Kwa nini ni rahisi kumsifia mtu akifa kuliko akiwa hai?

Hatupendi kuwasifu wengine wala kusikia wakisifiwa na wengine, lakini ni wepesi sana kumsifia marehemu. Na ni nadra kusikia tabia ya marehemu ikikosolewa. Hata waliokuwa hawamsifii akiwa hai, huomba fursa ya kuusemea vizuri wasifu wa mpendwa aliyetutoka.

Mtu fulani maarufu akifa, kwa mfano, watu ambao hata siku moja hawakuwahi kumsema marehemu enzi za uhai wake, ndio huanza kushindana kutundika picha zake zikiambatana na maneno ya ‘apumzike kwa amani’. Sasa swali, kwa nini ni vyepesi kumsifia marehemu asiyesikia kuliko kumsifia binadamu anayesikia?


NIKUSIMULIE visa viwili vya kweli. Wakati fulani nikisoma, nilipata bahati ya kusifiwa sana na mwalimu wangu. Alisifu kazi yangu mbele ya wanafunzi wenzangu. Na kipindi hicho ilianza kuwa kama kawaida fulani hivi kusifiwa na karibu kila mwalimu wangu aliyenifundisha. Kama umewahi kusifiwa na watu unaowaheshimu lazima utakuwa unaelewa. Kusifiwa raha sana. Lakni kabla hatujaendelea, nidokeze kwamba aya hiyo inaweza kuwasumbua baadhi ya wasomaji. Wengine watajiuliza, 'Ona sasa. Kulikuwa na sababu ya kujisifia hapa?!” Hii ni kawaida ya wanadamu wengi tunapowasikia wenzetu wakisema vijitukio chanya vilivyowahi kuwatokea.

Tuendelee na kisa chetu. Baada ya mwalimu kusema, “Nimevutiwa sana na hii kazi…mwombeni Christian muone alifanyaje,” jamaa mmoja akashindwa kujizuia. Akaona hii sasa ishakuwa too much. Kwa kile kilichoonekana kuwa ghadhabu na  kukerwa na kitendo cha mimi kusifiwa sifiwa, akaamua kumpasha Profesa, “Tutaigaje kazi ya Christian wakati ulisema amekosea pale kwenye nanihii? Tuelekeze mwenyewe!” Hakuja hata mmoja kuuliza nimefanyaje kazi isipokuwa rafiki zangu wawili. Unaweza kuona namna mwanadamu anavyokerwa na sifa zisizomhusu. 

Kisa cha pili, ni kule kule shule. Yametoka matokeo ya kazi za darasani wakati tunajiandaa na mtihani wa mwisho. Yamebandikwa ubaoni mahali kila mmoja anaweza kuona. Sasa mimi niko Maktaba najifanya kusoma nimetumwa na kijiji. Wao wanaita ‘kukata madesa’. Nashangaa napata jumbe wa simu kutoka kwa wanadarasa kadhaa ambao sina mazoea nao sana, ‘Vipi umeona kozi weki?’ Sikuvumilia. Nikaenda kuangalia. Nilinyong’onyea. Nilikuwa wa mwisho kasoro watu watatu. Alama 27, wa kwanza ana 40, wa mwisho ana 26.

‘Si ungekuwa hata wa mwisho kabisa?’ unajisemea mwenyewe kwa jinsi ulivyofurahi. Habari mbaya kwa wengine huwa habari njema kwa wengi wetu. Ndicho kilichotokea kwa baadhi ya wanafunzi wenzangu,“Sifa zote zile?...pole sana kaka.” Huku nikiwa najisikia aibu kushika mkia, jamaa mmoja akaamua kuwa mkweli wa hisia zake za furaha, “Hili somo safari hii lazima watu kadhaa washikwe.” Hao kadhaa ni pamoja na Christian. Bahati nzuri kama alivyosema Samweli Sitta dua la kuku halimpati mwewe. Nilinusurika kwenye tundu la sindano. 

Nilichotaka kukisema umekielewa. Mwanadamu wa kawaida hapendi kusikia mshindani wake akifanikiwa. Na yeye mwenyewe hayuko tayari kumsifia wala kumpongeza mtu anayemwona kuwa ni mshindani wake. Maisha haya bwana!

