Wanafunzi waonyesha namna teknolojia rahisi inavyoweza kurahisisha upigaji kura bila kufika kituoni

NIMEFIKA hapa Diamond Jubilee kama mwananchi anayetamani kujionea hamasa waliyonayo wanasayansi chipukizi kuonyesha kazi zao nzuri. Ni maonyesho ya tatu ya Sayansi katika ukumbi wa Diamond Jubilee ambayo hatimaye hapo kesho yatawaibua wanafunzi wawili kama washindi wa tatu wa shindano la wanasayansi chipukizi hapa nchini linaloandaliwa na Young Scientists Tanzania.

Baadhi ya washiriki kwenye ufunguzi wa maonyesho leo. Picha: @bwaya
Kwa hakika hamasa ni kubwa. Wanafunzi wamejawa na msisimko wa aina yake kuonyesha matokeo ya tafiti zao walizozifanya tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Wamejawa na matumaini, hasa kwa sababu ya maneno ya ufunguzi yaliyosemwa na Mkurugenzi wa YST, Dk Kamugisha wakati akiwakaribisha asubuhi ya leo.

"Tulipata maombi ya kushiriki kutoka shule zaidi ya 200...lakini ni maombi 100 pekee yalifanikiwa kupenya katika mchujo. Mpaka hapo ninyi ni washindi. Kilicho muhimu zaidi, ni kwamba pamoja na kwamba kazi zenu zitapitiwa na watu wanaoelewa vyema zaidi maeneo hayo mliyoyashughulikia, napenda kuwahakikishia kwamba, hawajui mlichokifanya. Tunaweza kusema, katika hayo mliyoyafanya, ninyi ndio wajuzi mtakaowaeleza wasichokijua. Tumieni fursa hiyo", aliwahakikishia wanafunzi na walimu wapatao 300 kutoka mikoa 20 nchini.

Katika vingi vilivyonisisimua asubuhi hii, ni teknolojia waliyokuja nayo wanafunzi wa Shule ya Sekondari St. Jude iliyoko mkoani Arusha, Ntekaniwa Mramba na Hashim Nyasuro.

Wanafunzi hawa wamekuja na mfumo rahisi wa upigaji kura kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno (SMS). Kinachofanyika, ni kwamba, mpiga kura anatumia simu yake ya mkononi kutuma jina au namba inayomwakilisha mgombea wake kwenda kwenye namba ya msimamizi wa uchaguzi au kura ya maoni. Kisha mfumo huo unasajili kura yake na kujumlisha na kura zilizopigwa tayari na kutoa idadi kamili ya kura alizopata mgombea huyo kwa wakati huo.

Maana yake ni kwamba kadri muda unavyokwenda, wapiga kura wanaweza kujua kura anazoendelea kuzipata mgombea husika kwa kulinganisha na wagombea wengine.

Wanafunzi hawa wanasema wameamua kutumia mfumo huu kwa sababu, kwanza, hauhitaji teknolojia kubwa na pili kutokana na ukweli kwamba hivi sasa simu ni kifaa rahisi zaidi kumilikiwa na wapiga kura wengi.

Wanafunzi Ntakaniwa Mramba na Hashim Nyasuro. Picha: @bwaya
"Mshiriki wa uchaguzi au kura ya maoni anahitaji kuwa na simu ya mkononi tu. Sana sana aweze tu  kujua namba anayotakiwa kuitumia kwa ajili ya kutuma jina au namba inayomwakilisha mgombea wake" anasema Ntekaniwa Mramba huku akionyesha majaribio kadhaa ya namna watu waliokuwepo wanavyoweza kupendekeza onyesho bora zaidi kwa mwaka huu kwenda kwenye namba ya simu aliyokuwa ameionyesha.

