Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -2

Tuliona katika makala iliyopita maana ya saikolojia na kuhitimisha kwamba kinachotazamwa zaidi katika saikolojia ni tabia. Kwa hakika matatizo mengi yanayoikabili jamii yetu chanzo chake ni tabia. Tabia ndio chanzo cha matendo tunayoyaona kama kukosekana kwa uaminifu, ubadhilifu wa mali za umma, ufisadi, migogoro ya ndoa, misuguano ya kijamii, chuki, upendo, ugaidi, unyanyapaa, ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kidini, changamoto za kimalezi na kadhalika. Yote haya yanaweza kuchambuliwa na kupatiwa majibu yake kwa kutumia sayansi ya tabia (saikolojia). Katika makala haya nitatoa mifano mifano kadhaa kuonesha namna sayansi ya tabia, inavyoweza kutumika kutatua matatizo yanayoikabili jamii.

Elimu na Kujifunza

Katika elimu, saikolojia hutumika katika kubaini mahitaji halisi ya mtoto kiufahamu, kijamii, kihisia na kimwili kulingana na umri wake. Kwa kuyaelewa hayo inakuwa nyepesi kuunda mtaala unaokidhi mahitaji hayo kwa ufasaha. Hili limekuwa likifanyika kwa kutumia saikolojia ya elimu katika mafunzo ya ualimu na elimu. Changamoto kubwa imekuwa ni namna walimu wanavyoweza kutafsiri malengo mapana ya mtaala katika kujibu mahitaji halisi ya mtoto.

Kupitia sayansi ya tabia, tunaweza kuelewa namna mwanadamu anavyojifunza, kuelewa na hata kutumia anachokielewa katika kuyaelewa na kuyafanya mazingira yake kuwa bora zaidi. Namna gani mtoto hujifunza lugha, na athari za lugha hiyo katika uelewa wake ni mambo ambayo kupitia saikolojia tunaweza kuyaelewa vizuri.

Mahusiano na Unasihi

Kijamii, matatizo ya kimahusiano baina ya watu yanayosababishwa na tofauti za kimtazamo, itikadi, imani na kadhalika yanaweza kuchambuliwa na kutatuliwa kwa kutumia saikolojia. Ilivyo ni kwamba zinapotokea hitilafu za kimahusiano, watu wengi hushindwa kuyatazama mambo kwa macho yasiyo ya upendeleo. Na kwa kawaida watu hukwepa kubeba lawama yanapotokea matatizo na kufanya juhudi za kuwafanya wengine wawajibikie matatizo ambayo wakati mwingine wameyasababisha wao.

Hapa ndipo, washauri nasaha, kwa kutumia saikolojia, wanapoweza kuwa msaada kwa kuwasaidia watu hawa kuelewa mzizi wa matatizo yao na hivyo kukabiliana vyema zaidi na matatizo hayo. Kazi ya mshauri nasaha si kutoa majibu, bali kutumia taarifa anazotoa mwenye tatizo ili kumsaidia kutambua kiini halisi cha tatizo ambalo mara nyingi hufunikwa na dalili tu zisizo tatizo halisi. Hivi ndivyo matatizo kama ya msongo wa mawazo, hasira, chuki, unyanyapaa, ubaguzi wa rangi, na mengineyo yanavyoweza kushughulikiwa kwa ushirikiano na washauri nasaha.

Kubadili Mitazamo na Tabia

Kadhalika, kupitia kanuni za saikolojia, programu endelevu za kijamii za kubadili tabia na mitazamo ya watu inayowakwaza katika kuishi maisha yenye ufanisi zinaweza kufanyika ili kuondoa au kupunguza matatizo ya kiafya, kijamii na kiimani. Kwa hakika, kuelewa jambo hakutoshi kubadili tabia ya mtu. Ni lazima zifanyike jitihada za kugeuza mitazamo ili kuweza kubadili tabia za watu.

Malezi na Makuzi ya Mtoto

Ni wazi kwamba wazazi wanakabiliwa na changamoto mpya za kimalezi zinazosababishwa na mabadiliko ya kijamii yanayoendelea. Malezi ya enzi za sasa hayafanani na yale ya miaka ya 90. Ni kweli kuwa kadri mtoto anavyokua kiumri, anakutana na changamoto nyingi ambazo ni vigumu kuzishughulikia  kikamilifu pasipo elimu ya saikolojia ya makuzi. Kwa kupitia elimu hii tunaweza kuwasaidia wazazi kuelewa kwa upana namna njema ya kujibu mahitaji ya watoto wao katika mazingira yanayobadilika kwa kasi na hivyo kuwafanya wakue wakiwa raia wenye mitazamo chanya kwa maisha yao wenyewe na watu wanaowazunguka.