Kutokuwasifia watu
Pamoja na na tabia ya kutokupenda kusikia wengine wakisifiwa, mwanadamu huwa ni wepesi sana kumsifia marehemu. Na ni nadra kusikia tabia ya marehemu ikikosolewa. Hata waliokuwa hawamsifii akiwa hai, huomba fursa ya kuusemea vizuri wasifu wa mpendwa aliyetutoka. Wakati mwingine unaweza kuona matukio dhahiri kwenye mitandao ya kijamii. Mtu fulani maarufu akifa, watu ambao hata siku moja hawakuwahi kumsema marehemu enzi za uhai wake, ndio huanza kushindana kutundika picha zake zikiambatana na maneno ya ‘apumzike kwa amani’.
Sasa utashangaa, kwa nini ni vyepesi kumsifia marehemu asiyesikia kuliko kumsifia binadamu anayesikia?

Kwanza kabisa, usiniambie ni hofu ya kifo wala maombolezo. Kwamba kwa kumswalia vizuri marehemu basi watu wanaamini watapata baraka? Labda ni hofu, uchungu na mazoea. Lakini kwa nini hata mwanamuziki fulani 'akipumzika kwa amani' vituo vya redio na televisheni huanza kumpa 'airtime' ya bure nyimbo zake zisikike? Kwa nini hawafanyi hivyo akiwa hai? Kwa nini akifa mtu kila mtu anatamani kunukuu maneno ya marehemu hata kama hakuwa kufanya hivyo enzi za uhai wake? Nataka kueleza kwa nini msukumo wa sifa za marehemu ni kwa sababu ya kunajua hasikii na wala hatanufaika na sifa tunazompa. Nitafafanua.

Ujue kwa asili mwanadamu ni mtu wa mashindano. Hili huwa ni nadra kwetu kulikiri. Tunashindana na hata wasioshindana na sisi. Tunazaliwa na shauku ya kuwazidi wengine. Kuwa juu ndio ugonjwa wa nafsi ya mwanadamu aliyetokana na Adamu na Hawa. Ugonjw auhuo ndio unarahisi kazi ya kumkosoa mtu na kumfanya ajisikie vibaya kuliko kumsifia mtu huyo huyo ajisikie vizuri. 

Ndivyo ilivyokuwa nilipojaribu kuanza makala hii kwa kujisifia. Kama wewe ni kama watu wengine huenda hata ulifyonza kwa kisa ambacho huenda ni cha kutunga. Lakini nilipokwambia ‘nilishika mkia’, huenda hadi pumzi zilikurudia. Well, natania. Lakini ukweli ni kuwa tunakerwa na lolote linaloonekana kuwa mafanikio kwa wengine wakati huo huo tukivutiwa na lolote linaloonekana kuwa kushindwa kwa wengine. Huwa hatusemi wazi lakini ndani ya mioyo ya wanadamu wengi ndivyo ilivyo. Mashindano.

Shauri ya tabia hii ya kupenda kuwazidi wengine, hatupendi kusema mema yao hali wakisikia. Hatupendi kuwapongeza kwa dhati wakisikia. Tunaogopa wakiwa na furaha sisi tutajisikia kuadhibiwa mioyoni. Tunajisikia embarrassment kuwafanya washindani wetu wajisikie vizuri. Na kwa mtiririko huo huo, utaona namna kuwakosoa na kuwaonesha wengine kuwa hawawezi ni njia ya nyepesi ya kuwafanya wajisikie/waonekane vibaya. Maana tunafurahi kuona washindani wetu wakijisikia kuadhibiwa. 

Vipi tunaposifu wengine?
Wakati tunakwepa kuwafanya wengine wajisikie ‘wako juu,’ mara nyingi sana tunapenda sisi wenyewe tuwe juu. Tunajisikia vizuri sana kusifiwa au kujisifu. Na wakati mwingine tunawasifu wale ambao tunajua tuna maslahi nao. Marafiki. Ndugu. Wakubwa na kadhalika. Sifa zinakuwa rushwa ya kuweka mazingira ya kunufaika. Si rahisi kwa mfano, mkubwa wako kazini kukusifu wewe mbele za watu hivi hivi tu kuliko wewe kumsifia yeye. Unatumia hulka ya mwanadamu kupenda sifa kujiwekea mazingira ya kupata unachokitaka. 

