Taarifa ya Utafiti wa Ajira na Kipato ya mwaka 2012 , iliyotolewa na Idara ya Takwimu ya Taifa mwezi Julai 2013, inaonyesha kwamba nchi yetu ina waajiriwa rasmi 1,550,018. Kati yao, asilimia 64.2 wameajiriwa katika sekta binafsi na waliobaki (asilimia 35.8) wameajiriwa katika sekta ya umma. Aidha, taarifa inasema ni asilimia 24.8 pekee ya wafanyakazi hawa, wanapata kipato cha kuanzia Tsh 500,001 kwa mwezi [vipato vya wafanyakazi wengi (asilimia 54.4) ni chini ya Tsh 300,000 kwa mwezi.] Nafasi za kazi zisizojazwa Takwimu za taarifa hiyo zinathibitisha kwamba moja wapo ya changamoto zinazokabili soko la ajira hapa nchini, ni kukosekana kwa waajiriwa wanaokidhi matarajio ya ajira. Kwa mfano, wakati kwa mwaka 2011/12 zilikuwepo nafasi za kazi 126,073 nchini kote, ni wafanyakazi wapya 74,474 tu waliweza kuingia kwenye soko la ajira kwa kipindi hicho. Kadhalika, takwimu hizo hizo zinaonyesha kuwa nafasi za kazi zipatazo 45,388 hazikuweza kujazwa katika kipindi hicho. ...