Yupi wa maana kwako: Akukosoaye ama akusifiaye?

Ipo haja kubwa ya sisi kama binadamu kuufahamu udhaifu wetu. Ni kazi ngumu ambayo watu wengi hatuipendi. Huenda ni kwa sababu ni kazi isiyoonekana kuwa na tija ya haraka haraka. Na pengine sitakosea nikisema ni zoezi linalojeruhi mtazamo wetu hasa ikiwa hatujielewi.

Mtu asiyejielewa ni rahisi kuumia akiambiwa alikokosea. Hufarijika sana akisifiwa kizembe. Kwa nini iko hivi, hapo ndiko twapaswa kuanzia: Je, sifa zamsaidiaje asiyejielewa?

Najua Mtambuzi ameandika mara nyingi kutusihi kuhusu kutokuutazama upande wa pili. Nakubaliana naye. Kwamba wengi wetu, hutumia muda mwingi sana kuutazama upande wa udhaifu/mapungufu waliyonayo watu wengine. Tunakuwa mafundi wa kuchambua madhaifu ya wengine. Kila kitu kinatazamwa kwa nia ya kugundua tatizo la wengine. Iwe katika haiba (personality), kazi, mafanikio nk. Ndio maana hata tunaposikia mwenzetu kaharibu mahala, twathubutu kufurahia (hata kama ni kimoyomoyo).

Kutokuungalia upande wa pili, vile vile ni aina fulani ya faraja. Ni juhudi za kutafuta farijiko la kisaikolojia mithili ya kujisahaulisha tatizo. Kila mtu anapenda kuishi kwa matumaini yanayopunguza hisia mbaya katika nafsi zetu. Kuangalia upande mzuri kuna faida.

Hata hivyo, hiyo haiondoi haja ya sisi tujitizama udhaifu/upungufu wa haiba/tabia zetu. Sababu, katika kujielewa, nadhani, tunawajibika sana katika kuyabaini madhaifu tuliyonayo. Yaani kujitazama udhaifu wetu kwa lengo la kujirekebisha. Sizungumzii kuhangaika na kazi ya kuona wapi pana kasoro ili tubaki na shinikizo la damu kwa hisia za kukosea. Nazungumzia kuutazama upungufu tulionao katika haiba zetu kwa kusudi la kuangalia namna ya kuurekebisha hata kama kufanya hivyo kwaweza kututoweshea "kifuraha flani" cha muda mfupi.

Kutokuujua udhaifu wako ni sawa kabisa na kuishi kwenye nyumba isiyoezekwa kwa matumaini kwamba mvua inyeshapo kuna miujiza itakunusuru na dhahama. Kwamba unaogomba kuingia gharama za muda mfupi wa "matengenezo" yanayokuhakikishia amani ya kudumu.

Wengi wetu tunapenda kusifiwa. Masikio yetu yamekaa mkao wa kupambwa sifa (hata kama ni za uongo) almuradi tujifariji kuwa na sie tupo. Pengine huu ndio ubinafsi ambao mzee wa changamoto anauhoji. Kwamba "sie" hawa hawa unaopenda mafagio, ndio hawa hawa tunakuja juu tuambiwapo kuwa tumekosea mahala (hata kama ni kwa nia njema kabisa). Hii ni kusema kuwa hatupendi kile tuwafanyiacho wengine, kifanywe kwetu.

Nayasema haya kwa sababu ninaamini kabisa kwamba ili kupiga hatua za kweli kwenda mbele, tunayo kila aina ya sababu ya kutafuta kuujua udhaifu wetu kwa lengo la kuushughulikia. Kwa sababu udhaifu huo waweza kuwa kero kwa wanaoishi nasi hata kama sisi hatuujui. Udhaifu huo waweza kuwa kizuizi cha tutuzinga kufika mahala ambapo tungeweza kufika.

Ni muhimu kwetu kuwa tayari kusikia watu wakituambia mapungufu yetu (bila kujali nia zao) kuliko kupanua masikio kusikia sifa tusizozistahili. Maana sifa hizo zaweza kuwa udhaifu wetu wa kutuzinga kufika tuendako.

Nilichotaka kuuliza ni hiki: Yupi huonekana kuwa wa maana kwako, akukosoaye ama akusifiaye? Ni kwa kwa kiasi gani jibu la swali hilo hapo juu linakusaidia kujua kiasi chako cha kujielewa, hapo ndiko uliko mjadala. Samahani kwa mwandiko wa mcharazo. Huo ndio udhaifu wangu wa kwanza.

