Malezi yanayofanya mtoto amsikilize na kumwamini mzazi

TAFITI zinaonesha kwamba watoto wengi  ni 'mayatima' wenye wazazi tunaoishi lakini hatupo kwenye maisha yao. Wazazi tupo lakini hatuna muda wa kujua hisia zao, fadhaa zao, maoni yao, hofu zao na hata matumaini yao. Aidha, tafiti hizo hizo zinasema wazazi wengi tunatumia muda mwingi na watoto wetu ama kuwaonya, kuwakosoa ama kuwapa hotuba/maagizo ya ‘fanya hivi, acha hiki’ kuliko tunavyowasaidia kujenga mahusiano ya moja kwa moja kati yetu na watoto.

Wazazi kwa upande wetu, tunajitetea kwamba maisha yamekuwa na pilika nyingi. Mambo yamebadilika hivyo yatupasa kutumia muda mwingi kutafuta pesa kujenga maisha ya baadae watakayoishi watoto wetu. Tunawavalisha, tunawalisha, tunawapeleka shule na kuhakikisha wanalala na kuishi kwa usalama. Katika jitihada zote hizo tunajikuta tukikosa muda wa kutulia na kujenga maisha ya sasa ya kimahusiano na watoto wetu ambayo kwa kiasi kikubwa huathiri maisha na mahusiano yetu na watoto wetu hapo baadae.

‘Elimu ya kujitegemea’ inavyowaathiri watoto
Wazazi wengi tunasubiri watoto ‘wapate akili’ ili tuanze dozi rasmi ya mihadhara ya maagizo, maelekezo, makanyo, maonyo na kadhalika, tukiamini mtoto hujifunza kwa mafundisho rasmi. Wakati mwingine tunaamini fimbo ndilo jibu la tabia njema ya mtoto. Tunatumia na vifungu vya biblia, ‘Usimnyime mtoto mapigo/fimbo’. Na tunawachapa kweli tukitarajia heshima na adabu.

Athari za mtazamo huu ni kwamba katika kipindi muhimu kabisa cha mtoto kujifunza, tangu anazaliwa mpaka miaka mitano, hatuwekezi vya kutosha. Tuko bize tukisaka maisha na kuwatelekeza watoto kimahusiano. Wanapofikisha miaka mitano tunawapeleka boarding wakapate elimu bora ya kimataifa itakayowasaidia kuzungumza kiingereza na sio kuwa binadamu atakayeishi na wenzake vizuri.

Tunasahau kwamba kipindi tunachodhani mtoto hajifunzi, ukweli ni kwamba hicho ndicho kipindi sahihi na muhimu kujifunza kuliko kipindi kingine chochote cha maisha ya mtoto. Ndicho kipindi mtoto anapojenga taswira ya ilivyo dunia na wakazi wake, tabia na ubinadamu, imani na tunu nyingine za msingi katika maisha.

Ni kipindi nyeti ambacho mtoto huhitaji mahusiano ya karibu kabisa na mzazi, ambaye naye shauri ya pesa, hapatikani. Kutokupatikana katika kipindi hiki muhimu, kumsikiliza mtoto na kuingiza kile tunachopenda kukiingiza katika moyo wa mtoto, huongeza umbali wa kimahusiano baina ya mtoto na mzazi.

Na bahati mbaya, umbali huu wa kimahusiano kati ya mzazi na mtoto huongezeka kadri mtoto anavyopata akili. Hukua akiviamini na kuvitegemea vyanzo vingine vya maarifa zaidi ya mzazi. Bila hata mtoto mwenyewe kung’amua, taratibu huanza kukosa imani na wazazi ingawa hujitahidi kuwaridhisha akiogopa fimbo na kelele. Mtoto huanza kumwona mzazi kama mtu mwingine yeyote anayeweza kumpa chakula, mavazi na malazi isipokuwa faraja ya moyo.

Hapa ndipo wanetu huanza kujifunza zaidi kupitia televisheni, marafiki na watu wengine kama walimu wanaokabiliwa na msongo wa mawazo ambao wakati mwingine hupanda mambo tofauti kabisa na mtazamo na matakwa ya sisi wazazi. Yote haya hufanyika bila taarifa ya mzazi ambaye yuko bize kutafuta maisha ya mbeleni ya mwanae.

