Rariki yangu Rama muuza magazeti

Kazi ya kwanza niliyoifanya baada ya kufika Singida ni kulazimisha matangazo ya blogu zetu. nimekuwa nikibadili 'settings' kwenye kila kompyuta niliyoitumia kwa kubadili 'home page' iliyopo kuwa blogu moja wapo kati ya nyingi tulizonazo watanzania. Nimebadili badili baadhi ya kopyuta na mpaka sasa kuna kama blogu kumi hivi kama home page. Kwahiyo, kama inavyotarajiwa, kila mtumiaji wa kompyuta husika anapojaribu kuingia mtandaoni, atasalimiwa na blogu ya kiswahili. Hiyo nadhani inaongeza wigo wa blogu zetu.

Nilifanya hivyo pia kwa baadhi ya miji niliyopita mwaka huu. Nadhani inasaidia kuzitangaza blogu.

Ukweli ni kwamba bado matumizi ya mtandao yamekuwa zaidi katika kuandikiana barua pepe na mambo yetu yaleee niliyoyasimulia juzi. Hata ivyo naamini mabadiliko hata kama yanaonekana kwenda taratibu, bado yanakuja. Ni wajibu wetu kuyachochea.

Leo nimekuja kwenye cafe nyingine. Hii kidogo iko wazi sio kama ile iliyokuwa imefunikwa gubi gubi. Kuna jamaa hapa tumekaa karibu. Ananicheki nafanya nini. Kazi kweli kweli. Na inaonekana anasoma kila ninachofanya. Anatabasamu mwenyewe. Nahisi kasoma sentensi hizi za kumsemea kwa wasomaji wangu. Anatingisha kichwa sasa hivi. Nadhani ananishangaa. Ananiangalia kwa kuibia bia. Nadhani ana maswali mengi kuliko majibu. Tuachane naye.

Miaka ya nyuma nikiwa kidato cha kwanza na pili mjini hapa nilikuwa na rafiki yangu wa muhimu sana. Rama. Rama alikuwa muuza magazeti mitaa ya Posta. Urafiki wetu na Rama ulikuwa na sababu. Sababu yenyewe ni kwamba kila siku ningeweza kwenda kwa Rama Magazeti na angeniruhusu kusoma magazeti yote ya siku hiyo. Enzi hizo nilikuwa msomaji mzuri sana wa magazeti japo sikuwa na uwezo wa kuyanunua. Niliweza kumudu kununua moja tu la wiki: Rai. Rai enzi hizo bwana halikuwa mchezo. Nikiwa nyumbani jana nilipekuwa pekua maktaba ya magazeti hayo. Rai limebadilika sana siku hizi. Kuna tofauti kubwa mno ya magazeti ya Rai enzi za nguvu ya Hoja na haya ya siku hizi. Ndio maana sishangai siku hizi watu wengi wameachana nalo. Nini kimetokea?

Basi. Rama nimemtafuta simwoni. Naambiwa siku hizi kaamua kufanya mambo mengine. Hauzi tena magazeti. Sina namba yake. Sina jinsi ya kumpata. Basi sikuwa na la kufanya. Rafiki yangu Rama aliyenipa ofa za kusoma magezeti kaachana na kazi ya kuuza habari, anafanya kazi gazi siku hizi? Bila yeye nadhani kiu yangu ya kusoma soma viandikwa ingefifia kama sio kupotea kabisa.

Naandika kuwashukuru wauza magazeti. Urafiki na watu hawa umenifunza mengi. Japo wengi wao hawasomi wanachouza, lakini kule kuwa wakarimu kwa wauziwaji kunawasaidia. Mimi sikuwa muuziwaji. Nilikuwa ombaomba wa nisicholipia. Nawaheshimu sana watu kama akina Rama. Kumbe kila anachofanya mtu kina nafasi yake katika jamii. Jamii ina watu tofauti tofauti. Wenye uwezo tofauti tofauti. Wenye matakwa tofauti tofauti. Wenye maoni tofauti tofauti. Kumbe ni kwa sababu ya tofauti hizo, tunazo sababu za kutosha kutegemeana na tushirikiana. Tukishirikiana tutafaidiana. Kwa nini tusiheshimiane?

Maoni

 1. Kaka ahsante sana. Umenikumbusha zamani wakati nikisoma. Nilikuwa msomaji mzuri wa hilo gazeti. Lilikuwa moto kweli kweli, sijui nini kilichotokea.
  Siku hizi hata silitamani, blog zinanitosha kupata ninachokihitaji.
  Nakushukuru kwa kazi nzuri uloifanya huko Singapore (Singida) kazi nzuri.
  Kuna rafiki yangu huko aitwaye Balthazar Nkhangaa.
  Napenda kukutakia kila la kheri katika mambo yako.
  Wikend njema.

  JibuFuta
 2. Huwa sitamani siku ya kuhojiwa niwataje walionisaidia kufika hapa nilipo. Amini usiamini, kama ukikaa chini na kuwaza kwa undani utagundua kuwa takribani kila aliyeshiriki maisha yako ana mchango. Nazungumzia hata wale waliokuudhi na ambao ulitaka kuwadhihirishia kuwa hawako sahihi ama wewe ni zaidi yao na kufanya maamuzi ambayo yamekunyanyua harakaharaka. Unadhani hawa hawastahili shukrani? Kuna mengi na wengi wa kushukuru na nikiambiwa nifanye hivyo ntasema kwa ujumla tu (ukiachilia ndugu wa karibu kama Baba, Mama, Dada, Kaka) maana wakati mwingine waweza kuchelewa basi kwa kuwa dereva kawahi kuondoka, na wakati unasubiri lifuatalo ukaonana na mtu ama baada ya kupanda la pili ukaongea na mtu ambaye atakupa "mchongo" unaoweza kubadili maisha yako. Unadhani utakumbuka kumshukuru yule dereva aliyekuacha? Lakini ni kweli kuwa kukuacha kwake kumebadili maisha yako? Wale walioachwa na Mv Bukoba wakawa wanalia kisha wakasikia kilichotokea wakati wanakaribia Mwanza unadhani walishukuru kuachwa? Ukiangalia sana, kila mtu ana nafasi yake kwenye maisha. Awe anasifia ama anakosoa. Tatizo ni namna tuamuavyo kuchukulia mahusiano yetu na wenzetu.
  Salamu kwa Rama ukimuona. Mwambie alichokirutubisha ndicho kitufanyacho tu-JIELEWE sasa

  JibuFuta
 3. Duu kuhusu gazeti ni kweli lakini je niwaambie kilichotokea? aisehee mtanilinda kweli? au mnaleta urani kazi kwelikweli

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kufanya Unapotafuta Kazi

Mbinu za Kumfundisha Mtoto Kusoma Akiwa Nyumbani

Kumsaidia Mtoto Kujifunza na Kumudu Lugha