Kwa wale tusio na maslahi nao na wasiotuhusu, mara nyingi hatupendi kuwasifia wasikie kwa masikio yao. Tunapolazimika kufanya hivyo, mara nyingi ni ama kwa hofu ya ‘nitaonekanaje’ kwa maana ya kulinda kutokuonekana muungwana au kwa kujua kabisa kufanya hivyo hakutuathiri kwa vyovyote.

Ndio maana hutashangaa kuona hotuba za hadharani kuwaaga, kuwaenzi au kuwatambua watu fulani hujaa sifa. Sababu? Tunafanya hivyo kwa sababu kufanya kinyume hadharani ni hasara kwetu. Hatupendi kuonekana watu wa ajabu mbele za watu hata kama ndani kabisa ya nafsi tunaweza kuwa tunasema kinyume na tunachotaka watu wasikie. Nia ni ile ile, ‘Nionekane mtu mwenye hekima,’ maana yake napambana kujiweka kwenye nafasi ya juu.

Sasa unaweza kuelewa kwa nini kumsifu marehemu asiyesikia ni rahisi na kila mmoja wetu anaweza kufanya hivyo. Kwanza, sifa kwa marehemu hazitutishi sisi tulio hai kwa sababu tunajua hana uwezo wa kujisikia vizuri hali ambayo wengi hatuipendi. Na pili, hatumkosoi kwa sababu tunajua hana uwezo wa kujisikia vibaya hali ambayo mara nyingi tunatamani itokee kama tulivyoona. Tatu, tunaogopa kushusha hadhi zetu kwa kumsemea vibaya marehemu hata kama tunajua alikuwa jambazi lililosumbua mtaani. Hofu ya kuonekana watu wa ajabu ndiyo ile nia tuliyokwisha izungumza ya kuhakikisha heshima zetu zinabaki juu.

Pengine marehemu angekuwa ana uwezo wa kusikia, hotuba za kumkumbuka zingeweza kufanyiwa marekebisho ya ‘kumpasha vidonge vyake’ anapokwenda kumpumzika kwa amani. Sababu? Ugonjwa wa nafsi.

Upo uwezekano wa kubadilika?
Ndio. Hatua ya kwanza ni kuhakikisha nafsi yako inapona kwa kujizoeza kuwafurahia mafanikio ya wengine. Maana nafsi iliyopona haitishwi na furaha wala mafanikio ya wengine. Nafsi iliyopona haifurahii uchungu wa wengine. Uponyaji wa nafsi unakuwezesha kufurahi na anayefurahi hata kama huna maslahi naye na kuhuzunika na wanaohuzunika hata kama huna maslahi nao.

Ukitaka kujua kujua hali ya nafsi yako chunguza unavyohusiana na watu. Je, uko tayari kumsikiliza mtu akijisifu bila kuumia ndani? Je, huna njaa ya kusema mafanikio yako unapokuwa na watu? Je, hujisikii vibaya kuona mwenzako amefanikiwa? Vipi unaposikia mtu uliyegombana naye mathalani, amepatwa na mabaya? Unaumia au unajisikia amani kwamba hatimaye yamemkuta? 

Je, uko tayari kusema ukweli hata kama kwa kuusema vile ulivyo utakufanya uonekane mtu dhaifu/dhalili? Je, unao uwezo wa kuwaambia watu mapungufu yao hata kama itakugharimu kufanya hivyo? Je, unaweza kuwatetea watu wasiokuwepo hata kama kwa kufanya hivyo hupati faida yoyote? Uko tayari kuchukua hatua ya kukiri makosa yako kwa wengine?

Nafsi yako ikipona, si tu utaweza kuwasema watu vyema bila kujisikia vibaya wakifurahi, lakini pia utaweza kutoa hotuba ya kusema madhaifu ya marehemu hadharani hata kama kwa kufanya hivyo utaonekana mtu wa ajabu. Very confusing eh? Hapana. Fikiria, kwa nini waombolezaji wengi wanaojua marehemu amefariki kwa maradhi ya UKIMWI huwa hawasemi? Moja, wanamnyanyapaa. Pili, hawajiamini. Tatu, nimeyasema haya ili tujitafakari na kubadilika.
christianbwaya [at] gmail [dot] com

Picha iliyotumika ulitumiwa awali na Brian Rubin wa blogu ya spacegamejunkie.com

Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Pay $900? I quit blogging