Maoni

 1. Kwa mtu anayenisifia kuhusu jambo fulani,kwa kweli ni lazima nilinganishe sifa na jambo lenyewe,kwamba mbali na kusifiwa,je na mimi binafsi naridhika na kinachopelekea mimi kusifiwa? Kwa sababu kuna wengine wanamsifia mtu ilihali wakijua kabisa alichokifanya ni upupu mtupu na pia kweli,kuna wengine wanamsifia mtu kweli kwa jambo fulani zuri lililofanyika.
  Kwa upande mwingine kwa kweli ukipata mtu anayeweza kukuambia udhaifu ulionao,hilo ni jambo zuri na la kushukuru.Upokee udhaifu ambao upande wa pili umekueleza,kaka chini alafu ujiulize,hivi udhaifu nilioambiwa ni kweli ninao.kama udhaifu ule unao,ni dhahiri kabisa utaugundua udhaifu wako.Kwa hali hii ya kukaa chini na kutafakari kuhusu udhaifu wako utagundua kuwa toka awali kuna jambo fulani ambalo ulikuwa hulitekelezi,swala hili la self assessment.
  Hata hivyo kuna swala jingine la wivu ambalo huambatana sana na kusifiwa pamoja na kuambiwa udhaifu.Kuna watu ambao huelezea udhaifu wa wengine ili tu kuwaharibia utu wao baada ya wao kufanya mambo mazuri na kuna wanaosifia wengine kwa kejeli tu,japokuwa wazi inaonekana kuwa kwa kile kilichopelekea kusifiwa hakikustahili,badala yake ilitakiwa iwekwe wazi kuwa watu hawakuridhika ili ajifikirie kuhusu kubadilika.
  Kulingana na maelezo yangu hapo juu kukosolewa na kusifiwa yote ni muhimu ktk kuyaelekea mafanikio.Nikikosolewa,mimi kama ni muungwana nitapokea na kufanyia kazi,na nikisifiwa,sitavimba kichwa,nitapima kwa nilichosifiwa nacho,inaögeza faraja na kuahidi kufanya mazuri zaidi.

  JibuFuta
 2. Ahsante sana kaka kulileta hili mezani.
  Pengine nianze kwa nukuu ifuatayo, "only your true friend will tell you the truth when your face is dirty"
  Kumbe yule akukosoaye ndiye afaaye zaidi. Na ndiyo maana wakati wa fainali za Miss Tanzania mwaka 2006, Lisa Jensen alipoulizwa swali anadhani rafiki ni nani, akajibu, "a friend is someone who can clearly see your weaknesses and help you to overcome them."
  Kumbe mtu akiweza kuyaona mapungufu, basi anatenda vema anapokusaidia kuyashinda. Atakusaidiaje endapo hatokukosoa?
  Hizi sifa mara nyingi ni vilemba vya ukoka. Mshairi mmoja alisema mara nyingi watu humsifia mtu wakiwa na sababu binafsi. Hivyo akawalinganisha na vioo vya kujitazamia. Akatahadharisha akisema, "beware of mirrors, because they only reflect what you think of your self."
  Kumbe watu wengi, mathalani maeneo ya kazi, wakimaizi kuwa bosi wao ni mpenda sifa basi kutwa nzima haweshi kumwaga sifa hata katika mambo ambayo kwa dhahiri hayahitaji sifa.
  Lakini pia sisi, wengi wetu tunayo mapokeo mabaya. Mara nyingi wale wanaotukosoa hatuwapendi. Tunasahau kuwa binadamu si wakamilifu.
  Tunasahau pia kuwa kukiri udhaifu hakumdhoofishi mtu, bali kunamuimarisha.
  Wengi wetu tunapenda vichwa vikubwa, kumwagiwa sifa tu.
  Nimeipenda sana mada hii. Hapa naweza nikaandika mpaka kesho, ngoja kwanza, nitafurahi kusoma maoni ya ndugu zangu.
  Ahsante sana.
  Alamsiki.

  JibuFuta
 3. Mambo mawili ya kuangalia kwa pamoja. Anayekusifia ni hakufai. Ila wewe ukiwa na tabia ya kusifia wenzako kikwelii kwa kutazama yale yanayostahili sifa, unafaa. Anayekukosoa ni mzuri kwa sababu anakuonyesha pa kujirekebisha. Tukumbuke si rahisi sisi kujua tuna udhaifu gani. Ila wewe ukiwa na tabia ya kuwakosoa wenzako kwa kuangalia mabaya yao, hufai. Tukumbuke hakuna asiye na mabaya.

  Kulijibu swali la bwaya nafikiri anayependa sifa hajiamini kama yule anayependa kukosoa wenzake. Anayependa kukosolewa anajiamini kama yule mwenye uwezo wa kumpongeza mwenzake anapofanya vizuri bila kujisikia wivu.

  Mimi ni mdau wa Arusha naugulia maumivu ya kufukuzwa chuo.

