‘Hakuna uhusiano wa elimu ya mzazi na ubora wa malezi’ –watafitiIMEJENGEKA dhana kwamba kiwango kikubwa cha elimu anachokuwa nacho mzazi kinaamaanisha ubora na ufanisi wa malezi. Katika nchi za ki-Magharibi kwa mfano, ubora wa malezi kwa maana ya uelewa wa mahitaji ya kisaikolojia ya mtoto umekuwa ukihusishwa na elimu ya wazazi inayokwenda sambamba na uwajibikaji wa kimalezi. Hali inaonekana kuwa tofauti katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara. 
Tafiti zilizofanywa kwa nyakati tofauti katika nchi za Tanzania, Botswana, Naijeria na Lesotho zinaonesha kwamba hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya elimu, kipato wala mafanikio ya kimaisha ya wazazi na ubora wa malezi ya watoto wao. Badala yake, katika hali ya kushangaza,  wazazi wasio na elimu na wenye kazi zisizo na hadhi ndio wanaoonekana kuwajibika zaidi kuliko wenzao wenye elimu ya kuanzia Shahada na kuendelea.

Watoto nchini Naijeria wakifurahia kuwa pamoja. Picha: naijamayor.com
Aidha, tafiti hizo zinaonesha wakati wazazi wenye elimu kubwa hawapati/hawana muda wa kukaa na kuwasiliana na watoto wao ipasavyo, bado angalau hujitahidi kuweka mazingira ya kujifunzia nyumbani kwa maana ya vitabu, televisheni, na vifaa vingine vya michezo kwa watoto. Kwa upande mwingine, wazazi wasio na elimu wala kazi zenye hadhi, wameonekana kuwa na uhusiano na watoto, wakitumia muda mwingi kuwafunza watoto tabia zinazokubalika katika jamii zao.
 

Hata hivyo, wazazi hawa wameonekana kushindwa kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia majumbani kwao kama wenzao wenye elimu.

Mazingira ya nyumbani
Watafiti karibu wote niliowataja mwisho wa makala haya wanakubaliana kwamba bila kuzingatia elimu wala kipato cha mzazi, mazingira ya nyumbani pamoja na mitazamo ya wazazi ndiyo hasa huathiri makuzi na malezi ya watoto. Wakati mazingira ya nyumbani yakimaanisha hali ya upendo unaooneshwa na wazazi kwa watoto, mahusiano ya wazazi wenyewe, mienendo ya wazazi, muda wanaoutumia  wazazi nyumbani na upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia; mitazamo ya wazazi kwa upande mwingine ni matarajio ya wazazi kwa watoto wao, jitihada za kuelewa na kujibu mahitaji ya kihisia ya mtoto, namna ya kuwapa moyo na hata kuwaadhibu watoto. 

Hata hivyo, matokeo ya tafiti hizo yanaonesha kwamba wazazi wengi wa Afrika huanza kujali, kufuatilia, kuelekeza na kuingilia shughuli za watoto wao wanapofikia kipindi cha kubalehe. Sababu kubwa inayotajwa ni kwamba katika kipindi hiki ndipo watoto huanza kuonesha tabia zisizowapendeza wazazi, ambazo kimsingi huwa ni matokeo ya kupuuzwa kwa mahitaji ya kihisia tangu awali. Kabla ya hapo, wazazi bila kujali elimu huamini hapana haja kubwa ya kuweka nguvu katika kujenga tabia ya mtoto.

Maana ya matokeo haya kwa wazazi
Barani Afrika, elimu ya darasani hamsaidii mtu kuwa mzazi bora wala kutokuwa nayo hamkufanyi mzazi kutimiza wajibu wake. Kinachoonekana ni kwamba ongozeko la elimu linaenda sambamba na ongezeko la majukumu mengine ambayo wazazi hujikuta wakiyapa uzito kuliko malezi. Kwa upande mwingine, kutokuwa na majukumu hayo huwa faida kwa mtoto ingawa changamoto inabaki kuwa uelewa sahihi wa mahitaji ya mtoto.

Inavyoonekana, mabadiliko ya kijamii na kiuchumi tunayoyashuhudia katika nchi zetu hizi, yanaleta changamoto mpya katika malezi. Wakati mzazi msomi akiathirika kwa kutoa muda wake katika kukabiliana na changamoto hizi nje ya familia, mzazi asiye na msomi naye anapambana na changamoto hizi hapo hapo nyumbani kwa namna yake.  Kwa namna moja au nyingine, aina za kazi tunazofanya kama wazazi, mitazamo yetu na changamoto nyinginezo huathiri namna tunavyojishughulisha na makuzi ya mtoto kihisia. 

Pengine ni wakati muafaka sisi kama wazazi na walezi kuanza kujenga utamaduni wa kuelewa hatua muhimu za ukuaji wa mtoto ili kutambua mahitaji na matatizo ya watoto tangu mtoto anapozaliwa. 

Kiungo cha tafiti na watafitiwa?
Zimefanyika tafiti nyingi sana kuhusu mahitaji na matatizo ya watoto barani Afrika. Kwa nini tafiti hizi haziwafikii walengwa? Sababu moja kubwa ni kwamba tafiti nyingi hulenga kukuza maarifa ya kitaaluma pekee.  Hufanywa kwa minajili ya watafiti kuwasiliana wao kwa wao na sio kutumika moja kwa moja katika kutatua matatizo halisi. Hii ndiyo sababu matokeo mengi huishia kupamba makabati ya maktaba za taasisi za elimu bila kufahamika kwa umma.

Pamoja na changamoto nyingi, blogu hii inalenga kuwa kiungo kati ya maktaba hizo na wazazi. Kwa majuma kadhaa tutafanya mapitio ya mahitaji ya msingi ya kisaikolojia katika vipindi mbalimbali vya umri wa mtoto tangu kuzaliwa mpaka miaka 20 kwa mgawanyo ufuatao: miaka 0 – 3, 3 – 6, 6 – 12 na 12 – 20. Lengo si kumwelekeza wala kumshauri yeyote nini cha kufanya, bali kujaribu kueneza maarifa yanayopatikana lakini hayafiki yanakostahili kufika. 

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa maandiko, tafnifu na vitabu vya watafiti wafuatao: A. Blair, I. Omari, T, Mwamwenda, D. Mbilinyi, A. Mbise, A. Oyewole na C. Nyinamuntu ambao wote wana kauli katika elimu ya makuzi na malezi ya mtoto.

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mbinu za Kumfundisha Mtoto Kusoma Akiwa Nyumbani

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Fumbo mfumbie mwerevu

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)