Mtoto huyu anapofikia umri wa kuanza kufanya mambo yake kwa uhuru kwa kutumia elimu hiyo aliyoipata kwa mfumo wa kujitegemea tangu amezaliwa , tena bila 'ukaguzi' wa mzazi, ndipo mzazi hukumbuka 'shuka asubuhi'. Huurejea wajibu wake na huanza jitihada za kutafuta/kulazimisha urafiki na mtoto wakati ambao mtoto hana haja na urafiki huo. Too late wanasema wazungu. Shughuli pekee inayoweza kufanyika kwa ufanisi katika kipindi hiki kizito ni kulalamika, kufoka na kuadhibu, mahusiano ambayo kwa hakika huongeza umbali wa mawasiliano baina ya mtoto na mzazi. Mzazi humwona mtoto ameasi, na mtoto humwona mzazi anajipendekeza na kumfuata fuata.

Tuyape malezi uzito unaostahili
Ili kukwepa fedheha ya kulazimisha urafiki na mtoto hapo baadae, tunashauriwa sisi kama wazazi tuyape malezi uzito unaostahili kuanzia pale tunapofikiria kupata mtoto. Na kwa kweli malezi ndiyo fursa pekee ya mtu kubadili maisha ya mtu mwingine vile apendavyo. Fursa hii huwezi kuipata hata kwa mwenzi/mpenzi wako maana katika mahusiano ya ukubwani kinachotokea zaidi ni kuchukuliana na sio kubadilishana tabia. Kwa hiyo kama kuna fursa pekee ya kubadili mtu katika dunia hii ni malezi. Tuitumie. 

Kupitia malezi mzazi anaweza kuwekeza apendavyo na kuumba tajiriba itakayoongoza mwelekeo wa maisha ya mtoto. Hata biblia imelieleza suala hili vizuri sana. Kwamba kile unachomfundisha mtoto kukifuata akiwa mdogo hatakiacha maisha yake yote. Kuwekeza katika ufahamu wa mtoto katika hatua za mwanzo kabisa za maisha yake huweka alama ya kudumu itakayoathiri mitazamo, imani na hata tabia ya mtoto katika maisha yake yote ya mbeleni. Tulitambue hili tunafukuzana na mipangilio ya kutafuta pesa.

Tupatikane kwa watoto, tuwasiliane na mioyo yao mapema
Hatuwezi kuwasiliana na moyo wa mtoto pasipo kupatikana. Kuwa nao, kucheza nao, kutembelea nao, kuzungumza nao na mambo yanayofanana na hayo huhakikisha tunaweka alama njema ya kudumu katika maisha ya mtoto. Kupatikana na kuwasiliana na moyo wa mtoto ni muhimu kuanze tangu anapozaliwa au hata anapohesabu majuma tumboni mwa mama.

Watoto wanaoishi kwenye kitongoji cha Mathare, Nairobi. Picha: @bwaya
Ingawa mfumo wa maisha ya sasa unatufanya tukose muda wa kuwa na mtoto mmoja moja kibinafsi na kuhusiana kwa karibu na moyo wake, bado huu ni wajibu wa msingi wa mzazi anayejitambua. Kwa kuelewa umuhimu wa mahusiano haya ya mwanzo, na kuchukulia malezi kwa uzito, tunaweza kabisa  kujenga utaratibu wa kuwa na muda maalum kwa siku wa kumsikiliza mtoto mmoja moja. Hili likifanyika tangu mtoto anapozaliwa, huongeza uwezekano wa sisi wazazi kuaminika kwa watoto na hivyo kuwa na nafasi ya kujua yaliyoujaa moyo wa mtoto na kuchukua hatua stahiki kungali ni mapema. Je, tunafanya hivi? Tunawapa watoto wetu muda wa kufurahia mahusiano na sisi wazazi 'kibinafsi'?

Fikiria jambo hili. Ukiweza kutumia saa 1 tu kwa wiki, sawa na dakika zisizofika kumi kwa siku kuzungumza kirafiki na mwanao mmoja mmoja, wakati anapofikisha umri wa miaka 12/13 anapopevuka na kuanza kujiona mtu mzima, utakuwa umekaa na mwanao kwa siku 27 tu! Fikiria. Wakati mtoto anaondoka nyumbani kwenda shule ya bweni akapate ufunguo wa maisha utakuwa umekaa nae kwa takribani mwezi mmoja tu! Miaka mingine yote ulimwacha akihusiana na televisheni na watu wengine usiowajua! 