  JibuFuta
 4. hehehe. serikali ya tanzania inajivunia mno kusifiwa nje huku ikilalamikiwa ndani na kuwashangaa wa ndani ya nchi wanaolalamika wakati wa nje wanashukuru na kupogeza hata kama wanachokipongeza hakionekani. yafaa tuangalie anayesifia ninani na asiyesifia na kwa nini hivyo.

  wanawake wengi humalizwa na sifa za kipuuzi kama vile umependeza.. umesuka vizuri... nk.

  lakini kuwa chanya ni muhimu kuliko kuwa hasi! umejaribu lakini... umejitahidi ila... ni wazo zuri japo hapa si mahali pake... nk

  JibuFuta
 5. Asante sana Kaka Bwaya.Ni swali zuri linaloweka "mstari mwembamba" kati ya hao wawili ulioliza (akosoaye na asifiaye). Kama walivyochangia waheshimiwa hapo juu, kusifia na kukosoa zote ni muhimu katika maisha yetu. Hapa (kwa mtazamo wangu) tatizo linakuja kwenye kipi chasifiwa ama nani asifiaye na pengine kwanini usifiwe? Utategemea sifa pale uendapo kutoa misaada. Si sehemu nyingi tunapoweza kupata watu wenye NIA NJEMA ya kukosoa. Lakini kuna kitu ambacho nakiona na sijaona aliyekichangia. Na hicho ni namna tupokeavyo sifa na ama makoseo tupewayo. Naamini njia njema ya kupokea sifa na makoseo ni kwa kuangalia "point of view" kuliko "tone". Sifa za kweli huenda kwenye point of view na hazijazwi uongo kuzipa tone nzito. Kwa hiyo kwangu mimi nadhani wote wana wana maana kwa kuwa siangalii VIPI AMESIFIA, bali naangalia NINI KIMESIFIWA. Na huo ni mtazamo wangu na nashukuru saana kwa mada hii nzuri na asante kwa wachangiaji wote.

  JibuFuta
 6. Mijadala yenu inasaidia.Nitashiriki mara nyingne japo kwa kusoma

  JibuFuta
 7. Mada imetulia na mkuu ameiwasilisha wakati muafaka.
  Pamoja na kwambawachangiaji walinitangulia wamesema karibu yote niliyotaka kuyasema, lakini naona sitotenda haki kama sitasema japo jambo moja ili kusherehesha mada hii.
  Ukweli ni kwamba kutokujiamini ndiko kunakosababaisha watu kuogopa kukosolewa,. Kama ukikuta mtu anapenda sana kusifiwa, basi jua kwamba huyo ni mtu ambaye hajiamini.

  Tunapokosolewa tusichukulie kwamba ndio tumeshindwa, bali tuikubali hiyo changamoto na kujirekebisha.

  hatuhitaji kusifiwa na mtu mwingine ili tukamilike.

  Sisi ni watu kamili.

  JibuFuta
 8. UKIMYA HUU UNANITISHA, SIJUI HUYU BWANA ANAKULA WAPI SIKUKUU?
  KILA NIKIPITA KATIKA MJI HUU SIONI HATA DALILI YA MTU, PAKO KIMYAAA!!!
  PAKO KIMYAAA!!
  SIJUI WENYEWE WAKO WAPI? MAANA HATA ILE MIFUGO, KUKU, BATA, MBUZI NA NG'OMBE NINAOWAKUTA HAPA NJE NAO HAWAPO,AU WENYEWE WAMEHAMA KUTAFUTA MALISHO MAPYA?

  JibuFuta
 9. Kiunganishacho kukosolewa na kusifiwa ni MAPUNGUFU.

  Binadamu anamapungufu ndio maana anafurahia sifa au kunyong'onyea akijulishwa mapungufu.

  Cha ajabu , kila mwanadamu anajua kuwa binadamu anamapungufu ingawa anaweza kuchukia akionyeshwa mapungufu.

  Binadamu anahitaji kusifiwa na kukosolewa kuendeleza mrindimo wakujisikia anaishi.

  Tatizo ni...
  ... akusifiaye au akukosoaye, ANAJUA nini?

  Akukosoaye maswala ya MUNGU kwa misingi ya Biblia wakati wewe unajua na kuamini biblia iliandikwa na watu kama Mheshimiwa Kikwete, utakosolewaje ukosoleke kwa kutishiwa NAYE usilewe halafu Yesu anatengeneza Mvinyo?


  Unaweza ukasifiwa kitu ufikiriacho ni uongo lakini kwa mtazamo wa asifiaye KWAKE ni kweli na kwake kikojoleo hakina tofauti na kinyeo.

  JibuFuta
 10. Nimerudi jamani.

  Swali kwa wadau wote: Tutaujuaje udhaifu wetu? Kuna watu wanaamini kabisa kuwa hawana mapungufu. Au yale wanayoamini si upungufu kumbe ndio upungufu. Na yale wanayodhani ndio upungufu kumbe wala si upungufu. Tutatumia vigezo gani kuyabaini mapungufu yetu?

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Fumbo mfumbie mwerevu