Dialectic thinking: Ukweli ni kinyume chake

Dialectic thinking ni nini kwa Kiswahili? Sijui. Ninahitaji msaada wa dharura wa BAKITA. Lakini wakati tunangoja fasiri fasaha, hebu, walau kwa sasa, tukubaliane kuwa dialetic thinking ni aina ya tafakuri inanyosisitiza katika migongano ya hoja. Migongano ya hoja, maana yake, ni kukubali kuhitalafiana kama namna njema ya ufikwaji wa hitimisho sahihi.

Hebu na tuiangalie falsafa hii kwa mifano rahisi.

Ukweli unatokana na tofauti. –tofauti hapa ikimaanisha opposite. Labda tuseme kinyume. Ukweli unatokana na kinyume cha ukweli huo. Kwamba vinyume (opposites) kwa asili hutegemeana.
Hebu angalia: Unawezaje kulielewa giza kama huwezi kuuelewa mwanga? Huwezi kujua kwamba unapenda kama hujawahi kuchukia. Huwezi kuielewa furaha kama hujui huzuni ikoje. Utajiri hauna maana bila umasikini? Huwezi kuwa mwerevu kama hakuna wajinga wanaokuzunguka. Uhai hauwezekani ikiwa atakuwepo mwanamke bila mwanamme. Mifano ni mingi na hata wewe ndugu msomaji unaweza kukubalina nami kwamba vitu vyote tunavyovijua vina kinyume chake. We angalia. Kusini na Kaskazini. Hasi na chanya. Haki na hukumu. Kulia na kushoto. Mbingu/pepo na Jehanamu. Mungu na Shetani na kadhalika kadhalika.

Hivyo unaweza kuona, mwingiliano (interpenetration) uliopo baina ya pande mbili zilizo kinyume cha kila mmoja. Upande mmoja tofauti huweza kupatikana ndani ya upande mwingine ambao ni kinyume chake. Kwamba kwa sababu giza linaendana, ama kutofautiana na mwanga, basi maana yake lazima kuna mwanga kidogo katika kila giza, na vivyo hivyo kuna giza kidogo katika kila mwanga.

Kwa kadiri ya kanuni hii lazima kuna chuki kidogo katika kila upendo, Na kama tukitazama kila jambo kwa makini sana, basi hatukosi kuona kinyume chake ndani mwake.

Falsafa hii hutukumbusha kutazama mambo kwa kuangalia na kinyume chake pia. Kama tulivyokwisha kuona, kila jambo lina kinyume chake. Mtazamo huu hutujulisha kwamba thamani yoyote tuliyonayo, kama ikionekana kuwa thamani kama ilivyo kwa kuangalia upande mmoja tu, basi thamani hiyo huwa ni mkanganyiko. Kwa sababu hata kama tungejaribu kukwepa kuangalia kinyume chake, lakini kiukweli kinyume hicho lazima kitajijumuisha tu kwenye upande huo mmoja tunaoung’ang’ania. Na kama tutaendelea kukazania upande mmoja tu, kwa sababu ya labda tuseme, uzuri wake, basi, uzuri huo hugeuka kuwa kinyume cha kile tulichokuwa tunajaribu kukikwepa mwanzo.

Kwa hiyo, dhana hii itushawishi kutafakri na kinyume cha kila tunachofikiri. Tusirahisishe chochote kwa sababu yoyote. Kila wakati uliza swali hata katika jambo ambalo kila mmoja analiona kuwa “aah si ndivyo inavyokuwaga?!” mawazo ambayo yatakufanya ushindwe kuujua ulimwengu unamoishi kwa ufasaha. Tabia ya kukimbilia upande wa jambo unaonekana kuwa “mzuri” haiwezi kutusaidia sana kuwa watu wajuvi wa mambo.
Vitu kama imani zetu, tuelewe kwamba zinatuzuia sana sana kufahamu mambo. Imani zinatufundisha upande mmoja tu wa shilingi. Bila shaka, itakuwa ni ajabu kama ni mimi tu huwasikia waamini wakigoma kujifunza “vinyume” vya imani zao. Mshangao: Utajuaje ubora wa imani yako bila kuifananisha na uduni wa imani za wengine? Si utabaki ni shabiki?