Hivi kwa jinsi maisha yalivyobana namna hii, wazazi tunapata hata dakika hizo kumi kwa siku kukaa na wanetu na kuwasikiliza na kuwasiliana nao kirafiki ukiacha kuonya na kuadhibu? Wengine tunaishi Dar es Salaam kikazi, watoto wako kwa bibi yao! Si ajabu hatufanikiwi kuwa na influence yoyote kwa watoto. Wakianza kufanya vitu vyao, tunaishia kulalamika ‘watoto wa siku hizi wameharibika.'

Tuwe vile tunavyotaka watoto wawe
Mtoto hujifunza kwa kiasi kikubwa kupitia kile kinachofanywa na watu wake muhimu wanaomzunguka. Ni muhimu kufanya kile tunachotaka mtoto akifanye. Tuwe na tabia na imani tunazotaka kuzihamisha kwa mtoto. Mathalani, kama ninatamani mtoto awe msomaji wa vitabu, ni lazima nihakikishe ninajenga mazingira ya usomaji nyumbani kwa kuonesha mfano mimi mwenyewe. Mtoto anakua akijua maisha ni kusoma. Na sihitaji kumwandalia somo la ‘umuhimu wa kusoma vitabu’ ili ajenge tabia ya kusoma. Nafanya ninachotaka afanye. Aone nikifanya ibada kama ningependa awe mwombaji na yeye. Niwe na upendo kwake na mke wangu kama ninataka awe mtu wa upendo kwa watu. 

Kadhalika, nikitaka atukane wenzake na siku nyingine anitukane na mimi kimoyomoyo, niwe na tabia ya kumtukana yeye na kumwambia maneno magumu. Nikinywa pombe mbele yake maana yake ninamwandaa kunywa pombe ukubwani hata kama ‘sijamfundisha’ kwa maneno. Maana mtoto hujifunza kwa wepesi kupitia yale ninayoyafanya mimi kama mzazi. Vinginevyo, nitakuwa na bahati  ikiwa mwenendo wangu utamwuudhi kiasi cha kumfanya aamue kuasi tabia zangu. Na hapo si ni mpaka ajue ninachofanya hakifai kwa binadamu wa kawaida?
Tuwapende watoto, wajisikie kukubalika
Ninapompenda mtoto vile alivyo bila kujali alichokifanya ninamfanya aelewe maana ya upendo na aniamini. Simpendi ili nimdai tabia njema. Hapana. Nampenda hata anapokosea. Nampenda kwa sababu ni mwanangu apatie au akosee. Na wala si kumdekeza. Wakati mwingine tunakosea kama wazazi. Tunawapenda watoto kama malipo ya tabia njema. Na wakati mwingine hatufichi, tunawaambia waziwazi kuwa tutawapenda kama watafanya tulichowaagiza kukifanya. Tutawapa zawadi wakifanya vizuri. Conditions.
 
Wanapokosea tunaonesha kuwachukia na wakati mwingine tunawatenga kihisia. Tunawakomoa watoto, eti! Hatuadhibu tabia zao, tunawaadhibu wenyewe. Hali hii huwafanya watoto wawe wanyonge na wajione hawakubaliki kama watu na mioyo yao hujisikia kubebeshwa deni na mzigo wa kutekeleza msukumo wa nje wasioona mantiki yake. Hakuna binadamu wa kawaida hufurahia shinikizo la namna hii na kwa kweli huwa ni vigumu sana mtoto wa jinsi hii kufundishika. Adhabu zitaongeza usugu.

Ni kweli kuna nyakati watoto huwa watundu na mzazi hulazimika kumfokea na kumwadhibu badala ya kufikiria kumjengea mtoto tabia anayoitaka. Lakini ni vyema tukaelewa kwamba adhabu na mashinikizo yasiyotanguliwa na upendo na mazingira ya kujenga tabia njema hayana matokeo chanya katika maisha ya mtoto.

Kiboko cha kweli anachokihitaji mtoto kujenga tabia njema ni upendo. Na wala kumpenda mtoto si kumdekeza kama tunavyoamini wazazi wengi tulikulia mazingira yaliyotindikiwa upendo. Hatukulelewa kwa upendo, tunahamishia magonjwa yetu kwa watoto. Samahani. Nilitaka kusema upendo halisi hujenga mazingira ya kupanda tabia zinazofaa bila kusubiri kuadhibu tabia zisizofaa zilizotokana na kunyimwa upendo.

