Shule za "yeboyebo" na Mimba za utotoni

Ni ajabu na kweli. Baada ya kubaini kuwa karibu vijana wengi wanaotumia internet hapa Singida, lengo lao ni kujiridhisha na picha za ngono, kumbe lipo tatizo jingine. Mimba za utotoni. Sijafikia kuhalalisha uhusiano uliopo kati ya uangaliaji wa picha za ngono na hili la mimba. Lakini kwa mbali naanza kuhisi. Kwa sababu nimegundua pia kuwa mitaa mingi imesheheni sehemu za kuonyeshea filamu za "kikubwa" ambapo ndiko zilipo prepo za wanafunzi wengi wa shule za yeboyebo (kata).

Ukweli ni kwamba siku hizi kila mwanafunzi "anafaulu" kuingia sekondari. Maana tumetoka nyakati zile za kufaulu na bado ukakosa nafasi, mpaka nyakati hizi ambapo unafeli na bado unaambiwa umefaulu.

Pamoja na neema ya kufaulu, karibu kila familia ninayoitembelea hapa Singida inauguza maumivu ya binti kuzaa kabla ya wakati. Mabinti wa shule za msingi na sekondari wanapachikwa mimba (Mara nyingine na waalimu wao ambao wengi ni wale wa voda fasta). Wale walioshindwa kuendelea na masomo wanazalia nyumbani. Idadi ya familia zilizoathirika na tatizo la mimba inatisha. Makanisani pia hali si shwari. Vijana wengi wamesimamishwa "ushirika" kwa kile kinachoitwa kufunga ndoa ilhali msichana akiwa mjamzito. Yaani mke anajifungua miezi mitano tu baada ya kula kiapo cha utiifu madhabahuni. Kazi kweli kweli.

Nimejaribu kuongea na wazazi kadhaa kuhusu kadhia hii. Hata hivyo wazazi wengi wanabaki kuwalaumu watoto wenyewe. Ukiwauliza 'wazazi watoto', wao wanawalaumu wanaume watu wazima wanaowaowalaghai. Wengine wanawalaumu wazazi wao kwamba hawajihusishi na maisha yao.

Bado sijajua chanzo hasa cha tatizo hili. Itoshe kwa sasa kuilaani tabia hii. Kukatisha masmo kwa sababu ya mimba si jambo la kufurahisha. Kuharibu maisha kwa sababu ya haraka za ujanani si jambo zuri. Mtoto kulea mtoto mwenzio, haya hayawezi kuwa maendeleo kwa tafsiri yoyote ile.

Maoni

 1. duh ipo kazi hapo, yaani haya mambo suluhu yake nini? au shule/elimu? je elimu ya namna gani? topiki ngumu imenishinda mkuu.
  Hebu tumwite dada Koero amwage hoja zake hapa tunamhitaji sana kwa hili na mengineyo.
  kwaheri kwa leo

  JibuFuta
 2. Kaka Bwaya ahsante sana. Ahsante kwa kusema jambo hili.
  Chanzo?
  Chanzo sijui nini, labda mmomonyoko wa maadili katika jamii. Watu wazima wanawalaghai mabinti wa umri wa kuwazaa, pengine wajukuu kabisa.
  Mabinti nao wamekuwa hawashikiki. Tuseme hawaambiliki.
  Hizi internet cafe...
  Sote twajua.
  Tunasema maendeleo huja na mamboleo.
  Labda niwaulize swali waungwana, kiwango cha mimba za utotoni kabla ya haya maendeleo ya teknolojia kilikuwaje?

  JibuFuta
 3. Kaka Bwaya, swala la mimba za utotoni, linaonekana kuwa kubwa sasa hivi kutokana na huu utitiri wa vyombo vya habari, lakini naamini jambo hili limekuwepo kwa kitambo kirefu tu.
  Hivi ni nani asiyejua kwamba huko vijijini ndipo ambapo jambo hili limeshika kasi kubwa?
  hebu tembelea vijiji vilivyoko kando kando ya hizi barabara kuu, uone jinsi vibinti vinavyojiuza kwa hawa madereva na utingo wa malori makubwa yanayosafiri kwenda Congo, Rwanda na Burundi.
  Kaka Bwaya wewe juzi ulikuwa Singida hali hii unaifahamu. Pale singida ni mfano mmojawapo, watoto wengi sana wameathirika na hizi mimba za utotoni.
  Huku mijini nako ndio usiseme, zawadi za chipsi mayai, lifti za bure na vizawadi vidogo vidogo vimechangia sana hizi mimba za utotoni, mimi nimesoma hapa mjini nayafahamu haya, kwani nimesumbuliwa na ninaendelea kusumbuliwa sana na mibaba mizima yenye familia zao.

  Kingine ni malezi ya wazazi wetu, nayo yamekosa maadili, hakuna nidhamu kabisa kati ya wazazi na watoto. Luninga nayo ni jinamizi tunalolifuga majumbani mwetu, hizo inteneti ndio usiseme, wewe mwenyewe umekiri kushuhudia kule Singida.

  Ningesema mengi lakini ngoja niwaachie wenzangu nao wachangie.

  JibuFuta
 4. Walionitangulia wamesema yote, hasa dada Koero.
  Sina cha kuongeza.
  Heri ya Mwaka mpya.

  JibuFuta
 5. Umasikini unachangia sana tatizo hili la KINAMAMA WENYE UMRI MDOGO.Kama dada Kowero alivyotangulia kusema,wasichana wanadanganywa kwa vitu vidogo kama chipsi,soda,nk.Msichana ambaye alizoea kupata mlo mmoja kwa siku tena wa mkono mmoja inakuwa rahisi sana kudanganywa na kina FATAKI(wanaume watu wazima wasio na adabu).
  Maadili nayo yanachangia sana.Kuna wasichana wengine wanaotumia changamoto ya umasikini ktk kujilinda na kutokujiingiza ktk swala la mapenzi na kujiimarisha vizuri hasa kwenye masomo ili kuweza kukabiliana na hali hii ya umasikini.Mtizamo huu unawezekana kwa msichana mwenye maadili mazuri na anayejua nini maana ya maisha.
  Kuna wasichana ambao wanatoka ktk familia zenye uwezo mkubwa lakini bado wanaangukia ktk janga hili.Hapa tunaweza kugundua kuwa wakati mwingine umasikini sio sababu na swala la maadili inabidi lichukue nafasi yake.
  "hivi hawa wasichana wadogo huwa hawafahamu kuwa wanadanganywa kwa kupewa viza wadi vidogovidogo na huwa hawajui mwisho wa hivi vizawadi ni nini? Pengine labda hata wasipopewa vizawadi vidogovidogo kama njia ya ulaghai hukubali tu. Dada Koero nisaidie hapa.

  JibuFuta
 6. Kazi kweli kweli, tuseme ngono ni tamu au? Hapa ndipo huwa nashindwa kujua lililojema kati ya kujenga vyumba vya madarasa na kuwaweka wanafunzi ndani mwake. Hata wale walioolewa wanatolewa kwenye ndoa zao eti wakasome, wasome nini kama hamna nyenzo za kusoma?

  Ni bora wahitimuo la saba waolewe kama wanawachumba kuliko kwenda kuzaa watoto wasiokuwa na baba. Akili tupu ni sawa na shamba la shetani. Kama vibinti damu inachemka, harafu mnavipeleka vikakae na walimu wanaolingana umri na akili, unategemea nini sasa? Waneolewa wangeweza kulea familia zao vizuri badala ya kulanda landa.

  Naishia hapa

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Pay $900? I quit blogging

Fumbo mfumbie mwerevu