Si bure kujaribu kuangalia “upande wa uani” wa imani zetu. Kushikilia kuwa “…hii ninayoiamini ndiyo kweli…” kutayabinya mawazo yako na kukuzuia kuelewa mambo. Kujielewa ninakokuzungumzia, ni pamoja na kudiriki kuangalia ule upande mwingine tunaoukwepaga. Huenda, ni kutokuujua huko, ndiko kunakokubinya usijielewe.

Maoni

 1. Ahsante sana bwana Bwaya kwa habari hii nzuri.

  Ingawa umeomba msaada BAKITA, lakini nimeona sina budi kusaidi kupendekeza neno linalofaa katika kutafsiri neno Dialectic thinking.
  baada ta kutafakari kwa kina makala yako nimeona neno "Fikra Mkabala" ndilo linalofaa zaidi katika kutafsiri neno hilo.
  Hata hivyo si vibaya iwapo wasomaji wengine watajitokeza na kuchangia.

  Nikija kwenye mada yako, maana hapo ndipo ulipogusa hisia zangu kiutambuzi, ningependa kuchangia japo kidogo.

  Kimsingi nakubaliana na wewe kwamba kila jambo lina kinyume chake, kwani bila kuwa na kinyume basi hilo jambo lisingekuwepo.

  Kwa hiyo kila jambo linakuwepo tu, pale linapokuwa na kinyume chake, na kama hakuna kinyume chake basi jambo hilo litakuwa ni la kufikirika.

  Umetoa mifano mingi sana, kwa hiyo sioni sababu ya kuongeza mfano wowote, ila lipo jambo moja hapa ambalo kwangu mimi naona lilikuwa ni la msingi zaidi katika mjumuisho wa mada yako.

  Nakubaliana na wewe kwamba ni vyema kujifunza pande mbili za kila jambo, kwa ajili ya kuwa wajuvi zaidi. lakini mimi naona kuna tatizo kidogo kuhusu hilo kutokana na mitazamo yetu katika kuayapima mambo, hasa kutokana na malezi yetu.

  Bwana Bwaya naamini utakubaliana na mimi kuwa katika malezi yetu, sisi tumefundishwa upande mbaya tu wa kila jambo na hata kutafsiri mambo huwa tunaangalia ule upande mbaya tu.

  Ni aghalabu sana kukuta mtu akijipongeza kwa kupata mafanikio japo kidogo katika mradi fulani ambao alitarajia mafanikio makubwa.

  Unaifahamu sababu?

  Sababu ni kwamba upande mbaya ndio uliotamalaki katika fikra zake, na kibaya zaidi ni kwamba upande huo mbaya hautatamalaki katika mazingira ya kujifunza, la hasha,
  utakuwa unazalisha mauamivu ya kihisia na majuto makubwa.

  Tumefundisha kuanglia upande mbaya si akwa kujifunza bali kwa kujilinganisha na wengine.
  Ndio maana uatakuta mtu amefanya mambo tisa mazuri yote yakawa yamefanikiwa, lakini likitokea la kumi likashindikana, basi hilo litachukuwa nafasi kubwa katika fikra kuliko yale tisa yaliyofanikiwa.

  Kwa hiyo basi tunatakiwa tuangalie upande wa pili katika kila jambo kwa kufikiri vizuri, kwani tukikaribisha fikra hasi ni kujiletea maumivu ya kihisia, tutakuwa tunajiumiza wenyewe.

  Ni hayo tu bwana Bwaya

  JibuFuta
 2. Mtambuzi,

  Nikushukuru sana kwa mchango wako mzuri, ulioshiba. Majumuisho uliyoyafanya, kwa hakika, ninayaunga mkono mia moja kwa mia moja.

  Ndio maana kuna umuhimu wa wasomaji kuacha maoni kwa lengo la kupanua mjadala. Kusoma na kuondoka, kunaturudisha kwenye enzi za magazetikongwe, kwamba alichokiandika mwandishi hakijadiliwi.

  Hata hivyo, najua kuna mada zinaleta utata hivyo watu wengi husita kushiriki mijadala. Na wengine huamua kushiriki kwa njia ya simu na barua pepe. Lakini kila inapofaa, nadhani, ni vizuri kujadiliana hata kama tofauti zitakuwa bayana. Tusiogope kutofautiana.

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Fumbo mfumbie mwerevu