Tushughulike na msongo wa nafsi zetu kwanza
Kazi ya kulea inahitaji nafsi iliyotulia. Nafsi isiyotafuta amani kwa kuumiza wengine. Ninapokuwa mzazi mwenye nafsi iliyosongwa na matatizo siwezi kutekeleza ipasavyo jukumu nyeti la malezi yatakayomjenga mtoto anayejitambua, anayejiamini na atakayekabiliana na changamoto za maisha ya ukubwani. Nitajikuta nikimtumia mtoto kama dodoki la kufyoza ugonjwa unaoisumbua nafsi yangu. Nitakuwa mwepesi, pasipo mimi kujua, kusema maneno magumu yasiyolingana na umri wa mtoto. Nitajisikia kuridhika kumfanya mtoto alie na kukosa amani. Nitaadhibu na kukemea kuliko ninavyowajibika kujenga imani, mitazamo na tabia njema. 

Ni muhimu sisi kama wazazi kushughulika na matatizo ya nafasi zetu na kuhakikisha kwamba tunahusiana vyema na nafsi zetu ili tuweze kujitoa kuwalea watoto wetu katika njia iwapasayo. Tukishashughulika na nafasi zetu, kinachofuata ni kujiuliza, tungependa watoto wetu waweje watakapoanza kujitegemea kimaamuzi? Kitu gani tungependa kichipue kwenye mioyo yao kitakachoongoza maisha yao ya sasa nay a baadae? Maana upo ukweli kwamba malezi yanachangia kwa kiasi kikubwa tabia tunazoziishi ukubwani. Kama tunapenda kutumia fursa ya kuumba tabia njema kwa watoto wetu, hatuwezi kukwepa kufanya maamuzi ya kulichukulia suala hili la malezi kwa uzito unaostahili. Malezi si kazi inayoweza kufanywa na yeyote. Tuyape uzito unaostahili.

christianbwaya@gmail.com

Maoni

 1. Nimependa hili somo nitarudi tena hapa...kuna kitu nafikiria

  JibuFuta
 2. Yasinta karibu sana. Tafadhali tushirikishe unachokifikiri tujifunze pamoja.

  JibuFuta
 3. Kuna hili jambo ambali huwa linanitatiza sana haya maisha ya siku hizi...yaani ile tabia ya kula chakula pamoja si mnakumbuka mlio na umri wangu jinsi ilivyokuwa na ule ni muda mzuri sana kwa familia kupasana habari zote za maisha. Lakini siku hizi kila mtu anakula kwa wakati wake...Hivi kwa nini tunapoteza utamaduni wetu?

  JibuFuta
 4. Ni kweli kabisa dada Yasinta. Utamaduni wa familia kula pamoja mezani unasaidia sana kujenga mahusiano na values/tunu za pamoja baina ya wanafamilia. Mnacheka, mnabadilishana habari nyepesi nyepesi na hivyo inakuwa rahisi kujua yanayoendelea kwa kila mwanafamilia.

  Lakini sasa, Yasinta, wazazi hasa sie akina baba tutapata wapi muda wa kula na familia/watoto wakati tuko bize na kusaka maisha mpaka saa tatu/tano usiku? Baba anayerudi nyumbani watoto wakiwa wamelala, na wa kwanza kuondoka (watoto wakiwa usingizini) atapata wapi muda wa kula na watoto?

  Kadhalika, mambo kama kuzorota kwa mahusiano baina ya wazazi, mashinikizo ya kimaisha na hata kutokuyapa malezi uzito wake yanaathiri kwa kiasi kikubwa utamaduni huu muhimu katika kujenga mahusiano ya karibu kati ya wazazi na watoto wao.

  Baba mwenye tatizo na mke wake anaweza kujikuta akikwepa meza ya chakula, kwa kisingizio cha 'mambo mengi' wakati kiukweli yuko baa anaharibu akili na vichwa vinavyofanana nae. Tunahitaji kubadilika. Turudishe utamaduni huu unaopotea kwa kasi kubwa.

  JibuFuta
 5. Nimejifunza mengi kwa somo hili, bila shaka nimeongeza maarifa ya malezi bora.

  JibuFuta
 6. ASANTE,,,IMENISAIDIA

  JibuFuta
 7. Nimejifunza Mambo mengi hapa, kaka nashukuru inawezekana kwa namna moja au nyingne nimekua nikimjaza mwanangu sum kwa kumchapa viboko badala ya maelekezo na urafiki

  JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3