua ulipo unapoelekea na uliotokea.

  Wakatabahu

  JibuFuta
 5. Unafiki!
  Mi huwa nauweka kundi moja na uongo na usengenyaji. Nadhani vinayagusa maisha ya watu wengi kwa namna moja ama nyingine.

  JibuFuta
 6. Nadhani nimesahau mila nyingi...maisha ya uingereza yaweza kumbadili mtu...lakini tena kwa njia nzuri. Kwa mfano mtu akinipigia simu na niko kwenye shughuli nyingine, humwomba ruhusa kumpigia baadaye na hufanya hivyo pia...sio maneno matupu tu!
  Kisha nchi za ulaya ni vigumu kumtembelea mtu bila kumjulisha kuwa utapitia au yeye kukukaribisha kwake... watu wana mipango yao na waweza simamishwa mlangoni maana hukutarajiwa...utamlaumu nani?

  JibuFuta
 7. bado natafakari,
  Nitapita baadae

  JibuFuta
 8. Kwa nini tusiweze kuwa wakweli kwa nafsi zetu na watu wanaotuzunguka hata kama ukweli huo utasababisha kutokueleweka? Kipi afadhali, kuwa mnafiki ili kujenga mahusiano yasiyo ya kweli ama kutokueleweka kwa kuwa mkweli? Na je, huu utamaduni wa kuoneana haya bado tunauhitaji katika jamii zetu? Gharama za unafiki ni kubwa nionavyo mimi.

  JibuFuta
 9. nakubaliana nawe bwaya. unafiki unaletwa na ubinafs mkubwa alionao binadamu wa leo. unaona linaingia suala la chakula hapa hata kama hujaliongelea sana kwamba ni kidogo. tangu lini chakula kikawa kingi? ni kidogo milele ba tunagawana kila kidogo tulichonacho.

  waafrika sisi tunaamini katika usawa ndio maana sihitaji appointment yako kuja kwangu, we njoo tu hali utakayokut ndo hiyo sio kuanza kudanganyana mala niko bize, mara nini. sisi sote ni wamoja, kwangu ni kwako na kwako ni kwangu sio uniombe ruhusa kama vile unakuja kunichinja. unafiki wa kizungu ni pamoja na uchoyo.

  kuna unafiki wa kimataifa wa kijifanya wanakusaidia uendeleee wakati wanachukua raslimali zako. unafiki unaukaribu na uzungu na labda ndio sababu wazungu wanakuja kuhubili injili ya upendo kwetu wakati wanapigana vita kama iraq na kwingine.

  unafiki unaendana na uchoyo, ubinafsi na fitina,
  nimetaupu vya kutosha

  JibuFuta
 10. I think there z aloot to discuss through dis thing hypocrite coz t leads also to poverty

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Malezi yanapokuwa ‘rasha rasha’ tuilaumu teknonojia?

Tumia Mbinu Hizi Kuelewa Unachokisoma -3

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3