Nawauliza ilikuwaje wakapata wazo hili? Hashim Nyasuro anasema kwa Kiingereza safi, "Shuleni tunajifunza somo la kompyuta na program zake. Tulipata wazo hili baada ya kusikia taarifa za watu wengi kushindwa kujitokeza kupiga kura shauri ya kutokuwa na muda wa kupanga foleni kusubiri kupiga kura...hiyo mara nyingine ikimaanisha watu hawana muda wa kupiga kura hata kama huenda wanataka kufanya hivyo...lakini vile vile kuna ucheleweshaji wa matokeo ya uchaguzi...hivyo tukaamua kutumia open source (zana huria) kujaribu kutatua tatizo hili."

Akieleza maana ya teknolojia hiyo katika jamii yetu, wanasayansi hawa chipukizi wanasema, "Zana hii ikitumika na kuboreshwa vizuri inaweza kutatua tatizo la watu kushindwa kujitokeza kupiga kura, kwa sababu mpiga kura hujitokeza siku ya uchaguzi kwa njia ya SMS pekee...hahitaji kujitokeza kimwili...lakini pia itarahisisha utangazaji wa matokeo".

Je, hakuna uwezekano wa mtu kupiga kura zaidi ya mara moja? Ntekaniwa Mramba anasema, "Haiwezekani. Mfumo huu hauruhusu mtu kupiga kura zaidi ya mara moja...ukishajisali (kujiandikisha) kwa kutuma namba yako kwa wasimamizi wa uchaguzi...namba hiyo inaruhusiwa kupiga kura mara moja tu. Sema tu changamoto ni kwamba kuna uwezekano wa mpiga kura kubadili chaguo lake la awali, lakini kamwe hawezi kuzidisha idadi ya kura."

Huo ni mfano mmoja wapo wa shughuli za kiutafiti zinazofanywa na wanafunzi wa sekondari kwa hamasa iliyoanzishwa na Young Scientists Tanzania. Nyingine nilizokutana nazo ni pamoja na:

Wanasayansi chikupikizi wakielezea utafiti wao kwa Jaji. Picha: @bwaya
"Namna mbadala ya kuacha uvutaji wa sigara kwa watu" inayowasilishwa na Barbaba Mziray na Aggrey Boniface wa Sekondari ya St Amedeus, mkoani Kilimanjaro.

"Kukabiliana na upungufu wa maji katika eneo la Umasaini kwa kutumia maji machafu" iliyofanywa na Michael Laurent na Robin Damas wa Sekondari ya Ilboru Arusha.

"Kwa namna gani uvumbuzi wa gesi asilia unavyoathiri maendeleo ya kiuchumi mkoani Mtwara" iliyoandikwa na Mwahija Hassan na Muzna Juma wa Umoja Sekondari, Mtwara.

"Uchambuzi wa mashambulio ya tindikali ya mara kwa mara Zanzibar" inayowasilishwa na Salha Jumbe Said na Maryam Khatib Mohamed kutoka Shule ya Haile Selassie.    Na nyingizo nyingi zinazofikia 100.

Maonyesho haya ya Young Scientists Tanzania yanaendelea katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, na yatafikia kilele chake kesho mchana ambapo washindi watatu kwa kila makundi yafuatayo watafahamika:
  • Baolojia na Sayansi ya Ekolojia (inayodhaminiwa na LearnIT)
  • Sayansi Asilia, kemia na Hisabati (inayodhaminiwa na COSTECH)
  • Sayansi ya Jamii na Tabia (inayodhaminiwa na Concern Worldwide)
  • Teknolojia (inayodhaminiwa na Karimjee Jivanjee Foundation).
Pamoja na hao, watakuwepo washindi wawili wa jumla, ambao wote hupatikana kwa kupitia usaili unaofanywa na joto la wataalam katika maeneo hayo manne.

Mashindano hayo hufanyika kila mwaka kati ya mwezi Agosti na Septemba yakiwashirikisha wanafunzi kutoka nchi nzima, mwaka huu yakiwa yamepata udhamini mkubwa wa BG Tanzania na Irish Aid.

Twitter: @bwaya

Maoni

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mbinu za Kumfundisha Mtoto Kusoma Akiwa Nyumbani

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3

Fumbo mfumbie mwerevu

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)