Kuwezesha Ushawishi kwa Wengine

Lipo pia suala la uongozi. Namna gani wanasiasa au viongozi wengine wanaweza kuwashawishi wananchi au watu wanaowaongoza kukubali mawazo yao wakati huo huo wakidhibiti mawazo ya watu wanaofikiri kinyume nao, panahitajika kanuni za saikolojia. Falsafa, mitazamo na imani za kisiasa zinaweza kuwaingia ipasavyo wafuasi wa wanasiasa, na kuwafanya wajipambanue na makundi yao ya kisiasa, kwa kutumia kanuni za kisaikolojia.

Kujua Mahitaji ya Wateja/Wadau

Sambamba na hilo, katika biashara na ofisini, unafanyaje kuongeza ari ya wafanyakazi ili waweze kufanya kazi pasipo kusukumwa hata kama huwalipi fedha za kutosha au kama mfanyabiashara anafanya kipi ili kuwavutia wateja kupenda bidhaa yake kupitia matangazo, katika mazingira ambayo biashara ni ushindani, unahitaji ushauri wa kisaikolojia. Unapoona tangazo linalomwonyesha mtu maarufu akitangaza bidhaa fulani, hayo ni matumizi ya saikolojia. Namna gani matangazo yanayolenga kubadili tabia za watu yanavyoweza kuandaliwa, nayo ni kazi ya saikolojia.

Mkanganyiko

Katika kuhitimisha  tunaweza kusema ni kweli kwamba saikolojia ni maisha ya kawaida. Huwezi kuhusiana na mtu bila kutumia misingi rahisi ya saikolojia. Hata hivyo, pamoja na kufahamika kijuu juu, bado nafasi ya saikolojia haijaanza kutambulika ipasavyo katika jamii. Bahati mbaya, uelewa potofu wa sayansi ya tabia, yaani saikolojia, ndio unaochukua nafasi na hivyo kuweza kuleta madhara makubwa jamii.

Kwa mfano, ushauri wa kimahusiano unaotolewa kwenye vyombo vingi vya habari, mara nyingi umejikita kwenye uzoefu binafsi anaokuwa nao 'mshauri' husika ambao si lazima ufanye kazi katika mukhtadha (contexts) mwingine. Ni hatari kuamini uzoefu wangu katika jambo fulani unaweza kutumika katika mazingira mengine kwa mtu mwingine. Tunapokuwa na watu wanaozungumza mambo yenye mwelekeo wa 'saikolojia' katika kujaribu kujibu matatizo ya jamii lakini yasiyokuwa na msingi wa kanuni halisi za saikolojia kisayansi, athari zake zaweza kuwa kubwa na hatari sana.

Pamoja na changamoto hizo, bado ni wazi kuwa elimu hii ikitolewa ipasavyo, na watu wenye uelewa sahihi, changamoto nyingi katika jamii zenye asili yake katika tabia, mitazamo na imani hasi zinaweza kutatuliwa na hivyo watu kuwa na fursa ya kujiletea maendeleo yao.

Mwandishi wa makala haya ni Mhadhiri Msaidizi wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Ana shahada ya Uzamili ya Saikolojia Tumizi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mawasiliano: bwaya@mwecau.ac.tz 

Maoni

  1. Hongera sana kwa elimu nzuri. Navyoelewa uzoefu ni elimu kubwa sana ambayo uwezi kuipuuza. Maana hata mwana saikolojia anautumia kuelewa mambo, hivyo hitimisho lako Mwl, lingesema wazi tu kuwa ushauri utolewe na wanasaikojia. Ingawa kwangu mimi kama anayetoa ushauri anauzoefu na eneo hilo atoe tu. Naeshimu pia taaluma za watu

    JibuFuta

Chapisha Maoni

Zilisomwa zaidi wiki hii...

Mambo Yanayoweza Kugusa Moyo wa Mwanamke-1

Maana ya Saikolojia na Nafasi Yake Katika Jamii -1

Mambo ya Kuzingatia Unapoandika Wasifu wa Kazi (Curriculum Vitae)

Mbinu za Kushinda Maswali ya Usaili wa Kazi - 1

Zijue Tabia Nne za Kiongozi Bora Kazini

Ukuaji wa Kiakili na Kimwili kwa Mtoto wa Miaka 0 – 3