Gwamaka: Kile tusichofundishwa madarasani

Leo nilipata fursa ya kupata chakula cha mchana na rafiki yangu Gwamaka. Gwamaka ni kijana mwenye changamoto nyingi. Ukiongea naye hukosi jipya. Ni mwanaharakati, mwanafalsafa mwenye kichwa kinachofikiri. Ni msomaji mzuri wa vitabu. Na unaweza kubashiri inakuwaje ukikutana na msomaji wa vitabu kama Gwamaka. Ni lazima nikiri kuwa vitabu vingi nilivyosoma, yeye ndiye alinishawishi. Hivi sasa kaniambia anasoma kitabu kiitwacho: Why we need you rich. Ameniahidi kuwa kina mambo mazuri katika eneo la fedha. Japo sijawa msomaji mzuri wa vitabu vya "fedha" nimeshawishika kukitafuta. Kwa hiyo unaweza kuona kwa nini tukio la kukutana naye huwa na umuhimu wa aina yake kwangu.

Basi. Gwamaka alipomaliza 'shule' aliamua kujikita katika shughuli binafsi. Hataki kuajiriwa. Aliwahi kuajiriwa miezi michache akaona sio. Hivi sasa yuko kwenye mchakato wa kutengeneza ofisi yake mwenyewe pale Mwenge, barabara ya Sam Nujoma. Mambo ya ujasiria mali. Kupata, kadiri ya unavyowekeza.

Anayo falsafa niipendayo: "what a school doesnt teach". Anaamini kuwa pamoja na mfumo wetu wa elimu kutujaza maarifa mengi, bado haoni ni vipi mfumo huo unatufundisha kufanikiwa katika maisha. Tunatengenezwa kuwa watu tegemezi wa kazi za kuajiriwa (pengine zisizo na tija). Shule zinatuandaa kuwa watumwa wa mawazo ya waajiri wetu.

Anasema kwa mfano, mtu akishahitimu kwa kupata cheti, akaajiriwa PPF tower, ofisi yenye kiyoyozi, usafiri (wa mkopo) kwenda na kurudi kazini, basi imetosha. Tabia hii imetulemaza. Haitufanyi tuwe wabunifu. Tutumie akili kujifanikisha. Tuchemshe akili zetu. Badala yake kila mtu anapigana kikumbo kula bingo kwenye mashirika makubwa makubwa yenye kuweza kumpa sifa za haraka haraka kwamba "jamaa ni mkurugenzi pale bwana!". Ndio maana leo hii msongamano hauishi jijini. Kwa sababu kila anayemaliza anataka kubanana kule kule.

Laiti, kwa kadiri ya Gwamaka, vijana wa leo wangetambua kuwa hawahitaji mtaji mnono kuliko "kijiwazo kidogo tu", nchi ingekuwa ingesonga mbele kwa kasi kubwa. Laiti kila mwanafunzi angesoma kwa malengo ya kuweza kupambana na mazingira yake yeye mwenyewe kivyake vyake, tusingekuwa tunazungumzia janga kubwa la ukosefu wa kazi wanalokumbana nalo wahitimu wa siku hizi.

Kwa mujibu wake (Gwamaka) kisichofundishwa shuleni ni namna ya kuvitumia vipaji tulivyonavyo kujiletea mafanikio yetu sisi wenyewe bila 'uzembe' wa kutafuta sifa za kuajiriwa pasipo tija. Anasema ushahidi wa hili ni kwamba mabilionea wengi wa dunia hii ni watu ambao hawakuwa na elimu kubwa. Hawakusoma sana. Wengine waliamua kuacha shule. Wakafanikiwa kwa sababu pamoja na kukosa "elimu" hawakukosa ujuzi wa kuvitumia vichwa vyao ipasavyo. Leo hii ni 'matajiri wa kutupa' pasipo hiyo tunayoiita elimu.

Je, unakubaliana na mawazo ya Gwamaka? Je, unafikiri utafanikiwa kwa kuringia "maarifa" ya darasani? Mfumo wetu wa elimu una mapungufu gani yanayotuzinga katika kutufinyanga kuwa watu wabunifu?

Maoni

 1. Nimefurahishwa na post ya rafiki yako Gwamaka hayo ndiyo mambo mimi mwenyewe pamoja kuwa nafanya sasa hivi ninakamilisha katiba yetu ya NGO inayoitwa Youth Development Network Organisation (YDNO)

  JibuFuta
 2. Nimepita hapa leo jioni.
  Habari ya Gwamaka nimeisoma na imenivutia sana.
  Samahani nina haraka kidogo, nitapita kuchangia wakati mwingine. nisalimie sana huyo bwana naomabunielekeze kuwa hicho kitabu kinpatikana wapi ili na mimi nikakinunue?

  JibuFuta
 3. Shabban kaka nini tena! Siku hhizi umekuwa spidi sana. Nani anakufanya kuwa mwenye haraka mara kwa mara! Bosi wako, mhadhhiri wako, nahiliu wako, ama mitikasi zako.


  Mimi simwungi mkono gwamaka moja kwa moja. elimu bado ni muhimu. isipokuwa elimu yetu inatuelimisha zaidi kuwa wategemezi wa ajira badala ya kujiajiri. elimu ya kukakariri zaidi.

  JibuFuta
 4. Aaaah Gwamaka!! falsafa yake nzuri sana nami yangu ni kiswahili inasema 'Tunajua tusichokijua'. Kaka Bwaya hii ina marefu sana ndiyo maana kila siku nakasirika nisomapo hii fani ya saynsi ya siasa yaani kukaririshwa tu na kadhalika. Lakini hii falsafa inahitaji muda kwani ipo katika Mchakato ili niifanyie hitimisho lake, mwelekeo, na msingi. Niligusia kidogo katika makala yangu Gazeti la RAI ile ya TUNAGOME SERA AU MFUMO? aliyesoma atagundua.

  JibuFuta
 5. Kaluse na yeyote anyependa kukisoma, kinapatikana bookshop moja pale Mlimani City. Kinauzwa Tsh.25,000.

  JibuFuta
 6. Anachosema Gwamaka ni kweli tupu. Mimi nampongeza kuonyesha kuwa ameelimika na sio kukariri masomo kama walivyo njemba wengi wanaomaliza chuo.

  Elimu ya Tanzania iko taabani bin taabani. Mimi nimekuwa nikijiuliza hivi kuna sababu gani ya sisi kuelendea kuukumabtia mfumo huu mbovu tuliourithi kutoka kwa wakoloni? Elimu isyofikirisha ya nini? Elimu inayojenga matabaka ya kazi gani?

  Umefika wakati wananchi wote tukashirikishwa kutengeneza mfumo bora utakaotuletea faida watanzania wote. Hatuwezi kuendelea kuwa chini ya kongwa la kikundi cha watu fulani wanaojidai kujua hatma ya watanzania wote.

  Bwaya kutumegea fikra za vijana ambao maoni yao hayasikiki kwingine safi sana

  JibuFuta
 7. Nimekusoma mzee, nitakitafuta.

  JibuFuta
 8. Mkongwe na mheshimiwa sana kwenye media Jenerali Ulimwengu aliwahi kuandika kuhusu elimu ya ukoloni ambavyo haitatukomboa. Na akatoa mifano ya namna tunavyoiga vitu ambavyo havijatengenezwa kwa ajili ya mazingira na maendeleo yetu. Nakubaliana naye kabisa. Kuwa elimu ni muhimu lakini pia tuangalie kama inatupeleka kule tutakako na sio kuishia kutumikia na kuendekeza yasiyoendekezeka. Kuendelea kuaminisha vizazi kuwa mkoloni fulani ndiye aliyegundua kitu ambacho tulikuwa nacho miaka yote. Lazima tujiulize kama mtu anayetamani kuendelea kuwa kiranja wa dunia ataweza kutupa elimu ya kutuwezesha kuwa na nguvu za kiuchumi kama yeye? Yawezekana? Lakini tatizo jingine ambalo GWAMAKA hajaligusia ni ujasiri wa kujaribu. Hao mamilionea walijaribu na kushindwa kabla hawajafanikiwa na mara zote unapojaribu na kushindwa unajifunza kitu ambacho hutojifunza mpaka ujaribu. Pasina kujaribu hautajifunza kwa hiyo ni lazima ujaribu ili ujue njia sahihi ya kujipanga upya ili ufanikiwe. Ni kitu ambacho wengi hatufanyi nyumbani labda kwa kuwa hatupendi "kutibua bajeti" yetu. Lakini ni njia pekee ya kufanikiwa. Kumbuka niliandika kuwa "tutavuna tulichopanda, yaani ni lazima tuwekeze ili tufanikiwe" Elimu yetu inaondoa ujinga na kutuwezesha kuwasiliana katika harakati zetu za kimaisha, lakini huo ni moto tu, na kama twahitaji "mlipuko wa mafanikio" basi twahitaji kumwaga "petroli ya ubunifu na ujasiri" katika elimu tuliyonayo.
  Asante kwa mada njema Kaka

  JibuFuta
 9. Mawazo ya Gwamaka ni mazuri lakini labda asubiri mafisadi wote wafe. Kila eneo wamelishikilia. Sekta binafsi ambazo ndizo anazozingumzia zote wamekata mafisadi. Hatufurukuti. Hii nchi imeuzwa ndugu zangu. Inauma sana.

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3